Tafuta

Wapendwa Taifa la Mungu, hii ni Noeli ya pekee katika maisha ya wengi. Ni Noeli katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Wapendwa Taifa la Mungu, hii ni Noeli ya pekee katika maisha ya wengi. Ni Noeli katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo.  (@VATICAN MEDIA)

Askofu Joseph R. Mlola: Ujumbe wa Noeli 2025 Na Mwaka Mpya 2026

Wapendwa Taifa la Mungu, hii ni Noeli ya pekee katika maisha ya wengi. Ni Noeli katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Noeli hii ni mwaliko wa kuendelea kumfurahia Mungu aliyetujalia nafasi ya kuuona tena Uso wake katika Mwanae mpendwa, Yesu Kristo aliyezaliwa duniani kwa kusudi la kukaa kwetu, kama anavyotuandikia Yohane Mwinjili akisema “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu” (Yoh. 1:14). Noeli ni Sherehe ya: Imani, Matumaini na Mapendo thabiti!

+Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS., -Jimbo Katoliki la Kigoma, Tanzania

Baba Mtakatifu Leo XIV, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, katika tafakari yake amejikita katika: Hekima ya Noeli inayofumbatwa katika amani "isiyo na silaha na inayopokonya silaha.” Noeli ni chemchemi ya Injili ya matumaini na furaha ya kweli; ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu na utume unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo. Tafakari ya Fumbo la Umwilisho, Neno aliyefanyika mwili inatia moyo neno jipya na la kweli katika Kanisa lote kwa kuwataka waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Noeli, ambayo ni adhimisho la fumbo la imani, mapendo na matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni Sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Ni sherehe ya matumaini, kwa sababu Mtoto Yesu anawasha tena matumaini ndani ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa ni vyombo na wajumbe wa amani. Wakiwa wamesheheni fadhila hizi nyoyoni mwao, kamwe hawawezi kuogopa usiku na kwamba, wanaweza kukabiliana kikamilifu na changamoto ya mapambazuko ya siku mpya. Nabii Isaya alitabiri na kusema; “Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.” Isa 9:2. Na Malaika wakawatangazia wachungaji kondeni kwamba: “maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Lk 2:11.

Noeli ni Sherehe ya furaha, imani na matumaini
Noeli ni Sherehe ya furaha, imani na matumaini   (@Vatican Media)

Wapendwa Taifa la Mungu, hii ni Noeli ya pekee katika maisha ya wengi. Ni Noeli katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Noeli hii ni mwaliko wa kuendelea kumfurahia Mungu aliyetujalia nafasi ya kuuona tena Uso wake katika Mwanae mpendwa, Yesu Kristo aliyezaliwa duniani kwa kusudi la kukaa kwetu, kama anavyotuandikia Yohane Mwinjili akisema “Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu” (Yoh. 1:14). Ninaomba myapokee machache haya ninayowashirikisha kama salamu zetu kwa Taifa la Mungu katika Sherehe hizi za Noeli ya Mwaka 2025 na Salamu za Mwaka mpya 2026. Unyenyekevu wa Mungu kwa faida ya mwanadamu. Kama Mungu aliye juu asingekubali kushuka chini, mwanadamu aliye chini asingeweza kupanda juu. Katika fumbo la Noeli tunatafakari jambo kuu na la kushangaza wenye Imani na wasiona Imani: Mungu amejinyenyekesha kwa ajili ya mwanadamu ili mwanadamu apandishwe hadi kushiriki maisha ya mbinguni pamoja na Mungu. Ni kwa sababu hiyo Mtakatifu Atanasi alisema "Mungu alifanyika mwanadamu, ili mwanadamu aweze kufanywa mshiriki wa umungu wake.”

Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo thabiti
Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo thabiti

