Tafuta

Mahusiano ya Elimu na maskini Mahusiano ya Elimu na maskini  

Katika Dilexi Te:Mahusiano yaliyopo kati ya Kanisa na elimu kwa maskini

Akihutubia wanazuoni,Papa Francisko aliwakumbusha kwamba,elimu imekuwa kielelezo cha pendo la kikristo.Papa Fransisko alisema kuwa;“Utume wenu umejaa vikwazo na furaha...ni utume wa upendo,kwa sababu huwezi kufundisha bila kupenda”.Kwa maana hii,tangu kale,wakristo wanaelewa kwamba maarifa hutuweka huru,hutupatia utu,na hutuleta karibu na ukweli.Kwa Kanisa,kuwafundisha maskini ilikuwa ni tendo la haki na imani.

Na  Padre Angelo Shikombe – Vatican.

Mpendwa msomaji/msikilizaji wa Radio Vatican, tunakuletea mwendelezo wa makala ya Wosia wa “Dilexi Te” yaani “Nimekupenda” wa Papa Leo XIV, uliotiwa saini mnamo tarehe 4 Oktoba 2025, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Mtakatifu Fransisko wa Assis. Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa waraka huu unaoitwa “DILEXI TE” yaani “nimekupenda” akinukuu kutoka kitabu cha ufunuo 3:9 sehemu inayosema: “…tazama, nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, nao watatambua ya kuwa nakupenda”. Leo tuendelee sura ya tatu inayoelezea Kanisa lililo kwa ajili ya maskini. 

Ndugu msomaji/msikilizaji tuanze kwa kuangalia mahusiano yaliyopo kati ya Kanisa na elimu kwa maskini. Akihutubia wanazuoni, Papa Francisko aliwakumbusha kwamba, elimu imekuwa kielelezo cha pendo la kikristo. Papa Fransisko alisema kuwa; “Utume wako umejaa vikwazo na furaha... ni utume wa upendo, kwa sababu huwezi kufundisha bila kupenda”. Kwa maana hii, tangu kale, wakristo wanaelewa kwamba maarifa hutuweka huru, hutupatia utu, na hutuleta karibu na ukweli. Kwa Kanisa, kuwafundisha maskini ilikuwa ni tendo la haki na imani. Tukiiga mwongozo na mfano wa Mwalimu anayefundisha talimungu na elimu dunia, anayejitwika jukumu la kulea watoto na vijana, hasa maskini zaidi, katika misingi ya ukweli na upendo. Utume huu umekuwa chimbuko la kuanzishwa kwa taasisi za elimu. Katika karne ya kumi na sita, Mtakatifu Yusufu Calasanz, alipoikosa elimu na mafunzo miongoni mwa vijana maskini wa Roma, aliamua kuanzisha shule ya kwanza ya bure ya umma barani Ulaya, karibu na kanisa la Mtakatifu Dorotea huko Trastevere. Shule hii ndiyo chimbuko ya utume wa Makasisi Maskini wa Mama wa Mungu wa shule za wacha Mungu, zinazojulikana kama Wapiga Piari, ambao baadaye waliibuka na kujiendeleza. Kusudi lao kuu lilikuwa kuelimisha vijana kwa kujipatia si ujuzi wa kiulimwengu tu, bali pia hekima ya maandiko matakatifu, wakifundishwa kutambua upendo wa Mungu katika maisha yao binafsi na katika historia.

Ndugu msomaji/msikilizaji, Kanisa linamtambua huyu kuhani jasiri kama "mwanzilishi wa kweli wa shule za kisasa za kikatoliki, zenye mlengo wa malezi fungamano ya watu wote. Kwa ushawishi huo, Mtakatifu Yohana Mbatizaji De La Salle, akibaini ukosefu wa haki unaosababishwa na kutengwa kwa watoto wa wafanyakazi wasisome na watoto wengine katika mfumo wa elimu ya ufaransa ya wakati huo, alianzisha shirika la mabruda wa shule za kikristo katika karne ya kumi na saba, akilenga kuwapa elimu bure, malezi thabiti na mazingira ya kindugu. De La Salle alilichukulia darasani kama mahali pa majiundo ya utu, na mahali pa uongofu. Katika vyuo vyake, sala, maarifa, nidhamu na kushiriki vilifungamanishwa. Kila mtoto alitambuliwa kuwa ni zawadi ya kipekee kutoka kwa Mungu, na mafundisho yalikuwa ni huduma kwa kuujenga ufalme wa Mungu.

