Tafuta

Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja Takatifu; Upadre na Ushemasi Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja Takatifu; Upadre na Ushemasi  (@Vatican Media)

Jimbo Katoliki Musoma Lafunga Lango La Jubilei ya Matumaini: Familia Na Ushemasi

Mama Kanisa anaziombea familia ili kweli ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya sala wanapewa malezi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Kwa njia ya imani inayopyaishwa kwa sala, waamini wataweza kugundua nyuso za jirani zao wahitaji, tayari kusikiliza na kujibu kilio chao. Askofu Msonganzila: Ukomavu!

Na Veneranda Flavian Malima, - Musoma

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Waamini na watu wenye mapenzi mema wahakikishe kwamba, kweli familia zinakuwa ni shule ya sala, ili kugundua na kuonja kwa mara nyingine tena uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja nao! Kwa njia hii, ataweza kuwakirimia zawadi ya amani, matumaini na furaha ya kweli. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kupyaishwa kwa njia ya sala, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mama Kanisa anaziombea familia ili kweli ziweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya sala wanapewa malezi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Kwa njia ya imani inayopyaishwa kwa sala, waamini wataweza kugundua nyuso za jirani zao wahitaji, tayari kusikiliza na kujibu kilio chao. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania amesema ukomavu wa Taifa zima unatokana na malezi thabiti ya familia na kwamba, wazazi wanahimizwa kulea na kuwarithisha maadili mema watoto wao huku watoto wakikumbushwa kuwaheshimu, kuwatii na kuwatunza wazazi wao. “Wazazi tusikimbie majukumu … watoto tusikimbie majukumu. Heshima kwa baba na mama ni kuweka akiba yako na watoto wako”, amesema Askofu Msonganzila.

Askofu Msonganzila wa Jimbo la Musoma
Askofu Msonganzila wa Jimbo la Musoma

Askofu Msonganzila aliyasema hayo wakati wa mahubiri yake katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama wa Mungu, Jimbo Katoliki Musoma katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Dominika tarehe 28 Desemba 2025 ambayo ilitumika kwa malengo matatu; kuadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; Kutoa Daraja la Ushemasi kwa Mafrateri watatu na kufunga Mwaka wa Jubilee Kuu ya 2025. Akirejea sehemu ya Injili ya Mt. 2: 13-15, 19-23; Ondoka umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikwambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii, akisema, kutoka Misri nalimwita mwanangu.” Kupitia Maandiko Matakatifu, Askofu Msonganzila alisema, Mtakatifu Yosefu anapata mamlaka ya kulea na kutunza uhai wa mtoto, baba na mama. Anaonesha uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility), na hivyo Yesu, Maria na Yosefu wamewajibika kwa pamoja. “Tusikwepe wajibu wa pamoja. Mamlaka ni tofauti; Mamlaka ya Mungu ni ya kuokoa … Mamlaka ya Herode ni ya kuangamiza”, alisema Askofu Msonganzila. Aliongeza kuwa, “Tujifunze kuwa watulivu na kuheshimu uwajibikaji wa pamoja … Maria alitulia alipojulishwa kuwa atakuwa Mama wa Mungu. Tuwe tayari kuilinda, kuitetea na kuitunza amani ya familia. Familia takatifu siyo ya kutafuta vitu.” Askofu Msonganzila alihitimisha mahubiri yake kwa kukazia tunu ya uwepo wa familia, “Tukipoteza familia tutakuwa na taifa la ajabu … Familia iwe shule ya upendo, amani, utu wema na mshikamano. Tuziombee familia zote, nchi yetu iwe ni familia ya makabila zaidi ya 120 … tuishi kama taifa moja na tukemee tabia ya Herode.”

Watoto wamekumbushwa umuhimu wa kuwaheshimu, kuwatii na kuwatunza
Watoto wamekumbushwa umuhimu wa kuwaheshimu, kuwatii na kuwatunza

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yamefunga tayari Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani. Kwa upande wa kufunga Maadhimisho ya Jubilee Kuu 2025; Askofu Msonganzila alisema kipindi hicho cha mwaka mmoja kimewapa waamini nafasi ya kuhiji, kukuza imani na amani. “Katika Jubilee, tumepata nafasi ya kuhiji, kupata amani na kumwimbia Mungu mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu. Ni muhimu kujihoji, Je tumetimiza majukumu yetu? Je, tumeyatimiza haya kwa sifa na utukufu wa Mungu? Tuombe msamaha pale tulipokosea, na tuwalee watoto wetu ipasavyo. Tuwe na tabia ya kupokea maelekezo ya wakubwa/viongozi wetu, yawe ni ya kuelekeza au ya kuonya. Tusitumie vibaya madaraka bali tujenge maelewano ya kifamilia na taifa, na tusitamani kuwa na amani ya mtutu wa bunduki bali ya moyoni.”

Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa
Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa   (@Vatican Media)

Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja Takatifu; Upadre na Ushemasi. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee, utume na neema ya Kristo Yesu. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa ya kudumu na hivyo kufananishwa na Kristo Yesu aliyejifanya “Shemasi”, yaani Mtumishi wa wote! Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza na kuhubiri Injili; kwa kusimamia na kubariki ndoa; kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa niaba ya Kanisa!Kwa mashemasi wapya watatu; James Mong’osi Weibe, Samwel Dede Ouma na Fredrick Augustine Kamugisha, Mhashamu Askofu Msonganzila aliwakumbusha umuhimu wa kusimamia haki, kulinda amani na upatanisho wakati wa kutekeleza majukumu yao ya: Kuongoza, Kutakatifuza na Kufundisha.

Jimbo Katoliki Musoma
31 Desemba 2025, 17:24