Tafuta

Mkutano mkuu wa Tatu wa Baraza hili la Kipapa unaonogeshwa na kauli mbiu: “Viungo vyote lazima viundwe ili kufanana na Kristo Yesu, hata yeye aumbike ndani yao” (Gal 4:19) Mkutano mkuu wa Tatu wa Baraza hili la Kipapa unaonogeshwa na kauli mbiu: “Viungo vyote lazima viundwe ili kufanana na Kristo Yesu, hata yeye aumbike ndani yao” (Gal 4:19)   (@Vatican Media)

Mkutano Mkuu wa Baraza la Kipapa La Walei, Familia Na Maisha: 2026

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake elekezi katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Tatu wa Baraza hili la Kipapa unaonogeshwa na kauli mbiu: “Viungo vyote lazima viundwe ili kufanana na Kristo Yesu, hata yeye aumbike ndani yao” (Gal 4:19) anakazia kuhusu malezi ya waamini walei katika maisha ya Kikristo na uzoefu wa maadhimisho ya mikutano ya Kimataifa.: Vijana, Familia na Wazee!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Ili kuweza kukabiliana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko kunako 15 Agosti 2016 katika barua yake binafsi, “Motu Proprio” “Sedula mater” alianzisha Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kama sehemu ya mchakato wa Sekretarieti kuu ya Vatican kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha na weledi mkubwa changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu katika barua hii anasema, Mama Kanisa, mwingi wa huruma na mapendo, katika historia ya maisha na utume wake, amekuwa karibu sana kwa waamini walei, familia pamoja na kuhimiza Injili ya uhai, kama kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa walimwengu. Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa waamini walei katika maisha na utume wake, kwani hawa wamepewa changamoto ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Majiundo na Malezi ya Kikristo kwa Waamini Walei
Majiundo na Malezi ya Kikristo kwa Waamini Walei   (@Vatican Media)

Baraza linawahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanalitegemeza Kanisa kwa karama na mapaji yao sanjari na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini walei watambue: dhamana, wajibu na haki zao msingi ndani ya Kanisa. Vyama na mashirika ya kitume ni muhimu sana katika kufunda, kulea, kukuza na kudumisha imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baraza liko mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha utume wa vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba, vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa leo na kwa siku za usoni. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake elekezi katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Tatu wa Baraza hili la Kipapa unaonogeshwa na kauli mbiu: “Viungo vyote lazima viundwe ili kufanana na Kristo Yesu, hata yeye aumbike ndani yao” (Gal 4:19) anakazia kuhusu malezi ya waamini walei katika maisha ya Kikristo na uzoefu wa maadhimisho ya mikutano ya Kimataifa.

Injili ya Uhai Dhidi ya Utamaduni wa Kifo
Injili ya Uhai Dhidi ya Utamaduni wa Kifo   (@Vatican Media)

Huu ni mkutano unaojikita katika kupembua mambo makuu katika maisha na utume wa Kanisa kama ambavyo yamebainishwa kwenye Katiba ya Kitume ya Papa Francisko: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Mkutano huu, ambao umefunguliwa Jumatano tarehe 4 Februari utafungwa rasmi tarehe 6 Februari 2026. Unajadili pamoja na mambo mengine: Utume wa waamini walei katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Umuhimu wa Injili ya maisha; Mwongozo wa Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni kwenye Makanisa Mahalia, Hija za Kitume za Maaskofu Mahalia mjini Vatican sanjari na umuhimu wa malezi na majiundo ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu: Katekisimu, Maisha ya Kisakramenti, Liturujia, Maisha ya Sala, Neno la Mungu na Huduma ya Upendo mintarafu malezi na majiundo ya Kiimani. Hii ni changamoto kwa Makanisa mahalia kuhakikisha kwamba, imani inapandikizwa, inapaliliwa na kudumishwa. Maaskofu mahalia waweke sera na mbinu mkakati wa malezi na makuzi ya imani kwa kukazia mambo msingi katika imani ya Kikristo.

Malezi na Majiundo Makini ya Imani kwa Waamini Walei Ni Muhimu
Malezi na Majiundo Makini ya Imani kwa Waamini Walei Ni Muhimu   (@Vatican Media)

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linapania kuibua Mwongozo wa Malezi na Majiundo ya Waamini Walei katika maisha na utume wa Kanisa. Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni yanafanya kumbukizi ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwake. Mikutano ya Familia Kimataifa imekwisha kuadhimishwa katika kipindi cha Miaka 32.Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na ukahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Siku ya Mababu, Mabibi na Wazee ni muda wa kuserebuka, kutoa faraja na kuonesha upendo kwa wazee, ili kujenga na kudumisha: Umoja, udugu, upendo na faraja tunu msingi katika maisha ya kijamii. Maadhimisho yote haya ni sera na mikakati ya shughuli za: Kichungaji na Kikanisa yanayopaswa kupyaishwa, kwa kusoma alama za nyakati, sanjari na mchakato wa uinjilishaji, ili kweli yaweze kuwa ni chemchemi ya neema na baraka inayodumu katika sakafu ya nyoyo za waamini, yaani ziwe ni siku kwa waamini hawa kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Kumbe, mkutano huu unalenga kutoa mchango mkubwa kwa Baraza, Baba Mtakatifu Leo XIV na Kanisa katika ujumla wake, kwa kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kikanisa.

Baraza la Kipapa
04 Februari 2026, 16:13