Tafuta

Wafungwa Mlango Mtakatifu wa Basilika ya Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta,Roma. Wafungwa Mlango Mtakatifu wa Basilika ya Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta,Roma.   (ANSA)

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei wahitimishwa katika Makanisa mahalia

Desemba 28,imehitimishwa ibada ya kufungwa kwa Milango Mitakatifu ya Basilika za kipapa.Kulingana na Tamko la Jubilei la“Spes non confundit,”ni matarajio kwamba Watu wa Mungu wanaweza kuwa wamekaribisha kikamilifu ujumbe wa matumaini katika neema ya Mungu na ishara zinazothibitisha ufanisi wake.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Ufunguzi Mkuu wa Mwaka wa Jubilei katika makanisa yote mahalia ulimwenguni ulifanyika kunako tarehe 29  Desemba 2024. Katika Mwanzo wa Tamko la Kutangaza kwa Jubilei ya Matumaini, una Kauli mbiu iliyoongoza kipinidi chote cha mwaka 2025 isemayo: Spes non Confundit, yaani,“Tumaini halikatishi tamaa” (Rm 5:5). Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ametuandikai kuwa  “katika roho ya matumaini, Mtume Paulo alitoa maneno haya ya kutia moyo kwa jumuiya ya Kikristo ya Roma. Tumaini pia ni ujumbe mkuu wa Jubile ijayo ambayo, kulingana na utamaduni wa kale, Papa hutangaza kila baada ya miaka ishirini na mitano.” Papa aliongeza kuandika  “Mawazo yangu yanawageukia mahujaji wote wa matumaini watakaosafiri kwenda Roma ili kupata uzoefu wa Mwaka Mtakatifu na kwa wale wengine wote ambao, ingawa hawawezi kutembelea Jiji la Mitume Petro na Paulo, wataiadhimisha katika Makanisa yao  mahalia. Kwa kila mtu, Jubile iwe wakati wa kukutana na Bwana Yesu, “mlango” (taz. Yh 10:7.9) wa wokovu wetu, ambaye Kanisa limepewa jukumu la kumtangaza siku zote, kila mahali na kwa wote kama “tumaini letu” (1 Tim 1:1) na (taz. Spes non Confund ,1).

Maskofu Mahalia waliteua makanisa kwa ajili ya waamini kupata rahema

Ni katika Mkutadha huo ambapo Maaskofu waliteua makanisa ambapo waamini wangeweza kupata Rehema kamili ya Jubilei ndani ya eneo la majimbo yao,na kama vile wale waliopata fursa ya kufanya hija kufika Roma. Kwa njia hiyo Dominika hii,  tarehe 28 Desemba 2025, Kardinali James Harvey, Mkuu wa Basilika ya Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta, Roma  aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ibada ya kufunga Mlango Mtakatifu.

Katika mahubiri yake alisema kuwa kufikia hitimisho siku zote ni wakati  muhimu "huku huruma ya Mungu ikibaki wazi daima. Mwaliko ni hasa kuendelea katika njia ya uongofu na matumaini" iliyoongozwa na Mwaka Mtakatifu. Katika Kanisa lililowekwa wakfu kwa kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo, maneno kutoka kwa Barua kwa Warumi yanasikika kwa nguvu maalum: "tumaini halikatishi tamaa, ambayo iliambatana na Jubilei nzima. Zaidi ya "kauli mbiu" tu, maneno haya ni "ungamo la imani" la kweli. Mtume wa Mataifa anakabidhi maneno haya kwa historia katika ufahamu wa ugumu wa maisha, baada ya kupitia kifungo, mateso, na kushindwa dhahiri. Hata hivyo tumaini halishindwi, kwa sababu halitegemei uwezo dhaifu wa kibinadamu, bali  kwa upendo mwaminifu wa Mungu."

Mahujaji wa Matumaini

Kauli mbiu ya Jubilei ya 2025 ilikuwa "Peregrinantes in Spem" – “Mahujaji wa Matumaini.” Katika Tangazo hilo la Papa Francisko alionesha matumaini kwamba kila mtu anaweza kuwa na matumaini. Matumaini yapo moyoni mwa kila mtu kama hamu na matarajio ya mema, hata kama hatujui kesho italeta nini. Papa Francisko alisisitiza kwamba “mara nyingi tunakutana na watu waliokata tamaa ambao wanatazama wakati ujao kwa mashaka na kukata tamaa, kana kwamba hakuna kitu kinachoweza kuwaletea furaha. Katika muktadha huu,” Papa Francisko alionesha “matumaini kwamba Jubilei itakuwa fursa kwa kila mtu kufufua matumaini.”

