Tafuta

Jimbo kuu la Tabora: Salam za Noeli na Mwaka Mpya 2025: Sherehe za Noeli; Mwaka wa Makatekista 2026; Haki na Amani nchini Tanzania. Jimbo kuu la Tabora: Salam za Noeli na Mwaka Mpya 2025: Sherehe za Noeli; Mwaka wa Makatekista 2026; Haki na Amani nchini Tanzania.  (@Vatican Media)

Jimbo Kuu la Tabora: Salam za Noeli na Mwaka Mpya 2026: Makatekista & Amani

Salam za Noel ina Mwaka Mpya 2026 kutoka Jimbo kuu la Tabora zinanogeshwa na kauli mbiu: “Kristo aliyezaliwa aendelee kutuunganisha: na kwa pamoja tuinjilishe ulimwengu.” Katika Salam na Ujumbe huu, waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya neema na baraka; kiungo kati ya Mungu na wanadamu; Maadhimisho ya Mwaka wa Makatekista Jimbo kuu la Tabora 2026; Jitihada za Kanisa kulinda na kutetea haki na amani nchini Tanzania!

Na Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Msaidizi Josaphat Bududu, - Jimbo kuu la Tabora.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Ni sherehe ya matumaini, kwa sababu Mtoto Yesu anawasha tena matumaini ndani ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa ni wajumbe wa amani. Wakiwa wamesheheni fadhila hizi nyoyoni mwao, kamwe hawawezi kuogopa usiku na kwamba, wanaweza kukabiliana na mapambazuko! Salam za Noel ina Mwaka Mpya 2026 kutoka Jimbo kuu la Tabora zinanogeshwa na kauli mbiu: “Kristo aliyezaliwa aendelee kutuunganisha: na kwa pamoja tuinjilishe ulimwengu.” Katika Salam na Ujumbe huu, waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya neema na baraka; kiungo kati ya Mungu na wanadamu, muungano huu uendeleze kazi ya ukombozi na hivyo kuwafanya kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Zifuatazo ni salam za Noel ina mwaka Mpya 2026 zinazonogeshwa na Kauli mbiu “Kristo aliyezaliwa aendelee kutuunganisha: Kwa pamoja tuinjilishe Ulimwengu.

Yesu anakuja kuujenga Ufalme wa Upendo, Haki na Amani
Yesu anakuja kuujenga Ufalme wa Upendo, Haki na Amani   (@VATICAN MEDIA)

Kwa Mapadre, Watawa, Waamini Walei na Watu wote wenye Mapenzi Mema.

1.      Tukiwa kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Noeli za Mwaka huu 2025, ambao kwetu ulikuwa ni Mwaka Mtakatifu wa Kanisa, Mwaka wa Rehema na Neema zilizoletwa na Jubilei tuliyoadhimisha, tunapenda kwa namna ya pekee tutoe tena shukrani zetu kwa Mungu Baba aliyemtuma Mwanae, Bwana na Mkombozi wetu zaidi ya miaka 2000 iliyopita na ambaye kazi yake ya ukombozi inaendelea kupitia katika Kanisa alilolianzisha na linalomkumbuka leo. “Naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” (Yn. 1:14) Tunafurahi tena katika Noeli hii, kwani tunakumbushwa ukweli kwamba Mungu hakai mbali nasi na hakika amejiunga nasi na yuko pamoja nasi na kwamba uwepo wake unaendelea kutuletea neema. 

Kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni utimilifu wa furaha
Kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni utimilifu wa furaha   (@Vatican Media)

2.      Kwa kuzaliwa kwake Yesu aliyekuwa Masiha, furaha iliyongojewa ilitimia.  Kama asemavyo Isaya: “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza.” (Isaya 9:2) Mtoto huyu aliyezaliwa aliwaunganisha wanadamu na Mungu waliyekuwa wamemkosea na hivyo kutengana naye. Hali hii aliyoiwezesha Bwana wetu Yesu Kristo, ni kazi ya ukombozi ambayo tunapenda iendelee, na katika Kanisa la leo, hili litawezekana iwapo huo muungano utabaki na kuimarika na kazi ya ukombozi aliyoianzisha itaendelezwa na hilo kundi linalomfuata.