Ndugu msikilizaji, katika karne ya kumi na tisa, huko Ufaransa, Mtakatifu Marcellin Champagnat alianzisha Taasisi iliyojulikana kama Shule za Marist Brothers. “Alikuwa makini sana kwa mahitaji ya kiroho na ya kielimu ya wakati wake, hasa kutokuijua dini na tabia ya kupuuzia miongoni mwa vijana. Alijitoa kwa moyo wote kuwaelimisha na kuwainjilisha watoto na vijana, hasa wale waliohitaji zaidi, wakati nafasi za kusoma zilipobaki kuwa kipaumbele cha wachache. Kwa msimamo huo huo, Mtakatifu John Bosco alianza taasisi ya Wasalesiana nchini Italia ikiwa na misingi mikuu mitatu; fikra, dini, na moyo wa ukarimu au wema. Mwenyeheri Antonio Rosmini alianzisha Taasisi ya Caritas, ambamo "hisani ya kiakili" yaani “intellectual charity” ilifungamanishwa na “msaada wa kimwili,” yaani “material charity” pamoja na huduma ya kichungaji” na hatima yake kufikia maendeleo fungamano ya mtu. Mashirika mengi ya watawa wa kike yamekuwa wahusika wakuu wa mapinduzi ya kimafundisho.

Mashirika yaliyoanzishwa kati ya karne ya kumi na nane na kumi na tisa, ni utume wa Ursuline, Masista wa Shirika la Bikira Maria mama yetu, Maestre Pie na wengine wengi, waliingia katika mazingira ambayo huduma ya serikali haikuwepo. Walianzisha mashule vijijini, katika vitongoji na makazi ya wafanyikazi. Walihamasisha sana juu ya elimu kwa wasichana. Masista walipambana na adui ujinga kwa kuielimisha na kuiinjilisha jamii, hasa katika maisha ya kila siku. Walikuza karama na roho za mashirika yao kwa njia ya sanaa, huku wakifunda na kulea dhamiri. Mafunzo hayo yalitumia kanuni nyepesi kueleweka; yaani kwa njia ya ukaribu, uvumilivu na upole. Walifundisha kwa mifano ya maisha yao katika nyakati za giza la ujinga na migogoro.  Mashirika ya wawekwa wakfu yalikuwa vinara vya matumaini. Utume wao ulikuwa kuunda mioyo, kujenga utamaduni wa kufikiri na kukuza utu. Kwa kufungamanisha maisha ya uchamungu na majitolea kwa wengine, walipambana na tamaduni za ubaguzi huku wakieneza huruma kwa jina la Kristo.

Ndugu msikilizaji, katika mtazamo wa imani ya kikristo, elimu kwa maskini si upendeleo bali ni wajibu. Watoto wana haki ya kupewa maarifa kama hitaji la msingi la kutambua utu wa mwanadamu. Kuwafundisha kunathibitisha thamani yao, na kuwapa zana wanazoweza kuzitumia kupambanua ukweli wa maisha yao. Mapokeo ya kikristo yanazingatia maarifa yatokanayo na neema za Mungu na yale maarifa yanayotokana na wajibu wa jamii. Elimu ya kikristo haikusudii kupata wataalamu tu, bali pia kupata watu wema, wanaoutafuta uzuri na ukweli. Shule za kikatoliki, kwa hiyo, zinapokuwa aminifu kama zilivyoanzishwa, zinakuwa mahali pa jumuiya, malezi fungamano na endelevu ya kiutu. Kuunganisha imani na utamaduni, kunasiha mbegu za vizazi vijazo, na kuheshimu ya sura ya Mungu na ujenzi wa jamii bora.

Ndugu msikilizaji, tumefikia hapa kwa leo katika mwendelezo wa barua ya kitume, usikose kutufuatilia katika vipindi vijavyo.  Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Angelo Shikombe.

Dilexi Te 10
02 Desemba 2025, 17:57