Rais Petr Pavel wa Jamhuri ya Watu wa Czech Akutana na Papa Leo XIV Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 19 Januari 2026 amekutana na kuzungumza na Bwana Petr Pavel, Rais wa Jamhuri ya watu wa Czech, ambaye baadaye alipata nafasi ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mazungumzo na mgeni wake, wamerejea kumshukuru Mungu kwa mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili na kwamba, kuna haja ya kuendelea kuyaimarisha zaidi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake.
Baadaye, wamejikita katika masuala ya pamoja mintarafu masuala ya kisiasa na kijamii, kikanda na Kimataifa, hasa zaidi vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta na kudumisha misingi ya haki na amani, kwa kukazia tunu msingi za maisha zitakazoiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuishi kwa amani na utulivu zaidi.