Askofu Mwandamizi Joseph Mwongela, Jimbo Katoliki la Machakos, Kenya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 4 Januari 2026 amemteua Askofu Joseph Mwongela wa Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya, kuwa Askofu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Katoliki la Machakos, nchini Kenya. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Joseph Mwongela alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kitui. Itakumbukwa kwamba, Askofu mwandamizi Mwongela alizaliwa tarehe 7 Aprili, 1968 huko Kakumi, Jimbo Katoliki la Kitui. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 7 Septemba 1996 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baada ya hapo kama Padre alibahatika kuwa Paroko-usu, Paroko, Mlezi na Mkurugenzi wa Miito.
Kati ya mwaka 2003 hadi mwaka 2008 alitumwa na Jimbo kwenda Roma ili kujiendeleza kwa masomo ya juu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian na kujipatia Shahada ya Uzamili na hatimaye, Shahada ya Uzamivu katika “Dogmatic Theology” kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, maarufu kama Angelicum. Kipindi cha Mwaka 2008 alitoa huduma ya kichungaji kwenye Hospitali ya “Mater Misericordiae,” Jimbo Katoliki la Kitui. Kati ya Mwaka 2008 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Muthale, Jimbo Katoliki la Kitui.
Kati ya Mwaka 2014-2015 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Yohane Paulo II kwa ajili ya masomo ya kitaaluma na Paroko wa Parokia ya Boma (Kanisa kuu la Our Lady of Africa). Na tangu mwaka 2015, alikuwa ni Makamu Askofu Jimbo Katoliki la Kitui. Tarehe 17 Machi 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kitui na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 29 Agosti 2020. Na ilipogota tarehe 4 Januari 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa ni Askofu Mwandamizi wa Jimbo Katoliki Machakosi, nchini Kenya.