Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu.   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli Kitaifa Jimbo Katoliki Kigoma 2025

Askofu Mlola amesema kuwa wakati Wakristo duniani kote wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, ni vyema Sherehe hizo ziambatane na mabadiliko ya maisha kwa Watanzania ili kuondokana na mambo yaliyojitokeza katika jamii na hatimaye waweze kuishi kwa: haki, amani, upendo, mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kuheshimiana kama wamoja. “Tuwe tayari kuzika tofauti zetu. Tubaki katika tunu zetu. Mungu ametuheshimisha, akatupenda upeo na anataka...

Na Daniel Msangya, Kigoma, Tanzania.

Noeli ni chemchemi ya Injili ya matumaini na furaha ya kweli; ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu na utume unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo. Tafakari ya Fumbo la Umwilisho, Neno aliyefanyika mwili inatia moyo neno jipya na la kweli katika Kanisa lote kwa kuwataka waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Noeli, ambayo ni adhimisho la fumbo la imani, mapendo na matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Ni sherehe ya matumaini, kwa sababu Mtoto Yesu anawasha tena matumaini ndani ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa ni vyombo na wajumbe wa amani. Wakiwa wamesheheni fadhila hizi nyoyoni mwao, kamwe hawawezi kuogopa usiku na kwamba, wanaweza kukabiliana kikamilifu na changamoto ya mapambazuko ya siku mpya. Hekima, umoja na amani ni ngao muhimu za watanzania mahali popote pale walipo, ili kuweza kudumisha uhuru na umoja, upendo, udugu na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Haki, umoja na amani ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa; haki na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu. Moja kati ya mahubiri ya kusisimua yaliyotolewa kwa lugha ya ushairi, hekima na uteuzi wa maneno ilihitimisha Noeli ya Bwana kwa mwaka 2025 katika kilele cha maadhimisho ya misa ya Noeli iliyofanyika kitaifa katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mshindaji la Jimbo Katoliki la Kigoma.

Noeli iwe ni fursa ya kuzika tofauti, kwa kujikita katika tunu msingi za kijamii
Noeli iwe ni fursa ya kuzika tofauti, kwa kujikita katika tunu msingi za kijamii   (AFP or licensors)

Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma alitumia maadhimisho hayo kutoa wito kama chachu ya kuzika tofauti za kidini na kiitikadi ili kujenga Kanisa na Taifa kwa ujumla. Askofu Mlola amesema kuwa wakati Wakristo duniani kote wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, ni vyema Sherehe hizo ziambatane na mabadiliko ya maisha kwa Watanzania ili kuondokana na mambo yaliyojitokeza katika jamii na hatimaye, waweze kuishi kwa: haki, amani, upendo, mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kuheshimiana kama wamoja. “Tuwe tayari kuzika tofauti zetu. Tubaki katika tunu zetu. Mungu ametuheshimisha, akatupenda sana, akatupenda mno, akatupenda upeo na anataka tufanane naye. Basi, tupendane tuwe tayari kuzika tofauti zetu kwa kuhakikisha tunang’oa visababishi vya kutofanana naye. Ukatili, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada za uongo, uchawi, hasira, fitina, uzushi, husuda, ulevi na ulafi.” Askofu Mlola alisisitiza mshikamano akihimiza waamini kushikamana katika Kristo, “tushikane na yale ya kiroho yanayotupeleka katika uzima, upendo, haki, amani, furaha, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.” Alisema, kuishi vizuri na Mungu ni kuwapenda jirani na kwamba, ili kumpenda Mungu tunaanza na jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ambaye Yesu mwana wa Mungu amekuja kudhihirisha hilo. “…tuishi kanuni ya dhahabu katika maisha yetu, naomba mlipokee na kulifanyia kazi katika Noeli hii, usimtendee mwenzako kile usichopenda kutendewa, kama unaona maisha yako yana thamani na unayapenda basi usifikirie kumdhuru mwingine, unapenda nyumba yako ibaki salama, usijiingize kuharibu nyumba ya wengine, kama unapenda upendwe – upende wengine, unapenda utendewe haki; utende haki kwa wengine, tambua pale inapoishia haki yako inaanza haki ya mwingine; hakuna sababu wala  haki ya kukanyaga haki ya wengine.”

