Kard.Fernández:Usiulize mwanga,bali moto,Mungu amewapatia wanadamu uwezo wa kufikiri!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Victor Manuel Fernández alifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ambalo yeye ni Mwenyekiti kwa tafakari ambapo alitoa mwaliko wa unyenyekevu wa kiakili na kiroho. Tukio hilo, lililoanza tarehe 27 hadi 29 Januari 2026 limewakusanya pamoja zaidi ya washiriki 70 waliokusanyika mjini Vatican. Kwa kuongozwa na mada ya “Usiulize kwa Mwanga,” bali kwa moto Kardinali alianza kusema “katika nyakati za mwisho, katika sala nimehisi mwaliko wa nguvu wa unyeyekevu wa kiakili, kwa kukumbuka maneno yale ya kale “Ubi umilitas ibi sapientia,” yaani msemo wa kilatini ukimaanisha “Penye unyenyekevu kuna hekima.” Kwa njia hiyo, Kardinali alipenda kuanza “mkutano guo, katika muktadha huo wa maombi, kwa mwaliko wa unyenyekevu huo wa kiakili.” Mungu amewapatia wanadamu uwezo wa kufikiri, ambao una wigo wa ulimwengu wote: tunaweza kufikiria kuhusu ulimwengu, historia, asili, tunaweza hata kufikiria kuhusu Mungu. Hata hivyo, uwezo huu wa ulimwengu wote wa kufikiri haimaanishi kwamba wanadamu wana uwezo kamili na kamili wa kutambua ukweli.
Hatuna uwezo wa kutafsiri maana zote na unyeti wa uhalisia wa mtu
Hata kwa msaada wa teknolojia zenye nguvu zaidi zinazoweza kufikiwa, haiwezekani kwa akili ya mwanadamu kufahamu ukweli katika ukamilifu wake na katika kila kipengele. Hili linawezekana kwa Mungu pekee. Shida ni kwamba, kwa sababu hiyo, hatuwezi kuwa na uelewa kamili wa hata sehemu ndogo ya ulimwengu huu, kwa sababu sehemu hiyo hiyo inaweza kueleweka kikamilifu tu kwa kuzingatia ukamilifu ambao imeunganishwa: kila kitu kimeunganishwa. Matokeo yake hatuna uwezo wa kutafsiri maana zote na unyeti wa uhalisia, wa mtu, wakati wa kihistoria, na wa ukweli.
Tunahitaji kuelewa aina za vitu na mahusiano yake mengi
Thomas wa Aquino alielezea kwamba utajiri usio na kikomo wa Mungu unaoneshwa vyema katika utajiri wa kitu kizima, ambacho aina yake hutoka "kutokana na nia ya wakala wa kwanza," ili "kile ambacho kila kitu kinakosa kuwakilisha wema wa kimungu hutolewa na vitu vingine." Hata hivyo, ikiwa kungekuwa na kiumbe mmoja tu, ingawa ni mkamilifu zaidi, hii ingekuwa hasara, kwa sababu wema wa Mungu "hauwezi kuwakilishwa vya kutosha na kiumbe mmoja." Kwa sababu hiyo hiyo, Papa Francisko alielezea, "tunahitaji kuelewa aina mbalimbali za vitu katika mahusiano yake mengi. Kwa hivyo, umuhimu na maana ya kiumbe chochote inaeleweka vyema ikiwa itazingatiwa katika muktadha wa mpango wa Mungu"(LS 86).
Kadiri sayansi na teknolojia inavyosonga mbele...
Kwa maneno mengine, Mtakatifu Yohane wa Msalaba alisema: "Tupenye kwenye kichaka cha kazi zako za ajabu […] ambazo wingi wake ni mkubwa na tofauti sana hivi kwamba unaweza kuitwa mnene. Ndani yake, kiukweli, kuna hekima nyingi na iliyojaa mafumbo […] yenye kina na kubwa sana hivi kwamba, haijalishi mtu anaijua kiasi gani, roho inaweza kupenya ndani zaidi, kwani ni kubwa na ina utajiri usioeleweka."(Wimbo 36, 10). Kadiri sayansi na teknolojia inavyozidi kusonga mbele, ndivyo tunavyopaswa kudumisha ufahamu huo wa mapungufu yetu, ya hitaji letu kwa Mungu ili tusianguke katika udanganyifu mbaya, ule ule uliosababisha kuzidi kwa uzushi, vita vya kidunia, Mauaji ya Kimbari, mauaji ya halaiki huko Gaza, hali zote ambazo zinahesabiwa haki kwa hoja za uongo. Shida ni kwamba jambo hilo hilo linaweza kutokea katika maisha yetu yote. Kiukweli, tunarudia udanganyifu huo kwa kuishi kwa kujiamini sana katika kile tunachokijua.
