Ukraine,Papa Leo XIV atuma misaada kwa ajili ya Dominika ya Familia Takatifu
Vatican News
Malori matatu, vipande vya mraba laki moja ambavyo, vikiyeyushwa katika maji kidogo, huwa supu zinazotoa nguvu pamoja na kuku na mboga. "Msukumo mdogo" kutoka kwa Papa Leo XIV, unafuu muhimu kwa familia za Kiukreni ambazo, wakati wa Dominika ya Familia Takatifu ya Nazareti, ambayo inaadhimishwa Desemba 28, zilipokea msaada wa kibinadamu kutoka Vatican.
Mkono wa kusaidia wale wanaofuata "njia chungu ya uhamisho"
Zawadi ya Papa Leo XIV, kama Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Upendo alivyoambia vyombo vya habari vya Vatican, ni wazo kwa familia ambazo, kama familia huko Nazareti, "hufuata njia chungu ya uhamisho wakitafuta kimbilio," wakipitia "hali kubwa ya wakimbizi, iliyooneshwa na hofu, ugumu, na kutokuwa na uhakika." Ishara ambayo, Kardinali aliongeza kuwa inaonesha jinsi Mungu, "anavyozaliwa katika familia kama hiyo, anataka kuwa pale ambapo mwanadamu yuko hatarini, ambapo mwanadamu anateseka, ambapo anakimbilia, ambapo anapata kukataliwa na kuachwa."
Ukaribu na familia zinazoteseka
Kardinali pia alisisitiza jinsi ambavyo, hata kabla ya Noeli, Papa alivyotuma misaada ya kifedha kwa nchi kadhaa kupitia Ofisi ya Baraza la Kipapa la Upendo na Mabalozi za Kitume. Kwa Ukraine, kabla ya Mkesha wa Noeli, malori matatu yaliyojaa misaada ya kibinadamu kutoka kampuni yachakula ya Kikorea ya Samyang yalifika Vatican. Msaada huo kisha ulielekezwa kwenye maeneo ya vita yaliyoathiriwa zaidi na mabomu, "ambapo hakuna umeme, hakuna maji, na hakuna joto." Malori yalifika mahali yalipokwenda. Hivyo, Kardinali Krajewski alihitimisha,Papa Leo XIV "haombi amani tu, bali anataka kuwepo katika familia zinazoteseka."
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida kwa kubofya hapa: Just click here.