Kufungwa kwa Mlango Mtakatifu katika Basilika za Kipapa

Kufungwa kwa Mlango Mtakatifu katika Basilika za Kipapa Roma ni ishara inayoonekana ya siku za mwisho za Mwaka Mtakatifu. Siku ya Noeli  ibada ya kufunga Mlango Mtakatifu wa Basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu ilifanyika, ikiongozwa na Kardinali Rolandas Makrickas. "Moyo wa Mungu unabaki wazi," alisisitiza Mkuu wa Basilica ya Liberia, ambaye alituomba tujifungue kusikiliza Neno, kuwakaribisha wengine, na msamaha. Tumaini ni nuru, limetafsiriwa kuwa sala na huduma kwa maskini, ili liwe Kanisa "lenye Injili mikononi mwetu na kaka na dada zetu mioyoni mwetu," Kardinali alisema.

Kufungwa kwa Mlango Mtakatifu wa Lateran Des 27

Mlango Mtakatifu huko huko Lateran, Roma  ulifungwa Jumamosi, tarehe 27 Desemba 2025. "Leo, tunapofunga Mlango Mtakatifu, tunamwimbia Baba wimbo wa shukrani kwa ishara zote za upendo wake kwetu, huku tukithamini mioyoni mwetu ufahamu na matumaini ambayo yamebaki wazi kwa watu wote: kukumbatia kwake huruma na amani," alisema Kardinali Baldassare Reina, Makamu wa Papa na Mkuu wa Basilika, ambaye aliongoza Ibada ya mis ana sherehe ya kufunga malngo Mtakatiru huo

Tarehe 6 Januari 2026, hitimisho la Jubilei kufunga Mlango Mtakatifu wa Mt. Petro

Baba Mtakatifu Leo XIV atahitimisha Jubilei ya Kawaida kwa kufunga Mlango Mtakatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 6 Januari 2026, sanjari na  Siku kuu ya Epifania, yaani Toke la Bwana. Akitangaza kufungwa kwa Mlango Mtakatifu, Papa Francisko alielezea matumaini yake: "Mwanga wa tumaini la Kikristo umfikie kila mtu, kama ujumbe wa upendo wa Mungu unaoelekezwa kwa wote! Na Kanisa liwe shahidi mwaminifu wa ujumbe huu katika kila sehemu ya dunia!" (Spes non confundit, 6).

Katika tamko la Jubilie lilibanisha kuwa “Tumaini hupata ushuhuda wake mkuu katika Mama wa Mungu. Katika Bikira Maria, tunaona kwamba tumaini si matumaini yasiyo na msingi bali ni zawadi ya neema katikati ya uhalisia wa maisha. Kama kila mama, kila Maria alipomtazama Mwanawe, alifikiria kuhusu mustakabali wake.Hakika aliendelea kutafakari moyoni mwake maneno aliyoambiwa Hekaluni na mzee Simeoni: “Mtoto huyu amekusudiwa kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli, na kuwa ishara itakayopingwa, ili mawazo ya ndani ya wengi yafunuliwe - na upanga utachoma roho yako pia” (Luka 2:34-35). Katika Uchungu wa msalaba, alishuhudia mateso na kifo cha Yesu, mwanawe asiye na hatia. Akiwa amezidiwa na huzuni, hata hivyo aliboresha “fiat” yaani Tazama mimi hapa yake, bila kuacha tumaini na imani yake kwa Mungu.  

Kwa njia hii, Maria alishirikiana kwa ajili yetu katika kutimiza yote ambayo Mwanawe alikuwa ametabiri alipotangaza kwamba angepaswa "kupitia mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka" (Marko 8:31). Katika uchungu wa huzuni hiyo, iliyotolewa kwa upendo, Maria akawa Mama yetu, Mama wa Tumaini. Sio kwa bahati kwamba uchaji wa watu wengi unaendelea kumwita Bikira Mtakatifu kama Stella Maris, jina linaloonyesha tumaini hakika kwamba, katikati ya dhoruba za maisha haya, Mama wa Mungu hutusaidia, hututegemeza na kututia moyo kuendelea katika tumaini na uaminifu( Spes non confundit, 24).”

Aidha Papa Francisko aliandika: “Ushuhuda wa waamini uwe kwa ulimwengu wetu chachu ya tumaini la kweli, ishara ya mbingu mpya na dunia mpya (taz. 2 Pet 3:13), ambapo wanaume na wanawake watakaa katika haki na maelewano, kwa matarajio ya furaha ya utimilifu wa ahadi za Bwana. Na tuvutwe hata sasa kwenye tumaini hili! Kupitia ushuhuda wetu, tumaini lisambae kwa wale wote wanaolitafuta kwa hamu. Jinsi tunavyoishi maisha yetu na viwaambie kwa maneno mengi: “Mtumaini Bwana! Shikamaneni imara, jipeni moyo na mtumaini Bwana!” (Zaburi 27:14). Nguvu ya tumaini na izidishe siku zetu, tunaposubiri kwa ujasiri kuja kwa Bwana Yesu Kristo, ambaye sifa na utukufu viwe kwake, sasa na milele(Spes non confundit, 25).”

KUFUNGA MILANGO MITAKATIFU

Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida kwa kubofya hapa: Just click here.

28 Desemba 2025, 14:38