Ili kuelewa chochote kikamilifu tujiruhusu kuangaziwa na Mungu
Hili linatuita kutambua mambo mawili:Kwamba ili kuelewa chochote kikamilifu, lazima tujiruhusu kuangaziwa na Mungu; lazima tumwite, tumwombe, tumsikilize, tumruhusu atuongoze kupitia vivuli. Imani inatuhakikishia kwamba tunaweza kufanya hivi kweli, na kwamba inawezekana kweli kwake kutuangazia ili tuweze kuona vizuri zaidi. Tumwamini Yeye. Kwamba ni lazima tutafakari, tufikirie, na tuchambue ukweli, lakini pia tuwasikilize wengine, tukikumbatia mitazamo yao inayoturuhusu kutambua vipengele vingine vya ukweli wenyewe, na kujifungulia mitazamo mingine. Kwa sababu hiyo, ni vizuri kwetu kuzingatia "pembezoni" ambapo mambo yanaonekana tofauti. Kwa njia hiyo, Papa Leo XIV hivi karibuni alisema kwamba "hakuna mtu aliye na ukweli wote; ni lazima sote tuutafute kwa unyenyekevu, na kuutafuta pamoja." Kwa hivyo, alipendekeza "Kanisa ambalo halijifungi lenyewe, lakini linabaki kumzingatia Mungu ili liweze kumsikiliza kila mtu kwa usawa,"(Mahubiri kwa kikundi cha kisinodi,26 Oktoba 2025).
Mahali pa kuandikia Hati zinazokuwa sehemu za majisterio ya kawaida
Kwa kawaida, hili ni kweli zaidi kuhusiana na ukweli wa imani. Leo hii, maarifa ya wanataalimungu kwa kawaida hupunguzwa hadi kwenye taaluma ya kitaalimungu au mada iliyotengwa, huku mafumbo ya imani yakiunganishwa katika uongozi wa thamani, ambapo kila kitu huangazwa hasa na ukweli huo mkuu unaounda moyo wa Injili. Hakika, mahali kama hapa, ambapo tuna fursa ya kutoa majibu yenye mamlaka, kuandika hati zinazokuwa sehemu ya majisterio ya kawaida, na hata kusahihisha na kulaani, hatari ya kupoteza upana wa mtazamo wetu ni kubwa zaidi. Lakini suala hili ni kubwa zaidi, kwa sababu leo, kwenye blogu yoyote, mtu yeyote, hata wale ambao hawajasoma Taalimungu sana, wanaelezea maoni na lawama zao kana kwamba wanazungumza ex cathedra. Hii ndiyo sababu ni lazima tupone Kanisani kote kwamba uhalisia mzuri unaopendekezwa na wahenga wakubwa na watafakuri wa Kanisa.
Kukanusha kunafaa zaidi kuliko uthibitisho
Kardinali aliendelea kusema, Kile kilichosemwa kuhusu mipaka ya akili zetu kinatumika kwa uhalisia wote, wa asili na wa ajabu, lakini zaidi ya yote kwa shimo la Mungu. Kwa hivyo “ningependa kumalizia kwa maneno machache kutoka kwa Mtakatifu Bonaventure: Katika Itinerarium mentis in Deum yaani, Safari ya Nafsi kwa Mungu aliuliza ni nani tunapaswa kuzungumzia maswali makubwa. Naye akajibu: "Si kwa nuru, bali kwa moto unaowaka na kusafirisha kila kitu [...]Moto huu ni Mungu, ambaye makaa yake yako Yerusalemu, na Kristo anauwasha kwa ari ya shauku yake kali zaidi”(It. VII, 6). Na mwishoni mwa utafiti wake kuhusu sayansi ya Kristo, alisema kwamba, katika safari hii, "kukanusha kunafaa zaidi kuliko uthibitisho, ubora wa juu zaidi kuliko uthibitisho chanya. Ukimya wa ndani huchangia zaidi katika kuupitia kuliko maneno. Kwa hivyo, katika hatua hii, majadiliano yetu lazima yaishe, na ni bora kumwomba Bwana atupe uzoefu tunaozungumzia"(De Sc. Chti. VII, ad ob 21), Alihitimisha.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here