Ask.Mkuu Balestrero:Vatican inathamini juhudi kuwasaidia wakimbizi na mataifa yenye hifadhi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Askofu Mkuu Ettore Balestrero Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika ofisi za Umoja wa Mataifa, taasisi Maalum na Mashirika ya Kimataifa huko Geneva Uswiss alitoa hotuba yake katika Jukwaa la Mapitio ya Maendeleo ya Wakimbizi Duniani, huko Geneva, Uswiss tarehe 17 Desemba 2025, ambapo alianza kusema kuwa tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Wakimbizi, jumuiya ya kimataifa imepiga hatua kubwa katika kukuza uwajibikaji wa pamoja na kupanua njia kwa watu binafsi wanaohitaji ulinzi wa kimataifa. Hata hivyo, ni lazima tukubali kwamba kuhamishwa kwa lazima kote ulimwenguni kunaendelea kusababisha mateso makubwa kwa wanadamu. Maisha mengi bado yanaharibiwa na vurugu, migogoro, na mateso. Kwa hivyo, ingawa kuimarisha juhudi za ulinzi bado ni muhimu, kutafuta njia za kushughulikia sababu kuu za kuhamishwa kwa lazima kumekuwa kipaumbele kikubwa zaidi.
Kurudi salama wakimbizi katika nchi zao lazima kuhakikishwe
Askofu Mkuu Balestrero aliongeza kusema kuwa zaidi ya hayo, kurudi kwa wakimbizi salama na kwa heshima katika nchi zao lazima kuhakikishwe. Kwa kweli, ni muhimu kusisitiza kwamba wale wanaotaka kurudi nyumbani wanapaswa kuweza kufanya hivyo salama. Vatican inathamini juhudi zilizofanywa katika Jukwaa la Pili la Wakimbizi la Kimataifa ili kuwasaidia wakimbizi na mataifa yenye hifadhi na kupata suluhisho thabiti. Miaka miwili baadaye kutoka katika Jukwaa, kuhakikisha utii kamili wa kanuni ya kutowarudisha wakimbizi - iliyoainishwa katika Mkataba wa Wakimbizi wa 1951 - kupitia ushirikiano mkubwa wa kimataifa na kugawana mizigo, bado ni muhimu ili kupunguza shinikizo kwa Nchi zinazowahifadhi wakimbizi.
'Kuunganishwa tena kwa familia ni muhimu'
Askofu Mkuu Balestrero aidha alisisitiza kuwa kwa kuzingatia kuongezeka kwa mvutano wa kimataifa na mateso yanayoendelea, ni muhimu kwamba mwitikio wetu wa pamoja unategemea kanuni ya uwajibikaji wa pamoja. Mataifa hasa yale yanayopakana na maeneo ya migogoro, yayopaswa kutarajiwa kubeba mzigo wa watu wengi kuhama peke yao. Kanuni ya uwajibikaji wa pamoja inapaswa kupanuliwa zaidi ya misaada ya dharura ili kujumuisha uwekezaji katika amani ya kudumu, maridhiano na ujenzi mpya baada ya migogoro. Vile vile, sera na vitendo lazima vitoe kipaumbele kwa usalama, ulinzi, na matibabu ya kibinadamu kwa wakimbizi, heshima ya kanuni ya kutowarudisha wakimbizi pamoja na utekelezaji wa hatua za kuzuia vurugu na unyonyaji. Kuungana tena kwa familia kunapaswa kupewa kipaumbele katika kutambua jukumu muhimu la familia katika maendeleo ya binadamu, ustawi wa kisaikolojia, na utulivu wa kijamii.
'Tunapokabiliwa na hali mbaya, watu wenye roho nzuri ya amani wapatikane'
Vatican, aliongeza kusema kuwa inafurahi kwamba, katika Jukwaa la Pili la Wakimbizi Duniani, Mataifa kadhaa yaliahidi kuongeza idadi ya makazi yao na kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wakimbizi wachanga. Katika muktadha huu, Kiti Kitakatifu kinasisitiza umuhimu wa mtandao unaopanuka wa ushirikiano ambao unaweza kuunganisha serikali, mashirika ya kidini, na asasi za kiraia katika kufuata na kutimiza ahadi tofauti zilizotolewa kwa wakimbizi. Papa Leo XIV anatukumbusha kwamba, "tunapokabiliwa na hali za kutisha na uwezekano wa uharibifu wa kimataifa, ni muhimu kwamba kuwe na hamu inayoongezeka katika mioyo ya watu kwa mustakabali wa amani na heshima kwa utu wa wote. Hisia hii inatoa mwanga wa matumaini katikati ya kukata tamaa. Hatimaye, Mwakilishi wa Vatican alitumia wakati huo kumpatia shukrani kutoka Kiti Kitakatifu kwa Bwana Filippo Grandi, Kamishna wetu Mkuu kwa muongo mmoja uliopita, na kutambua huduma yake ya kujitolea kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi. Alimshukuru sana Kamishana huyo.