Tafuta

Kardinali Parolin,Katibu wa Vatican ndani ya Kanisa Kuu la Brussels wakati wa maadhimisho ya miaka 800 tangu kujengawa kwake. Kardinali Parolin,Katibu wa Vatican ndani ya Kanisa Kuu la Brussels wakati wa maadhimisho ya miaka 800 tangu kujengawa kwake.  (©Tommy Scholtes, sj)

Kard,Parolin:Ukristo hautoi suluhisho za kiufundi,bali unapendekeza maadili ya kibinadamu!

Kardinali Parolin,Katibu wa Vatican aliongoza Ibada ya Misa Takatifu katika maadhimisho ya miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels,tarehe 11 Januari 2026.Katika mahubiru yake alisema:“Ulaya kwa sasa inakabiliwa na kipindi kilichojaa udhaifu,hofu,na migawanyiko ambayo si ya kisiasa au kijamii tu,bali pia ya ndani na kiutamaduni,matatizo ambayo yanadhoofisha mizizi yake.Katika muktadha huu,Ukristo hautoi suluhisho za kiufundi,bali ni maadili muhimu ya kibinadamu.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

“Ikiwa Ulaya itafungua tena milango yake kwa Kristo haitaogopa kuokoa mipaka ya nchi,mifumo ya kiuchumi pamoja na mifumo ya kisiasa,nyanja kubwa za utamaduni,ustaarabu,na maendeleo, mustakabali wake hautabaki kutawaliwa na kutokuwa na uhakika na hofu,bali utafunguka kwenye msimu mpya wa maisha wa ndani na wa nje,wenye manufaa na uamuzi kwa ulimwengu mzima bado unaotishiwa na mawingu ya vita na kimbunga kinachowezekana cha maangamizi ya kinyuklia.” Haya yalisikika ndani ya Mahubiri ya Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican wakati wa kuongoza  Ibada ya Misa Takatifu, Dominika tarehe 11 Januari 2026 kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels nchini Ubelgiji. Katika mahubiri yake alionesha awali ya yote alifurahi kuongoza sherehe hiyo ya Ekaristi katika Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, ambayo ilihitimisha kipindi cha Noeli na sambamba na hafla ya kuadhimisha miaka mia nane ya Kanisa kuu hilo.

Kardinali Parolin akiadhimisha misa ya  maadhimisho ya miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels
Kardinali Parolin akiadhimisha misa ya maadhimisho ya miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels

Salamu za Papa na shukrani za makaribisho

Kardinali Parolin alilitoa  salamu za dhati na ukaribu wa kiroho za Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye, katika hafla hiyo, alitaka kuelezea kwa njia maalum ushirika wake na Kanisa hilo na nchi hiyo kwa kumteua kuwa Mwakilishi wwake. Aliwasalimia kwa heshima Wakuu wao Mfalme na Malkia, na Nyumba ya Kifalme, akiwashukuru kwa uwepo wao, ishara ya uhusiano wa kihistoria wenye heshima na matunda kati ya maisha ya Kanisa na maisha ya kitaasisi ya Ubelgiji. Kadhalika alimsalimia kwa dhati Kardinali Jozef De Kesel, Askofu Mkuu wa Mechelen-Brussels, Askofu Mkuu Luc Terlinden, na alimshukuru kwa makaribisho yake na kwa huduma ya kichungaji ambayo anaongoza Kanisa hilo. Pamoja naye salamu zaliwaendea Maaskofu waliokuwapo, mapadra makuhani, mashemasi, watu waliowekwa wakfu,na watu wote wa Mungu waliokusanyika hapo. Ushiriki wa mamlaka za kiraia na za kikanisa, na waamini wengi, ambao waliipatia  wakati huo umuhimu unaozidi kumbu kumbu yenyewe na kutoa mwaliko wa kutambua umuhimu wake wa kikanisa, kihistoria na kiroho.

Imani ya kikristo haipo nje

Kardinali Parolin kadhalika alianza kuzungumza kwa Lugha ya kiingereza kuwa, “Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, inayoadhimishwa mahali hapa penye historia nyingi, inatuweka mbele yetu ukweli muhimu: imani ya Kikristo haipo nje ya wakati au pembezoni mwa historia, lakini hukua ndani yake, katika maeneo halisi na kupitia jamii halisi. Hapo, kwenye kilima hicho imani ilichukua mizizi muda mrefu kabla ya jengo tunalolipenda leo hii. Kuanzia Kanisa la awali lililowekwa wakfu kwa Mtakatifu Mikaeli hadi kanisa la Kirumi, na hatimaye mwanzo wa jengo kubwa la Kigothic katika karne ya kumi na tatu,  hatua hizi zinaashiria safari ndefu na ya subira. Hili ni ukweli wa wazi: Kanisa halizaliwi kutokana na tendo moja la pekee au mpango uliokamilika kwa wakati mmoja tu, bali kutokana na uaminifu unaoenea vizazi, ambapo kila mtu hupokea, hulinda na kushika kile alichokabidhiwa. Kwa karne nane, Kanisa Kuu hili limeshuhudia na kusindikiza maisha ya Kikristo ya jiji, na ya nchi, kupitia vipindi tofauti sana. Miundo yake ya usanifu na kisanii huhifadhi kumbukumbu ya imani ambayo haikuepuka maswali ya wakati wake, lakini ilijaribu kuishi ndani yake, ikikubali kazi inayohitaji utambuzi na uongofu.”

Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels
Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels   (ANSA)

Watakatifu wanazungumziza wito wa Kikanisa

Katibu Mkuu wa Vatican alisisitiza kuwa “Watakatifu walinzi wenyewe huzungumzia wito huu wa kikanisa. Mtakatifu Mikaeli anatualika kuwa makini na utambuzi, huku Mtakatifu Gudula akitukumbusha kwamba imani hukua kupitia uaminifu wa kila siku. Kwa pamoja, wanaelekeza kwenye Kanisa lililoitwa kuishi pamoja ukweli na huduma, uimara na upole. Historia ndefu kama hiyo haizuii mitazamo yetu kutazama yaliyopita, bali inayafungua kwenye wakati ujao; haialiki kumbukumbu za zamani, bali matumaini. Kutoka katika Kanisa Kuu hili, lililopo katikati ya Brussels, mitazamo ya macho yetu inafunguka kuelekea Ulaya. Sio kwa bahati mbaya kwamba jiji hili limekuwa mojawapo ya maeneo ambapo Ulaya inatafuta kufikiria upya na kujijenga: njia panda ya watu, lugha na tamaduni, zinazojulikana kwa utamaduni wa mazungumzo na upatanisho. Brussels inatukumbusha kwamba Ulaya imezaliwa kutokana na kukutana na uwezo wa kukumbatia  tofauti pamoja.”

Ulaya inakabilia na kipindi cha udhaifu, hofu na migawanyiko

Na tena Kardinali Parolin aliendelea na lugha ya kifaransa akisema: “Ulaya kwa sasa inakabiliwa na kipindi kilichojaa udhaifu, hofu, na migawanyiko ambayo si ya kisiasa au kijamii tu, bali pia ya ndani na kitamaduni—matatizo ambayo yanadhoofisha mizizi yake. Katika muktadha huu, Ukristo hautoi suluhisho za kiufundi, bali ni maadili muhimu ya kibinadamu: Inatukumbusha kwamba heshima ya mtu hutangulia hesabu zote, kwamba haki hukua kwa kujumuisha na si kwa kutenganisha, kwamba amani huzaliwa kutokana na utambuzi wa mwingine na si kutokana na usawa wa hofu. Hili ni pendekezo rahisi lakini lenye uamuzi, ambalo halitafuti kujilazimisha, bali kuelimisha dhamiri.

Kardinali wakati wa misa huki Brussels
Kardinali wakati wa misa huki Brussels

Katika muktadha wa kihistoria tunaopitia sasa, inaonekana kama unabii kurudia wito uliotolewa katika Madhabahu ya Santiago de Compostela na Mtakatifu Yohane Paul II mnamo tarehe 9 Novemba 1982, ambao ni muhimu zaidi leo hii kuliko hapo awali: "Ikiwa Ulaya itafungua milango yake kwa Kristo tena na haitaogopa kufungua kwa nguvu yake ya kuokoa mipaka ya nchi, mifumo ya kiuchumi pamoja na mifumo ya kisiasa, nyanja kubwa za utamaduni, ustaarabu, na maendeleo, mustakabali wake hautabaki kutawaliwa na kutokuwa na uhakika na hofu, bali utafunguka kwenye msimu mpya maisha, ya ndani na  nje, wenye manufaa na uamuzi kwa ulimwengu mzima, ambao bado unaotishiwa na mawingu ya vita na kimbunga kinachowezekana cha maangamizi ya nyuklia."

Kardinali Parolin alibainisha kuhusu hili kwamba: “Maono haya yalichukua sura katika historia halisi ya Ulaya, shukrani kwa wanaume kama  vile Robert Schuman, Konrad Adenauer, na Alcide De Gasperi, ambao waliweza kufikiria bara si kama muungano wa maslahi tu, bali kama jumuiya iliyoanzishwa juu ya upatanisho na ukuu wa mtu binafsi na manufaa ya wote. Walielewa kwamba baada ya mipasuko ya historia, ilikuwa muhimu kujenga upya si tu miundo, bali pia kuaminiana. Ni katika muktadha huu ambapo moja ya changamoto muhimu zaidi kwa Kanisa leo hutokea. Sio tu kuwa wachache kwa idadi, hali ambayo mara nyingi huambatana na historia ya Kikristo—bali matarajio ya kuwa yasiyo na maana. Sio udhaifu wa idadi unaodhoofisha ushuhuda wa jumuiya ya Kikristo, bali ni kupoteza ujasiri wake wa kiinjili. Kanisa hudhoofika linapoacha kuwa chumvi inayotoa ladha, mwanga unaoangazia, chachu inayofanya mambo yakue.”

