Papa akutana na Waziri Mkuu wa Lebanon
Vatican News
Katika matarajio ya ziara ijayo ya Kitume ya Papa Leo XIV ya kwenda nchini Lebanon, iliyopangwa kufanyika Novemba 30 hadi tarehe 2 Desemba 2025, Jumamosi asubuhi tarehe 25 Oktoba 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam akiambatana na Naibu Waziri Mkuu Tarek Mitri katika Mkutano uliyofanyika mjini Vatican.
Baadaye, alikutana na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, akifuatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Vatican wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa.
Wakati wa majadiliano, kulingana na taarifa kutoka Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican, "matarajio ya pamoja ya Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu yalioneshwa." Baadaye, "mkutano huo ulitambua matumaini yaliyowekwa na watu wa Lebanon katika mchakato wa mageuzi na utulivu wa nchi hiyo na kupanuka hadi muktadha wa kikanda, kwa matumaini ya pamoja kwamba utulivu kamili wa Levant nzima utapatikana hivi karibuni."