Askofu Joseph Roman Mlola ameongoza Ibada ya Sherehe ya Noeli 2025
Askofu Joseph Roman Mlola ameongoza Ibada ya Sherehe ya Noeli 2025   (Jugo Media)

Askofu Mlolaa lihimiza unyenyekevu, “tujinyenyekeze kila mmoja aliye mkubwa kwa umri au madaraka au mdogo kwa umri, ulimwengu huu utakuwa mahali pazuri sana pa kuishi, kuheshimiana, kukutana na kutatua yasiyompendeza Mungu wala jirani, hakutakuwa na chuki, hakutakuwa na kukosa haki na amani, hakutakuwa na sababu ya malumbano kati ya jamii na katika itikadi mbalimbali za watu. Yesu amekuja, anaishi nasi na huonekana katika maisha yetu, kati ya maskini wanaoihitaji msaada, wagonjwa wanaohitaji huduma, vijana wanaohitaji kusikiliszwa katika hofu na mahangaika yao ya maisha, wazee wa umri wanaohitaji heshima na matunzo, familia zinazopitia changamoto na magumu ya kiuchumi na maisha kiujumla, hawa ndio ambao tunapaswa kuwahudumia, hawa ndio Yesu aliposema; ulipomhudumia mmojawapo wa wadogo ulinihudumia mimi, tusikae mbali na baraka hizi. Haya ndiyo yanayotufanya tuingie kule mbinguni. Wale waliotenda haya wamepata nafasi ya kufika kwake mbinguni, wale waliomkanyaga tu, hawasikilizi hata kama wanayo madaraka na nafasi lakini hawakutimiza wajibu wao, mahala pao panafahamika tusipatafute hapo.” Askofu Joseph Mlola alisema Yesu aliye nuru na mwanga wa Ulimwengu alikuja ulimweguni awaangazie watu katika njia ya kwenda mbinguni. Mtoto Yesu ni kiini cha matumaini, kiini cha haki na amani, licha ya kuzaliwa katika hali na mazingira duni, Kristo Yesu ni nuru ya mataifa, kielelezo cha ukweli wa  Kimungu, chachu ya mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu kama anavyosimulia Mtakatifu  Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho juu ya hekima na busara ya Kimungu akisema bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia ili awaabishe wenye hekima tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu, tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa naam, vitu ambavyo havipo ili avibatilishe vile vilivyopo. Mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele ya Mungu (Rej 1Wakor1:27-29).

Haki, Umoja na Amani ni nyenzo msingi wa maendeleo fungamani.
Haki, Umoja na Amani ni nyenzo msingi wa maendeleo fungamani.

Askofu Mlola alisema Kristo Yesu amekuja ili tusamehewe dhambi zetu, amekuja ili kutuondolea huzuni zetu, amekuja ili kutusafisha mioyo yetu, kutukomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti; kutoka katika utumwa wa Shetani kwa gharama ya uhai wake. “Amekuja kuwaganga wale walio hawawezi, walio wagonjwa, waliovunjika na kupondeka moyo; kwa hiyo nasi tunaalikwa, tulio wafuasi wake Kristo Yesu, kumpa moyo wako uliojaa tamaa za makuu ya dunia kupita kiasi, ili upate moyo wa kuona mahitaji ya wengine. Anakualika umpe moyo wako uliojaa tamaa za mali, uliojaa uchu wa madaraka. Mruhusu aingie ndani yako, ndani ya moyo wako uliojaa tamaa za mwili na kusahau yale yanayokupa uzima, yale ya kiroho. Haya yanawezekana tu pale utakapojinyenyekesha mbele za Mungu kama Mtoto Yesu alivyonyenyekea, hakung’ang’ania Umungu wake, akakubali kujishusha na kuwa kama sisi. Nasi tujinyenyekeshe mbele za Mungu kwa njia ya sala ambazo ni njia pekee za kuzungumza na Muumba wetu. Mtoto aliyezaliwa na kukaa kwetu; Mungu Nafsi ya Pili, anatualika tujifunze kwake ili tufanane naye tupate nasi kuzaliwa upya. Katika maisha yetu, kiasi cha kujaliwa nasi kuushiriki Umungu wake; kama tulivyosali katika sala. Yeye amekubali kushiriki ubinadamu wetu akubali kutushirikisha Umungu wake. Anatualika tuongozwe na hekima ya Kimungu, katika maisha yetu tujue kuyatenda yaliyo mema na kuyaacha yaliyo mabaya yasiyompendeza Mungu wala Mwanadamu.

