Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV ameunda Jimbo Jipya la Caia na kumteuwa Askofu Msaidizi António Manuel Bogaio Constantino, M.C.C.J., wa Jimbo kuu la Beira, Msumbiji kuwa Askofu wake wa kwanza. Baba Mtakatifu Leo XIV ameunda Jimbo Jipya la Caia na kumteuwa Askofu Msaidizi António Manuel Bogaio Constantino, M.C.C.J., wa Jimbo kuu la Beira, Msumbiji kuwa Askofu wake wa kwanza.  (Vatican Media)

Askofu António Manuel Bogaio Constantino Jimbo Katoliki la Caia, Msumbiji

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 23 Desemba 2025 ameunda Jimbo Jipya la Caia (Dioecesis Caiana) nchini Msumbiji na kumteuwa Askofu Msaidizi António Manuel Bogaio Constantino, M.C.C.J., wa Jimbo kuu la Beira, Msumbiji kuwa Askofu wake wa kwanza. Jimbo la Caia limeundwa baada ya Baba Mtakatifu Leo XIV kumega Jimbo kuu la Beira, Jimbo la Chimoio, Quelimane na Jimbo Katoliki la Tete. Lina Parokia 16, Mapadre Jimbo 15, Watawa wa kike 17 na Waseminari 18

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Lengo la Mama Kanisa kuunda Majimbo mapya ndani ya Kanisa Katoliki kunalenga kusogeza huduma za kiroho na kichungaji kwa watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tarehe 23 Desemba 2025 ameunda Jimbo Jipya la Caia (Dioecesis Caiana) nchini Msumbiji na kumteuwa Askofu Msaidizi António Manuel Bogaio Constantino, M.C.C.J., wa Jimbo kuu la Beira, Msumbiji kuwa Askofu wake wa kwanza. Jimbo la Caia limeundwa baada ya Baba Mtakatifu Leo XIV kumega Jimbo kuu la Beira, Jimbo la Chimoio, Quelimane na Jimbo Katoliki la Tete. Ni Jimbo ambalo lina ukubwa wa kilometa 54, 569; Idadi ya watu ni 1, 603, 063. Jimbo linaundwa na Parokia 16 zitakazo hudumiwa na Mapadre Jimbo 15 na Watawa 8. Kwa bahati mbaya Jimbo jipya la Caia halina watawa wa kiume, lakini watawa wa kike ni 17 pamoja na Majandokasisi 18. Parokia ya “São Mateus Apóstolo” inakuwa ni Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Caia.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Barai Afrika
Hija ya Kitume ya Papa Francisko Barai Afrika   (Vatican Media)

Itakumbukwa kwamba, Askofu António Manuel Bogaio Constantino, M.C.C.J., wa Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, maarufu kama Wamisionari wa Comboni, alizaliwa tarehe 9 Novemba 1969 mjini Beira, Msumbiji. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kipadre, tarehe 13 Juni 2001 akapewa Daraja takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Beira. Tarehe 13 Desemba 2022, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Beira, Msumbiji na hatimaye, kuwekwa wakfu tarehe 19 Februari 2023. Tarehe 23 Desemba 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Jipya la Caia (Dioecesis Caiana) nchini Msumbiji.

Uteuzi Msumbiji
23 Desemba 2025, 15:12