Askofu Prosper Balthazar Lyimo Jimbo Katoliki Bariadi, Tanzania
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Alhamisi tarehe 8 Januari 2026 ameunda Jimbo Jipya la Bariadi “Bariadensis” nchini Tanzania na kumteua Askofu Msaidizi Prosper Balthazar Lyimo wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania kuwa Askofu wake wa kwanza. Jimbo Katoliki la Bariadi limemegwa kutoka katika Jimbo Katoliki la Shinyanga na hivyo linakuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Mwanza na Makao makuu ya Jimbo yatakuwa mjini Bariadi na Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Bariadi ni Parokia ya Mwinjili Yohane, ingawa ujenzi wa Kanisa kuu jipya, la Mtakatifu Luka, unaendelea mjini Bariadi. Askofu Prosper Balthazar Lyimo, baada ya kupokea taarifa hii anakiri kwamba, haikuwa rahisi sana kwake kupokea uteuzi huu, lakini baada ya kusali na kutafakari, akakubali kutekeleza mapenzi ya Mungu, akitambua kwamba, Mungu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, atamtegemeza katika maisha na wito huu mpya. Amewashukuru watu wa Mungu Jimbo kuu la Arusha kwa upendo, ushauri na ushirikiano. Mama Kanisa anatambua na kukiri kwamba: Kanisa ni moja, takatifu katoliki na la mitume. Ni matumaini yake kwamba, familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Bariadi itampokea na hivyo kushirikiana kwa karibu zaidi kufanya kazi. Amewaomba watu wa Mungu kuendelea kumsindikiza kwa sala na kutakiana heri na baraka, ili waendelee kumtumikia Mungu kwa moyo wa furaha, sala na shukrani. Amekazia moyo wa huduma unaofumbatwa katika furaha na unaopenda amani siku zote kwani amani ina thamani kubwa zaidi kuliko utajiri wa dunia hii.
Itakumbukwa kwamba, Askofu Prosper Balthazar Lyimo alizaliwa kunako tarehe 20 Agosti 1964 huko Kyou-Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo yake ya shule ya msingi huko Maua na Arusha, alijiunga na Seminari ndogo ya Jimbo Katoliki Arusha. Alipata masomo yake ya Falsafa kwenye Seminari kuu ya Kibosho, iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi na masomo ya Taalimungu alipata Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.
Baada ya majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa Jimbo kuu la Arusha kunako tarehe 4 Julai 1997. Tangu wakati huo alikuwa ni mlezi katika Seminari ndogo ya Jimbo kuu la Arusha kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 1999. Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2004 alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2007 alipelekwa na Jimbo kwa ajili ya masomo ya juu mjini Roma, kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana. Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2008 alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha. Kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2011 Askofu Prosper Balthazar Lyimo, alitumwa na Jimbo kuu la Arusha kwa ajili ya masomo ya juu nchini Canada na huko akajipatia shahada ya uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paul, kilichoko mjini Ottawa. Na kunako mwaka 2011 alirejea nchini Tanzania na kupangiwa kazi ya kuwa Katibu mkuu na Mkuu wa Mahakama ya Jimbo kuu la Arusha. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 11 Novemba 2014 akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania na hatimaye kuwekwa wakfu tarehe 15 Februari 2015.
Na ilipogota tarehe 8 Januari 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bariadi, nchini Tanzania. Jimbo Katoliki la Bariadi “Bariadensis” ina Parokia 19 zitakazohudumiwa na Mapadre Jimbo 35, Mapadre watawa 8 na limebahatika kuwa na watawa wa kiume 11 na watawa wa kike ni 32. Majandokasisi wa Jimbo la Bariadi ni 48 na kwamba, lina taasisi za elimu zipatazo 7 na zile za afya ni 7.