Askofu Mlola: Unyenyekevu ni msingi wa ujenzi wa haki na amani
Askofu Mlola: Unyenyekevu ni msingi wa ujenzi wa haki na amani

Bahati mbaya katika nyakati zetu hizi, anasema Askofu Mlola, watu wanakimbilia maovu zaidi kuliko yale yaliyo mema. Mungu anakuja kukaa kwetu anazaliwa katika hali yetu ya kibinadamu ila Yeye hakuwa na dhambi. Anatufundisha kutambua thamani kubwa ya zawadi aliyotukirimia ya uhai ambayo ni Mungu pekee mwenye mamlaka nayo. Naye akachukuwa mwili amezaliwa kama sisi na kuyapa heshima kubwa maisha, na uhai wa binadamu. Mtu yeyote asiote ndoto iwe ya mchana au usiku katika maisha yake au kufikiria tu kuutoa uhai wa mwenzake au hata wake mwenyewe bali ni mali ya Mungu; kimsingi si mwili wake ni mali ya Mungu. Mwenye mamlaka ya uhai yupo, tusijitwalie jukumu lisilotuhusu na tuwe na hofu ya Mungu maishani mwetu. Askofu Joseph Mlola aliweka msisitizo katika uhai wa mtu akifafanua kuwa unaanza tangu kutungwa mimba mpaka Mungu mwenyewe atakapoamua kuutoa. “Kufikiri na kutenda kinyume na ukweli huo ni kukosa hekima inayotudai kuchagua yaliyo mema na ya Kimungu na kuacha yaliyo mabaya ya yule mwovu.  Hekima ambayo ni Mungu mwenyewe ambaye amejishusha na hata kuchukuwa mwili na kuzaliwa na mwanamke ili kutukomboa sisi wanadamu wadhambi. Kuzaliwa kwa Mtoto Yesu kutukumbushe wajibu wa kila mmoja wetu wa kulinda na kuheshimu uhai, tulinde haki ya kila mmoja wetu kuishi, ni haki msingi, kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu amuombe Mtoto Yesu aliyezaliwa kati yetu na ambaye ni Mfalme wa haki na amani, ni mshauri wa ajabu, atuletee amani mioyoni mwetu, katika familia zetu, jumuiya zetu na katika taifa letu. Ili kazi aliyokuja kuifanya hapa duniani ionekane popote pale katika ulimwengu mzima.” 

Fumbo la Umwilisho ni chemchemi ya: Imani, furaha, amani na upendo
Fumbo la Umwilisho ni chemchemi ya: Imani, furaha, amani na upendo   (Vatican Media)

Kwa mujibu wa Askofu Mlola; Imanueli, yaani “Mungu pamoja nasi” maana yake ni Mungu pamoja nasi katika maumivu yetu, umaskini wetu, mahangaiko na matumaini yetu, kwamba, amekuja katikati yetu ili tumtumainie na kumkimbilia (Zaburi 33:21), katika Waraka wake Paulo kwa Warumi amesisitiza kuwa Mungu ni Tumaini awajaze furaha na amani mpate kuzidi kuwa na nguvu (Warumi15:13.) Noeli ya mwaka 2025, kwa mujibu wa Askofu Mlola ni mwanzo mpya wa maisha na kwamba hili siyo jambo la kurudia au mazoea bali tuwe viumbe wapya na kubadilisha maisha yetu kwa kuthamini utu wetu na miili yetu kwani imetolewa na Mungu na kwamba miili yetu ni mahekalu ya Roho Mtakatifu hivyo itumike kwa makausudio ya Mungu na kadri inavyompendeza Mungu. Kwani amethamini utu wetu na kutwaa mwili kama sisi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kuhusu mavazi Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma alisema, hata Kristo Yesu alivalishwa nguo za kitoto lakini katika nyakati hizi hakuna heshima katika uvaaji kwa kadri inavyompendeza Mungu. Mavazi ambayo ni sehemu muhimi siku hizi yanavaliwa kinyume na baadhi ya vijana kwa kushindwa kuiga mazuri. “Tusiige kila kitu kama dodoki, likiingia kwenye maji linachukuwa kila kitu bali tubaki katika tunu zetu kuendena na desturi zetu njema za Kiafrika. Alitoa mfano wa mavazi yanayofungiwa karibu na magoti na kuonya miaka ijayo tutazivuta chini kwani suruari sasa zinazofungiwa kwenye magoti badala ya kusetiri maungo ya binadamu.

Noeli 2025 Tanzania
05 Januari 2026, 15:08