Uzinduzi wa Pango na Mti wa Noeli katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Vatican News.
Mti wa Noeli na mandhari ya Pango la Kuzaliwa kwa Yesu katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, vyote viliwashwa na kuzinduliwa rasmi Jumatatu jioni tarehe 15 Desemba 2025 na Sr Raffaella Petrini, Gavana wa Jiji la Vatican. Wakati wa hotuba yake alisema: "Leo, katika uwanja huu unaokumbatia ulimwengu, mandhari ya Pango la kuzaliwa kwa Yesu na mti wa Noeli si mapambo ya Noeli tu, bali ni ishara za ushirika, wito wa amani na utunzaji wa uumbaji, na mialiko ya udugu wa ulimwengu wote, ambao Mtakatifu Francis aliuweka juu ya yote na ambao ukawa alama ya karama yake," alisisistiza huku akikumbuka jinsi ambavyo mwaka ujao 2026 utakavyokuwa kumbukumbu ya miaka 800 ya kifo cha Mtakatifu wa Assisi, ambaye alianza utamaduni wa mandhari ya Pango la kuzaliwa kwa Yesu mnamo mwaka 1223.
Wawakilishi wa kidini na wa kiraia kutoka majimbo yaliyotoa vitu hivyo walikuwepo na kuzungumza katika tukio la uzinduzi, na mapema siku hiyo walipata hata nafasi ya kukutana na Papa Leo XIV. Bendi ya Jeshi la Vatican, pamoja na kwaya na bendi tofauti kutoka majimbo, ziliimba nyimbo na ngoma za kiutamaduni za Noeli. Pango la Kuzaliwa kwa Yesu na mti vitabaki kwenye maonesho hayo hadi mwisho wa Kipindi cha Noeli, ambao unaambatana na Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana Dominika tarehe 11 Januari 2026.
Jimbo la Nocera Inferiore-Sarno kusini mwa Italia lilijikita na maandalizi ya Pango la kuzaliwa kwa Yesu, na iliwakilishwa na Askofu wake Giuseppe Giudice. Badala yake mti wa Noeli ulitoka Jimbo la Bolzano-Bressanone, kaskazini mwa Italia, na Askofu, Ivo Muser, pia alikuwepo. Askofu Mkuu Emilio Nappa na Giuseppe Puglisi-Alibrandi, wote wawili makatibu wakuu wa Mji wa Vatican, pia walishiriki katika tukio la uzinduzi.
Pango la kuzaliwa kwa Yesu limepangwa kwenye mstatili wa mita 17 kwa 12 (futi 56 kwa futi 39), wenye urefu wa mita 7.70 (futi 25). Pango linaakisi vipengele vingi vya usanifu na utamaduni wa kiutamaduni kutoka eneo la Agro Nocerino-Sarnese, pamoja na kuashiria kwa watakatifu fulani na watu wa kidini muhimu kwa eneo hilo, kama vile Mtakatifu Alphonsus Maria De Liguori, mwanzilishi wa Shirika la Mkombozi -Redentorist) na Watumishi wa Mungu, Padre Enrico Smaldone na Alfonso Russo. Pia linajumuisha alama zinazoakisi urithi wa chakula na divai ya eneo hilo. Barabara za lami zinaonesha barabara za kale za Warumi katika mabamba ya mawe, na wachungaji kwa ukubwa wa maisha na sanamu za wanyama zimeunganishwa juu yake.
Mti wa Noeli ni aina ya spruce wa Ulaya na ulitoka Jimbo la Bolzano-Bressanone. Una urefu wa mita 25 (futi 82) na uzani wa takriban kilo 8000 (zaidi kilo 17000) na ulikuwa zawadi kutoka manispaa za Lagundo na Ultimo huko kaskazini mwa Italia. Mbali na mti mkuu, kuna miti mingine 40 midogo pia italetwa Vatican ambayo itatumika kupamba ofisi, maeneo ya umma na majengo katika Mji wa Vatican. Mwishoni mwa kipindi cha Noeli , mafuta muhimu yatatolewa kutoka kwenye matawi ya mti, huku mbao zilizobaki zitasindikwa na chama, kwa kuzingatia kanuni ya kuheshimu kazi ya uumbaji.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Bonyeza hapa: Just click here