Kardinali Pengo Alikuwa Mzee Mahiri, Mwenye Msimamo, Mpenda Haki Na Amani
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Napoli, Italia.
Mama Kanisa katika Utanguzi wa II wa wafu anaeleza kuwa tunasikitika kwa sababu tunajua kwamba tutakufa, lakini hata hivyo tunafarijiwa kwa ahadi ya uzima wa milele na ya kwamba “uzima wa waamini hauondolewi ila unageuzwa tu” na tena “tunapata makao ya milele, yakiisha bomolewa makao ya hapa duniani.” Kwa maneno haya ya Mama Kanisa mwanadamu anapatiwa uhakika wa maisha baada ya kifo, ambapo anakutana na Muumba wake baada ya kuhitimisha maisha na utume wake katika hija ya duniani. Bwana Wetu Yesu msalabani anatupatia maana zaidi ya kifo pale ambapo anatamka kwamba anaikabidhi roho yake katika mikono ya Baba yake na kisha kuinamisha kichwa na kukata roho. Na hivyo kwa muamini Mkristo, kifo ni tendo la kukabidhi roho yake mikononi mwa Mungu Baba yake. Ni katika uelewa huo mpana wa kifo Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam “alikabidhi roho yake mikononi mwa Mungu Baba yake” mnamo Februari 19, 2026 majira ya saa 4:00 usiku katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, (JKCI) Jijini Dar es Salaam. Kama ambavyo kifo kinasikitisha, ndivyo pia Maaskofu wenzake wanavyoendelea kusikitika kwa kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo huku wakiendelea kumuombea huruma ya Mungu na wakijawa imani na matumaini katika ufufuko wa wafu.
Ni katika muktadha huo Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza anaeleza kusikitishwa kwake na taarifa ya kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Askofu Nkwande anaeleza kuwa alianza kumfahamu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wakati Kardinali Pengo akiwa Padre na yeye Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande akiwa mwanafunzi katika Seminari ya Mtakatifu Pio X Makoko Jimbo Katoliki la Musoma ambapo Pengo alifika mara kwa mara kumsalimu Askofu wa Jimbo la Musoma wakati huo Hayati Anthony Petro Mayala. Hata hivyo, Askofu Nkwande anaeleza kuwa alimfahamu kwa ukaribu zaidi Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo baada ya yeye kuwa Askofu wa Bunda mwaka 2011 na hivyo kufanya naye kazi kwa karibu zaidi katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambapo Mwadhama Pengo, akiwa miongoni mwa wazee, aliwasaidia kuwaonesha njia na kuwaelekeza namna ya kuishi kama Maaskofu na zaidi namna ya kuishi na waamini. Askofu Nkwande anasema Mwadhama Kardinali Pengo “alikuwa Mzee mahiri, Mwenye msimamo na alipenda haki na amani itendeke” na hivyo kuwafundisha Maaskofu wenzake kutenda haki na ya kwamba hakukaa kimya pale Maaskofu wenzake walipokosea au walipokwenda kinyume na kile ambacho yeye aliamini ni sawa.
Sanjari na hayo, Askofu Nkwande anamkumbuka sana Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa kuhusika kwa karibu sana katika maandalizi ya ziara ya ujio wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania mwaka 1990 akiwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Askofu Nkwande anamkumbuka Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa jinsi alivyoipenda Seminari Kuu ya Segerea na jinsi alivyowatia moyo waseminari kwa kuwataka wawe na moyo mkuu, hasa nyakati ya changamoto za wito. Mwadhama Kardinali Pengo ndiye Gambera wa kwanza kabisa wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Karol Lwanga Segerea, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam. Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Optatam totius” Juu ya Malezi ya Waseminaristi linasistiza kuwa Mapadre wote wanatakiwa kuiona seminari kama ndiyo moyo halisi wa jimbo na kuitegemeza kwa hiari. OT, n 5.
Ikumbukwe kwamba Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ndiye aliyemweka wakfu na kumsimika Mhashamu Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Bunda mnamo tarehe 20 Februari 2011 akisaidiana na Askofu Mkuu Juda Thaddaeus Ruwa’ichi OFMCap, akiwa Askofu Mkuu wa Mwanza nyakati hizo, na Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma. Askofu Mkuu Nkwande anawasihi waamini wa Jimbo Kuu Katoliki Mwanza kumsindikiza Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kwa sala na hata kuwaomba waamini wanaoweza kwenda kushiriki mazishi yake. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo anatarajiwa kuzikwa Jumamosi Februari 28, 2026 katika eneo la Kituo cha Hija la Pugu, mahali ambapo yeye mwenyewe alipachagua na kutayarisha kaburi. Mwadhama alichagua kuzikwa Dar es Salaam kwa kuwa sehemu kubwa ya utumishi wake kama Askofu amefanya katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam na ya kwamba angependa kuzikwa Pugu ili alale mahali ambapo Wamissionari wa kwanza walioinjilisha Dar es Salaam wamezikwa.