Wapendwa Taifa la Mungu, unyenyekevu hata leo tunauhitaji. Tulio wakubwa kwa sababu ya umri au madaraka, tunahitaji unyenyekevu ili tuweze kuwafikia wale walio chini yetu. Daktari asiye mnyenyekevu hawezi kumtibu mgonjwa, maana hataweza kujishusha hata kufikia kuzungumza lugha inayopokelewa na mgonjwa ili ajieleze kwake kwa uhuru, kwa nia ya kupata tiba anayoihitaji. Hata wale walio wadogo wanauhitaji unyenyekevu, ili waweze kumpokea huyu mkubwa ambaye anakuja kwao ili ashiriki furaha, taabu na changamoto zao, kwa nia ya kutaka kuwaelekeza namna nzuri ya kuhusiana na Mungu, watu na viumbe wengine. Mtu anayekuja kwetu kwa nia ya kutusaidia akiwa mwenye nia njema na kama hakuna mashaka yoyote kuhusu anachotuelekeza, siyo wa kukwepa au kutupilia mbali kwa visingizio kwamba, hata bila yeye twaweza kujimudu. Neno alifanyika Mwili kwa ajili yetu, tumpokee ili atufundisha kuishi maisha mapya yanayokubalika kwa Mungu na yenye faida na hamasa kwa wengine.

Mungu anawafundisha waja wake njia ya upendo, haki na amani
Mungu anawafundisha waja wake njia ya upendo, haki na amani

Tufurahi kwa shukrani, Yesu amekuja duniani na kukaa kwetu. Kuna kishawishi cha walelewa kukosa furaha ya moyo, pale mlezi wao anapoamua kukaa karibu nao kwa masaa mengi. Kuna kishawishi cha kukosa amani ya moyo pale kiongozi anapoweka kambi na kuishi karibu sana na anaowaongoza. Kuna kishawishi cha watendaji wa nyadhifa za chini kufikiri kuwa wamesongwa, pale ambapo mtendaji mkuu anaamua kuhamishia makazi na ofisi yake, kati ya ofisi na makazi ya watendaji wa nyadhifa za chini. Bwana ameamua kuweka makazi yake kati ya makazi yetu. Dunia ni nyumba yetu sote wanadamu. Noeli ni tangazo la uamuzi wa Mungu kuweka makao yake kati yetu. Ni kweli, Neno wa Mungu amefanyika mwanadamu ili akaa kwetu wanadamu.

Askofu Joseph Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma
Askofu Joseph Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma   (Jugo Media)

Dunia na wapenda dunia, wanaweza kuuchukia uamzi huu wa Mungu wakidhani kuwa Mungu amekuja kuwasonga. Mungu hajaja duniani kutupeleleza. Hajaja duniani kutukebehi. Hajaja duniani kutucheka. Hajaja duniani kutupa ahadi za uongo. Hajaja duniani kwa nia mbaya. Amekuja duniani kutuletea mwanga wa mpya na matumaini mapya kwamba dunia iliyojaa upendo, amani, furaha, msamaha juhudi ya kazi, uaminifu, ukweli haki inawezekana. Hata kama mambo yameshaharibika au yanaelekea kuharibika, tunaweza bado kuuona mwanga wa matumaini kwa maisha ya sasa na ya baadaye ikiwa tutakubali kumkaribisha Mungu katika maisha yetu ya kiimani, ya kisiasa, ya kijamii, ya kielimu na ya kibiashara. Tusimfukuzie mbali kama mgeni. Vyote vilivyoko duniani na mbinguni ni mali yake. Tukumbuke kuwa, Mungu ameamua kukaa kati yetu ili atuongoze na kutufundisha njia ya upendo, haki, amani, uwajibikaji na uaminifu katika huduma zetu kwa wengine pamoja na Mungu mwenyewe anayeshughulikia na kuthamini maisha yetu.

Noeli ni Sherehe ya Imani, Matumaini na Mapendo Thabiti
Noeli ni Sherehe ya Imani, Matumaini na Mapendo Thabiti

Msiogope: Yesu alipozaliwa, Malaika aliwaambia wachungaji “Msiogope, kwa maana ninawaletea Habari Njema.” Tunapenda kuwatia moyo wote wana Taifa la Mungu. Tusiogope. Hatuko peke yetu sasa na wala hatutakuwa peke yetu mwanzoni mwa mwaka mpya, katikati ya mwaka mpya na mwishoni mwa mwaka 2026. Mungu ameamua kuweka maskani yake pamoja nasi wanadamu. Tunamtakia baraka, ulinzi, amani, furaha na mafanikio katika maisha kila mmoja wenu. Mungu awabariki na daima na awajalie kuuonja uwepo na upendo wake. Heri ya Noeli na mwaka mpya 2026.

+ Askofu Joseph Roman Mlola, ALCP/OSS.

Jimbo Katoliki la Kigoma, Tanzania.

Noeli na Mwaka Mpya 2026
16 Januari 2026, 15:13