Tafuta

2025.12.30 Misa ya kumbukizi ya Papa Benedikto XVI 2025.12.30 Misa ya kumbukizi ya Papa Benedikto XVI   (@VATICAN MEDIA)

Kard.Müller:Ratzinger,Taalimungu yake ni zawadi kwa Kanisa!

Katika kumbukizi ya miaka mitatu ya kifo cha Papa BenediKto XVI,Kardinali Muller aliongoza Misa katika Kanisa Kuu la Vatican.Katika mahubiri yake,alisisitiza kuwa marehemu Papa aliacha urithi mkubwa wa kitaalimungu na wa kipekee,hivyo anachukuliwa kuwa mmoja wa wasomi wakuu wa Kikatoliki leo hii.Na alikumbusha kwamba Papa Leo XIV anatumia urithi wa kiroho na kitaalimungu wa Mtakatifu Agostino,kwa sababu hiyo wote wawili wanamweka Yesu Kristo katikati ya imani ya Kanisa!

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Kardinali Gerhard Ludwig Müller, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapap Mafundisho Tanzu ya Kanisa  alasiri tarehe 30 Desemba 2025 aliongoza Ibada ya Misa katika Madhabahu ya Kiti cha  Basilika ya Mtakatifu Petro, kwa ajili ya  kumkumbuka Marehemu Papa Benedikto XVI, katika kumbukizi ya miaka mitatu ya kifo chake kilichotokea tarehe 31 Desemba 2022, akiwa na umri wa miaka 95. Ibada hiyo, iliyoudhuriwa na mapadre kadhaa na Padre Federico Lombardi, Rais wa Mfuko wa Kipapa wa  Joseph Ratzinger-Benedict XVI,  ambapo Kardinali katika mahubiri yake alithibitisha kwamba Ratzinger "si mtu wa zamani, bali ni mshiriki wa Mwili ulio hai wa Kristo, ambao ni mmoja mbinguni na duniani," na akaelekeza mawazo yake kwa  Papa Leo XIV.  “Kama Papa Benedikto XVI , yeye pia anatumia urithi wa kiroho na kitaalimungu wa mwalimu wa Kanisa, Mtakatifu Augustine, kwa sababu hii wote wawili wanamweka Yesu Kristo katikati ya imani ya Kanisa, mwili wa Kristo (in illo uno unum sumus.)

Misa ya kuombea Papa Benedikto XVI
Misa ya kuombea Papa Benedikto XVI   (@VATICAN MEDIA)

Katika mahubiri yake, yaliyotolewa kwa Kiingereza, Kardinali aidha alirudia maisha ya Papa Mjerumani, ambaye, kama profesa wa Taalimungu  na kama mhubiri, alijiweka mwenyewe katika huduma ya Neno kila mara. Kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa , alionesha bidii ya hali ya juu na usahihi wa kiakili, na kama papa, alikuwa mmoja wa wataalimunu wakuu  katika Kiti cha Petro. Alituachia urithi mkubwa wa kitaalimungu wa ubora wa kipekee na ametambuliwa kwa usahihi kama mmoja wa wasomi wakubwa Wakatoliki wa wakati wetu,  alisema Kardinali Müller, na kuongeza kwamba "hata Jürgen Habermas, mwakilishi wa  Shule ya Frankfurt ya Marxism ambaye anawakilisha ulimwengu wa kielimu wa usasa usiomcha Mungu, alitafuta mazungumzo naye, akiwa ameshawishika kwamba waamini na wasioamini wanaweza kufanya kazi pamoja kuokoa ulimwengu wa kisasa kutokana na kifo baridi cha kupinga ubinadamu na harakati za kifalsafa zinazotetea kutumia sayansi na teknolojia ili kushinda mapungufu ya msingi ya binadamu kama vile kuzeeka, magonjwa, mipaka ya utambuzikuongeza uwezo wa kimwili na kiakili kufikia hali ya “baada ya mwanadamu.

Kubariki kaburi la Hayati papa Benedikto XIV
Kubariki kaburi la Hayati papa Benedikto XIV   (@VATICAN MEDIA)

Kwa mujibu wa Kardinali Muller alisisitiza kuwa Taalimungu ya Ratzinger ni zawadi kwa Kanisa lote na kwa vizazi vijavyo. Kazi zake kamili, kama mpango wa vitabu kumi na sita vyenye takriban kurasa 25,000, zinafaa kwa yeyote mwenye maslahi ya kiroho, kitaalimungu, kifalsafa, au ya kinadharia-kiutamaduni, ya kale na mapya, au anayetaka kuchunguza zaidi mwaka wa liturujia au Mtaguso wa Pili wa Vatican. Ikiwa Mkristo anayetafuta msukumo na mwenye shida katika imani yake angeniuliza anapaswa kusoma nini zaidi ya yote, angependekeza vitabu  vitatu kuhusu Yesu wa Nazareti, Kardinali Müller aliendelea, kwamba vitabu hivyo vitatu vilichapishwa chini ya jina lake binafsi ili kutofautisha mamlaka yake ya kitaalimungu na yale ya Papa.

Tafakari ya Kardinali pia iligusia mgongano kati ya imani na sababu ulioibuka kutoka katika nuru. Mara nyingi imeonekana kwamba hitimisho la utafiti wa kibiblia wa kihistoria-kiuhakiki, epistemolojia ya kifalsafa, na hata hasa katika maswali kuhusu asili ya ulimwengu na uhai, imani katika Mungu Muumba na katika Yesu Kristo, Mwokozi pekee, zilikuwa za kupingana lakini  hata hivyo, hakuna kupingana na Ukweli uliofunuliwa kuhusu ulimwengu na ubinadamu na kwamba imani haihitaji kuthibitishwa na hitimisho zinazoweza kukosea za sayansi ya majaribio, kwani imejengwa juu ya Neno la Mungu, ambalo kupitia hilo vyote vilivyopo vilitokea.  Zaidi ya hayo, Yesu, Mungu kweli na mwanadamu wa kweli, ni ukweli wenyewe katika Utu wake wa Kimungu. Kwa hivyo, Kardinali Mullar alisisitiza,  kuwa ujuzi wetu wa Mungu katika Roho Mtakatifu haukosei na hauwezi kutiliwa shaka na maarifa ya kidunia tu. Hakika, kazi ya wataalimungu  ni kuonesha umoja kati ya imani iliyofunuliwa na maarifa ya hivi karibuni ya kidunia yaliyooneshwa katika nadharia.

Kaburi la Hayati Papa Benedikto XVI
Kaburi la Hayati Papa Benedikto XVI   (@VATICAN MEDIA)

Hatimaye, Kardinali Müller alisisitiza kile ambacho Papa Ratzinger alirudia mara nyingi: kwamba "Ukristo, pamoja na mafanikio yake yote makubwa ya kiutamaduni katika mafundisho ya kijamii, muziki na sanaa, fasihi na falsafa, si nadharia au mtazamo wa ulimwengu, bali ni kukutana na mtu, Yesu, ambaye ndiye Ukweli, nuru inayomwangazia kila mwanadamu. Hata hivyo, Kanisa si shirika lililoundwa na mwanadamu lenye mpango mkubwa wa kimaadili na kijamii, bali ni jumuiya ya wanafunzi wa Kristo, wanaokiri kwa ulimwengu kwamba wametafakari utukufu wake, kama Mwana pekee kutoka kwa Baba, aliyejaa neema na ukweli, wanafunzi ambao miongoni mwao ni Joseph Ratzinger, Mtaalimungu, Askofu, Kardinali, na hatimaye Papa.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here

31 Desemba 2025, 15:52