Kristo Yesu awe ni chachu ya Uinjilishaji wa kina: Mahitaji ya mtu mzima!
Kristo Yesu awe ni chachu ya Uinjilishaji wa kina: Mahitaji ya mtu mzima!   (@VATICAN MEDIA)

3.      Ndugu zangu tunaofurahia kuzaliwa kwa Mkombozi, kama ujumbe huu wa Noeli na Mwaka Mpya unavyotualika, tunapaswa kusali ili kwamba huyu Imanueli aliyezaliwa miaka zaidi ya 2000 iliyopita na anayezaliwa leo mioyoni mwetu, aendelee kutuunganisha na kwa pamoja twende kuinjilisha ulimwengu na hivyo kuifanya kazi yake hiyo ya ukombozi. Tumsikilize yeye na kuyasikia maneno yake aliyosema kuhusu ukweli huu. Kabla ya kurudi kwa Baba yake, aliwaombea wafuasi wake, wadumu katika umoja: “Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakao niamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” (Yn 17:20) Ni Kristo huyo huyo aliyetumwa na Baba, yeye naye aliwatuma mitume (Yn 20:21) akisema: “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mt 28 19-20) Kutoka kwa Mitume Kanisa limeipokea kazi hii na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu linaendelea kuutimiza wajibu huu, na kama Kristo mwenyewe alivyo amuru, litapaswa kufanya hivyo mpaka mwisho wa dunia. Yanatufariji maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyosema kwa Mitume kabla ya kupaa kwake mbinguni, kama alivyoyaleta kwetu mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume akisema: “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” (Mdo 1:8.) 

Jimbo kuu la Tabora Nchini Tanzania
Jimbo kuu la Tabora Nchini Tanzania

4.      Kanisa letu, likiongozwa na hao waliowekwa kulisimamia, halichoki na linaendelea kuwaalika Waamini kukuza umoja katika Kristo linapowajibika kuifanya kazi ya Uinjilishaji. Baba Mtakatifu Leo XIV, katika kuhamasisha na kuwatayarisha Waamini kwa ajili ya Maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni na Mkumbukwa Papa Pio XI, itakayoadhimishwa tarehe 18 Oktoba 2026, tayari ameainisha mada itakayotuongoza. “Wamoja Katika Kristo, Wamoja katika Utume.” Mada hiyo, kwa tafsiri ya kawaida, inayachukua mawazo makuu mawili ya Umoja katika Kristo na kuungana pamoja katika Utume au Uinjilishaji. Basi tunawaalikeni Waamini wote, tukiongozwa na Ofisi yetu ya Misioni na Mashirika ya Kipapa, kuungana na Kanisa lote la Kiulimwengu katika Maandalizi na Maadhimisho yenyewe, ambayo hakika yatazidi kutuimarisha katika roho ya umoja chini ya Yesu Kristo aliye kichwa chetu, tukibaki tumeungana katika kuendeleza kazi ya umisionari na hivyo kulijenga Kanisa kama alivyotuamuru yeye aliye Bwana na Mkombozi wetu.  

Roho Mtakatifu ni Mgawaji wa Karama na Mapaji
Roho Mtakatifu ni Mgawaji wa Karama na Mapaji   (Vatican Media)

5.      Katika ujumbe wetu wa Noeli na Mwaka Mpya uliowafikia kwenye maadhimisho ya Noeli ya Mwaka 2024, tuliwashukuru kwa yote mliyoyafanya mkiwa mmeungana na Kanisa la kiulimwengu kwenye maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 16 wa kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, iliyokuwa na mada na Kauli Mbiu ya: “Kanisa la Kisinodi – Umoja, Ushiriki na Utume”, iliyozinduliwa mwaka 2021 na kuhitimishwa mwezi Oktoba mwaka 2024.  Katika kuhitimisha Mkutano huo mkumbukwa Papa Francisko, alisema kuwa ni kweli mikutano ya Sinodi imehitimishwa lakini roho ya Sinodi hiyo inaendelea na ni lazima ibaki hai katika maisha yetu ya ushuhuda na uinjilishaji wa pamoja.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi Uwajibikaji wa watu wa Mungu
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi Uwajibikaji wa watu wa Mungu   (Vatican Media)

