Tafuta

Mbele ya  Bunge la Ulaya kuna Bendera za Nchi Wanachama wa Ulaya. Mbele ya Bunge la Ulaya kuna Bendera za Nchi Wanachama wa Ulaya. 

Luxembourg,Maadili ya Kikatoliki na Ujenzi wa Amani barani Ulaya

Mfuko wa Kipapa wa Centesimus Annus Pro-Pontefice,COMECE,na Shule ya Dini na Jamii ya Luxembourg wameandaa mkutano utakaofanyika Januari 23.Mada ni pamoja na kukuza diplomasia na ukosefu wa usawa wa kijamii kama sababu za migogoro.Washiriki ni pamoja na maafisa wa EU,wawakilishi wa makanisa ya Kikristo,wataalamu wa kitaaluma,washauri wa sera wanaowakilisha wadau wa taasisi mbalimbali.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Mawazo ya kijamii ya Kikatoliki na maadili ya ulimwengu yanawezaje kuchangia katika kukuza na kujenga amani barani Ulaya? Mada hii itajadiliwa katika mkutano wa Kimataifa wenye kauli mbiu: "Kujenga Amani barani Ulaya: Jukumu Gani la Mawazo ya Kijamii ya Kikatoliki na Maadili ya Ulimwengu?," uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa tarehe 23 Januari 2026, kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni masaa ya Ulaya, huko Luxembourg. Mkutano huo umeandaliwa na Mfuko wa Kipapa wa Centesimus Annus Pro-Pontefice, COMECE (Tume ya Baraza la Maaskofu wa Umoja wa Ulaya), na Shule ya Dini na Jamii ya Luxembourg (LSRS).

Kuzingatia Ujenzi Upya wa Ukraine

Kwa hiyo Mkutano huo,  utazingatia suala la ujenzi wa amani, linaloeleweka kama mchakato wa kimataifa na jumuishi unaojumuisha vipimo vyote vya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kiutamaduni, na uhusiano vinavyohusika katika kujenga amani endelevu. Ingawa mkutano huu ni wa kimataifa, lakini umakini maalum utapewa kwa upande wa Ulaya. Mkutano huu utapangwa katika vikao kadhaa vya mada, kila kimoja kikiwa kimejitolea kwa kipengele maalum cha ujenzi wa amani: kuanzia kukuza mazungumzo na diplomasia hadi ujenzi mpya wa nyenzo na kijamii wa jamii zilizopitia migogoro, huku ukizingatia zaidi ujenzi mpya wa Ukraine.

Mada za Mkutano

Uangalifu maalum pia utapewa kwa mabadiliko kutoka uchumi wa vita hadi uchumi unaozingatia amani, kuchambua jinsi sera za kiuchumi na vyombo vya kifedha vinavyoweza kusaidia kupona, ustahimilivu, na utulivu wa muda mrefu. Vikao hivyo pia vitashughulikia changamoto ya ukosefu wa usawa wa kijamii, kutambua jukumu lao kama vichocheo vya migogoro na kama vikwazo vya amani endelevu, ili kupanga njia kuelekea haki na ujumuishaji mkubwa wa kijamii. Majadiliano pia yataakisi jukumu la ujumuishaji wa Ulaya kama mpango wa kujenga amani, kwa kuzingatia jinsi upanuzi, ushirikiano, na maadili ya pamoja yanaweza kuchangia maridhiano, kujenga uaminifu, na uimarishaji wa taasisi za kidemokrasia barani kote.

Mkutano huo utawaleta pamoja maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya, wawakilishi wa Makanisa ya Kikristo, Wabunge wa Bunge la Ulaya, wataalamu wa kitaaluma, washauri wa sera wanaowakilisha wadau mbalimbali, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, wachumi, na viongozi wa biashara. Hafla hiyo pia itajumuisha jumbe za video kutoka kwa Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, pamoja na wawakilishi wengine wa ngazi ya juu wa taasisi za Uomoja wa Ulaya(EU.)

Usajili na ushiriki mtandaoni

Mkutano huo utafanyika katika Shule ya Dini na Jamii ya Luxembourg (LSRS), Kituo cha Yohane XXIII, 52, (rue Jules Wilhelm, L-2728 Luxembourg.).Kabla ya kuanza Mkutano huo, itatanguliwa na Maadhimisho ya  Misa  saa 2:00 asubuhi, na mkutano utaanza saa 3:00 kamili asubuhi majira ya Ulaya. Mkutano huo utafanyika kwa Kiingereza na Kifaransa.

Ushiriki utawezekana mtandaoni, kwani tukio hilo litarushwa moja kwa moja. Taarifa za utiririshaji zitawasilishwa baada ya usajili. Usajili ni wa lazima na unaweza kufanywa sasa kupitia:https://www.lsrs.lu/fr/news/centesimus-annus-pro-pontifice-foundation-european-conference-2. Programu kamili ya mkutano inapatikana kwenye Tofuti ya Mfuko wa Kipapa wa Centesmus annus,bonyeza hapa:www.centesimusannus.org

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

 

21 Januari 2026, 11:11