Misa ya maadhimisho ya miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels
Misa ya maadhimisho ya miaka 800 ya Kanisa Kuu la Brussels

Kanisa husafiri kupitia hilo na kama uwepo unaosindikiza

Katibu Mkuu wa Vatican, tena kwa lugha ya kiingereza alisema kuwa: “Kanisa halisimami juu ya historia, wala haliungani nayo tu; badala yake, husafiri kupitia hilo kama uwepo unaosindikiza, unaotambua na kutumikia. Mapokeo ya Kikristo yameelezea hili kupitia taswira rahisi lakini zenye nguvu: ni nyumba, kwa sababu Mungu anakaa ndani yake; mwili, kwa sababu Kristo anaendelea kuishi na kutenda kupitia kwake; na watu, kwa sababu hakuna mtu anayesafiri kwa imani peke yake. Kama Mababa walivyotukumbusha, Kanisa ni takatifu kwa sababu ya zawadi inayopokea, lakini dhaifu kwa sababu ya mipaka ya viungo vyake. Kwa sababu hii, haliishi kwa ukamilifu, bali kwa neema; si kwa kujitosheleza, bali kwa ushirika.

Ndani ya safari hii ya Kanisa kupitia wakati, Neno la Mungu linaendelea kujifanya lisikike, si kama ujumbe wa mbali, bali kama sauti inayoingia katika uzima, inayoupa mwelekeo, na kujibu maswali yetu ya ndani kabisa, bila kuyaepuka. Akigeukia masomo, Kardinali Parolin alibainisha kwamba, “Somo la kwanza linatupatia moja ya taswira bora zaidi katika Maandiko yote: Mtumishi wa Bwana. Hajilazimishi, bali hulinda kile kilicho dhaifu; Havunji mwanzi uliopondeka, bali huendelea kuwaka moto unaowaka. Haki yake inakuja kupitia upole na ukaribu, badala ya nguvu inayotawala. Ufunuo huu unafikia utimilifu wake katika Yesu, ambaye anachagua kuingia kikamilifu katika hali ya kibinadamu. Anashuka ndani ya maji ya Yordani si kwa sababu ya hitaji la kibinafsi, bali kushiriki katika kusubiri na uchovu wa wote wanaotafuta wokovu. Anakubali nafasi yake kati ya wenye dhambi, bila kufanya ubaguzi. Ni ishara ya kimya lakini yenye uamuzi. Ni baada tu ya kujinyima huku ndipo mbingu inafunguka na sauti ya Baba inasikika: “Huyu ni Mwanangu mpendwa.” Mpangilio uko wazi: na hauonekani katika kutengana, bali katika kushiriki. Kile kilichotokea katika Yordani kisha kikawa njia ya maisha na utume, kama Matendo ya Mitume yanavyoshuhudia: Kristo alizunguka-zunguka akitenda mema na kuponya wote, bila ubaguzi. Huu ndio umbo la kudumu la uwepo wa Kikristo katika historia.

Ndani ya Kanisa Kuu la Brussels
Ndani ya Kanisa Kuu la Brussels

Mtazamo wa macho yetu kwa Maria:Fumbo la Kristo na Kanisa

Kardinali tena kwa kuendelea kuchanganya lugha hizi mbili kwa kifaransa, alizungumza akisema, “wapendwa kaka na dada, Kifungu hiki cha Injili pia kinazungumzia moja kwa moja maisha yetu. Katika ubatizo, tulizamishwa katika Kristo na kuingizwa katika uhalisia mkuu kuliko sisi wenyewe. Sisi sio wale tunaojenga Kanisa: sisi ndio mawe ambayo Bwana hutumia. Kanisa hukua wakati tofauti zinapokuwa chanzo cha utajiri na wakati upendo ndio kifungo kinacholiunganisha pamoja. Katika safari hii, macho yetu yanamtazama Maria, ambaye Mtaguso wa Pili wa Vatican unamtafakari katika fumbo la Kristo na Kanisa.

Ndani yake, Kanisa linajifunza kwamba kuzaa matunda hakutokani na nguvu ya miundo, bali kutoka kwa uwazi kwa hatua ya Mungu; si kutokana na mwonekano wa haraka, bali kutokana na uaminifu wa subira.” Na hatimaye kwa kuzungumza kiingeza alisema kuwa “Kutoka katika Kanisa Kuu hili, ishara ya imani iliyokomaa kwa karne nyingi, tunainua maombi yetu kwa Bwana kwa ajili ya Kanisa, kwa ajili ya jiji la Brussels, kwa ajili ya Ubelgiji, kwa ajili ya Ulaya na kwa ajili ya jumuiya ya mataifa. Zaidi ya hayo, tuombe kwamba mahali hapa paendelee kuwa nyumba iliyo wazi na nafasi ya ushirika, ambapo Injili huunda dhamiri zenye uwezo wa haki, uwajibikaji na matumaini. Amina. "

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

12 Januari 2026, 11:58