6.      Katika muktadha wa maneno hayo yaliyosemwa na Papa Francisko, ya kuendeleza hiyo roho ya Kanisa la kisinodi katika utume na maisha ya Kanisa, tunaalikwa tukiwa pamoja na Kanisa la kiulimwengu kuingia katika awamu ya Tatu itakayoendeleza roho ya Kanisa la Kisinodi inayojikita katika utekelezaji wa maazimio yaliyoletwa kwetu kwenye hati iliyotolewa baada ya kuhitimisha Mkutano wa Sinodi na kupitishwa na mkumbukwa Papa Francisko. Katika utekelezaji huo tunaalikwa kama wana-Kanisa kusisitiza na kuyakuza yale ambayo yataliona Kanisa linakua na kuendelea kujengeka likiongozwa na mifumo na tabia ya utendaji wa pamoja, tukimsikiliza na tukiongozwa na nguvu za Roho Mtakatifu anayebaki nasi daima. Ni imani yetu kuwa tunapoingia katika awamu hii ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa 16 wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Kanisa la Kisinodi, tutakuwa tayari kuhamasishwa na kuelimishwa na Makundi maalumu kama Kanisa Mahalia, ili kwa umoja katika Kristo na tukiwa tumeungana tutaweza kuifanya kazi ya Uinjilishaji unaoendana na wakati na mazingira ya leo kwa weledi, mbinu na taratibu zenye kuleta matokeo chanya yenye kuujenga ufalme wa Mungu na hivyo kuendeleza kazi ya kumkomboa Mwanadamu na Ulimwengu kwa ujumla.

7.      Tumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye mpaka sasa, kama Kanisa Mahalia la Tabora, ametuongoza na tayari tulianza kwa namna fulani na tunaendelea kuyaweka katika utekelezaji yale ambayo yataufanya utume wetu uendane na yaliyoazimiwa na yanayokuza roho ya kisinodi katika utendaji; tukisali, kutafakari pamoja, kuzungumzana na kufanya maamuzi ya pamoja kama Kanisa la Kisinodi.  Hii ni pamoja na kuweka sera, taratibu, vyombo na mifumo, katika shughuli za kiutawala na kichungaji, vitakavyotusaidia kwenye utendaji na hata katika kufanya maamuzi ya pamoja kwa faida na manufaa ya Kanisa zima.  Mwaka wote wa 2026 kadiri ya maelekezo kutoka Roma, utakuwa ni mwaka wa kuifanya hiyo kazi na zoezi la utekelezaji wa yaliyopitishwa kwenye Hati ya Mwisho ya Sinodi ya Maaskofu ya 2024, litakalofuatiwa na tathmini zitakazofanyika kuanzia Mwaka 2027.  Tunawaalikeni waamini wote muwe tayari kushiriki kikamilifu katika kutekeleza yanayopaswa kufanyika kadiri ya miongozo na taratibu zitakazo tufikia.

Unenzi wa Kanisa la Kisinodi Jimbo Kuu la Tabora, Tanzania
Unenzi wa Kanisa la Kisinodi Jimbo Kuu la Tabora, Tanzania

8.      Tunapoyafikiria makundi mbalimbali yanayowajibika na yanayotoa mchango mkubwa kiuchungaji na yanayopaswa kushirikishwa kikamilifu katika utendaji na hata katika mipango na upitishaji wa maamuzi yahusuyo kazi za kulijenga Kanisa, ni kundi la Makatekista linaloshiriki kwa namna ya pekee katika kukuza imani, kuelimisha mintarafu maadili ya Kanisa na hata kushuhudia imani kwa mifano na majitoleo ya sadaka katika shughuli za utume na maisha ya Kanisa kwa ujumla. Utume wa Makatekista ambao Mkumbukwa Papa Francisko alipenda na akaupa hadhi ya kuwa huduma inayotambulika rasmi katika Kanisa kwa Hati maalumu ijulikanayo kama “Antiquum Ministerium” yaani “Huduma ya Kale” ya mwaka 2021, sisi wana Jimbo Kuu la Tabora hatunabudi kuuenzi na kuukuza tukitamani kulipa nguvu Jeshi hili la Wainjilishaji ambalo tangu mwanzo wa Kanisa la Agano Jipya limefanya kazi kubwa na kuchangia katika kukua kwa Kanisa kwa kazi nzuri za kichungaji zilizofanywa na Makatekista wa Kiume na Kike ambao wakiongozwa na nguvu ya Roho Mtakatifu wamejitolea maisha yao na wengine mpaka kufa mashahidi kwa sababu ya kulijenga Kanisa. Nao ni kati ya wale wahudumu wanaoongozwa na nguvu ya Roho Mtakatifu kama wabatizwa na wakawa tayari kuyafanya mapenzi ya Mungu katika huduma hii. Tuyakumbuke daima yale maneno ya Mtume Paulo anapowaongelea wahudumu kama hawa waliozijenga zile jumuiya za kwanza za wakristo wakiongozwa na karama zilizowashukia kutoka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: “Basi pana tofauti za karama: bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yule yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii.......lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.” (1Kor 12:4-11.)

Makatekista ni Jeshi kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji
Makatekista ni Jeshi kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji

9.      Hizo huduma alizoainisha Mtume Paulo, zaweza kufanywa na kila mbatizwa kutegemea na atakavyoitikia sauti ya Roho Mtakatifu. Vivyo hivyo kuitikia sauti ya kutoa huduma ya kikatekista itamtegemea mtu anayeitwa akawa tayari kuisikia na kuifuata sauti ya Roho Mtakatifu. Katika kanisa letu hapa Tabora, tunao walioitwa wakaitika Wake kwa Waume na watakuwepo wengine ambao wako tayari kuitika hata siku za usoni na wakawa tayari kujitoa kwa ajili ya huduma hii kama Makatekista. Ndugu zangu, baada ya kutafakari kwa kina na tukithamini huduma inayotolewa na kundi hili la watumishi na wahudumu, wanaosaidiana na Mapadre, Mashemasi na hata wazazi na wasimamizi katika Familia za Kikristo kwenye kazi za uinjilishaji, tumeamua tuutangaze Mwaka 2026 uwe ni Mwaka wa Makatekista tukilenga kuhamasisha wito huu, kuwaenzi Makatekista, kukuza utume wa Makatekista katika Malezi na majifunzo yao na kwa namna ya pekee kuwawezesha kwa hali na mali ili waweze kujitolea kwa kujituma zaidi wakiyafurahia nasi tukiyafurahia matunda ya kazi zao wanapochangia kwa weledi na ubora zaidi katika kulijenga Kanisa letu. Kumbe, ndugu zangu, ili tuweze kuyafikia malengo yetu mintarafu, kukuza utume wa Makatekista tunaalikwa sote tuwe tayari kushiriki kama Kanisa la kisinodi katika kusali, kutafakari, kujadiliana, na katika kutoa maamuzi yatakayotusaidia kukuza na kuuwezesha utume huu muhimu.

Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa matumaini, imani na mapendo
Maadhimisho ya Jubilei ni muda wa matumaini, imani na mapendo   (ANSA)

10.    Tunaapoumaliza mwaka huu wa 2025, uliokuwa Mwaka wa Jubilei inayohitimishwa rasmi, tarehe 28 Desemba 2025, tunapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru kwa ushirikiano mliouonesha katika kuyafanya yote ambayo yamechangia kwa namna moja au nyingine kulijenga Kanisa letu Mahalia la Tabora na hivyo kuliwezesha kuendeleza kazi ya Uinjilishaji wa kina katika maeneo mbalimbali ya utume, ikiwa ni pamoja na kuitumia fursa hii ya Mwaka Mtakatifu kutujenga kiroho na kimwili kwa mazoezi na shughuli za kiroho zilizofanyika. Kwa namna ya pekee tunawashukuru kwa mwitikio chanya mlioonesha wa kuijenga nguvu ya kiuchumi kwa malengo ya kuzifanya kazi za uinjilishaji tukizikimbilia kwanza na kuthamini nguvu tulizonazo kabla ya kwenda nje.  Ni matumaini yetu kuwa mikakati tuliyojiwekea katika suala hili na mingine itakayobuniwa siku za usoni, itaweza kuyaleta mabadiliko na hivyo kutupeleka kwenye malengo yetu tarajiwa.

Kanisa linakazia: Usawa, mshikamano, haki, upendo, ukweli na amani
Kanisa linakazia: Usawa, mshikamano, haki, upendo, ukweli na amani   (AFP or licensors)

11.    Mkombozi aliyezaliwa na anayezaliwa leo katika mioyo yetu anakuja kuujenga Ufalme wa Upendo, Haki na Amani. Kama tunavyofahamu, pamoja na hali ya utulivu na amani ya kawaida tuliyokuwanayo Nchini mwetu, hali hii ilibadilika na kutokuwa rafiki kwa matukio yaliyoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2025. Kanisa likifahamu wajibu wake wa kushiriki katika kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani, halikukaa kimya bali limejitahidi kufanya kila lililowezekana ikiwa ni pamoja na kusali likiwa na matumaini ya kuona tunaishi katika jamii inayoongozwa na hizo tunu za umoja, usawa, mshikamano, upendo, ukweli, amani, na yote tunayoamini kuwa yataujenga Ufalme wa Mungu na kumkomboa Mwanadamu kimwili na kiroho. Ndugu zangu, sisi tunaoamini katika Huruma na Upendo wa Mungu usio na mipaka, tunaalikwa tuendelee kumwomba huyo mwenye uwezo ayabadilishe yale yanayoonekana kushindikana na yenye kusababisha magumu tunayoyapitia, watu wabadilishe mioyo yao na kutaka kuyaona mazuri na yenye kuleta ustawi katika nyanja zote za kidini, kisiasa, kijamii na hata kiuchumi. Pamoja na kuwaalika kwamba sote tuwe ni vyombo vya kuujenga Ufalme wa Mungu, tukiwajibika kila mmoja anavyoweza, kuyaleta na kuyawezesha hayo yaliyotajwa hapo juu, tunawaomba kuendelea kuiombea Nchi yetu ya Tanzania Amani na tuyaombee Mataifa yote Amani. Kule kwenye machafuko, kutoelewana, magonvi na vita tumwombe Imanueli, Mfalme wa amani aweke Mkono wake na Amani itawale. 

Kanisa: Haki na amani vitawale tena katika maisha ya Watanzania
Kanisa: Haki na amani vitawale tena katika maisha ya Watanzania

12.    Tumwombe Mama Bikira Maria aliyemleta Mkombozi na Mfalme wa Amani hapa ulimwenguni, awe nasi akitusindikiza na kutuombea ili tuyafanye Mapenzi ya Mungu kama alivyofanya mwanaye akitaka watu wote waokoke. Na tuyasikie maneno yake na kufuata nyayo zake yeye anayesema kuwa: “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho.” (Yn 6:38-40.) Heri ya Noeli na Baraka za Mwenyezi Mungu kwa Mwaka Mpya.

Salam za Noeli na Baraka Kwa Mwaka Mpya 2026
Salam za Noeli na Baraka Kwa Mwaka Mpya 2026   (@VATICAN MEDIA)

Imetolewa Tabora, 24 Desemba 2025

+Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora.

Na +Josaphat Bududu, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Tabora.

Jimbo Kuu la Tabora

 

29 Desemba 2025, 13:44