Malkia Camilla apongeza utume wa Watawa Ulimwenguni kote
Na Linda Bordoni na Angella Rwezaula- Vatican.
Malkia Camilla wa Uingereza, akiwa katika ziara yake na mme wake, alipata fursa ya kukutana na kundi la Viongozi wakuu wa Watawa wa Kike kutoka Umoja wa Kimataifa wa Mama Wakuu wa Mashirika ya Kitawa (UISG), mjini Roma siku ya Alhamisi tarehe 23 Oktoba 2025 kwa kuvutiwa sana huduma yao ya kusindikiza watu wanaoishi katika hali za migogoro, umaskini, na kuhama makazi ulimwenguni kote.
Mkutano huo ulifanyika katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Beda kufuatia adhimisho la kiekumene katika Basilika la Mtakatifu Paulo, Nje ya Ukuta, lililohudhuriwa na Mfalme Charles III na Malkia Camilla wakati wa ziara yao rasmi katika Kiti Kitakatifu. Ziara ya kuwatembelea watawa hawa ilitokea wakati Mfalme akikutana na Mkuu wa Seminari na wanafunzi, ambapo Malkia alikaribishwa na wawakilishi sita wa UISG ambao walishirikishana juu ya historia za kazi yao na utume unaowaunganisha wanawake watawa kutoka mabara mbalimbali katika huduma ya hadhi ya kibinadamu.
Mwishoni mwa mazungumzo, Masista walimkabidhi Malkia Camilla mchoro wa ishara uliyochorwa na Sr Sandra De Filippis, mwanachama wa Talitha Kum, mtandao wa kimataifa wa Umoja huo (UISG) wa kupambana na biashara haramu ya binadamu. Mchoro huo unaonesha nyuso za wanawake na watoto waliojeruhiwa, lakini wenye uthabiti ambao wamenusurika na biashara haramu ya binadamu, na katikati kwenye mchoro, kuna mkono ulionyooshwa wenye ndege karibu kutaka kuruka. Mchoro unanawakilisha hali zote ambazo ni mateso na mabadiliko, ukumbusho, kama Sr Abby Avelino, Mratibu wa Kimataifa wa Talitha Kum, alivyoeleza, kwamba “hata katika maumivu makali, kunaweza kuwapo mwanga, uzuri, na tumaini.”
Malkia aliwashukuru Masista kwa zawadi na kwa historia zao. “Inagusa sana kusikia kile mnachokifanya,” alisema. “Nanyenyekeshwa na kazi yenu na kwa nguvu na ujasiri wa wale mnaowahudumia.”
Familia ya Kimataifa ya Wanawake Watawa
Akilitambulisha kundi hilo, Sr Roxanne Schares, Katibu wa UISG, alielezea utume na upeo wa shirika hilo. “Umoja wa Kimataifa wa Wakuu wa Mashirika ya kike ya Kitawa unakusanya pamoja zaidi ya viongozi 1,900 wa Mashirika ya kitawa kutoka nchi 95,” alisema. “Pamoja, tunawakilisha takriban Masista 600,000 wanaoishi na kufanya kazi katika utumishi kwa watu wa Mungu katika shule, hospitali, kambi za wakimbizi, misheni za vijijini, na jumuiya ambazo mara nyingi ziko pembezoni.”
Sr Roxanne alielezea UISG kama “mtandao wa ushirika na mshikamano,” unaounganisha wanawake watawa wanaojishughulisha na elimu, huduma za afya, kazi za kijamii, utetezi, na haki ya ikolojia. “Masista wetu hawajafungwa katika Konventi; wapo ulimwenguni wakiandamana na wahamiaji, wakimbizi, watu waliofanyiwa biashara haramu, na maskini,” alisema.
Wakimbizi ni Mahujaji wa Tumaini
Akifafanua juu ya uzoefu wake mwenyewe wa umisionari, Sr Roxanne alikumbuka miaka yake kumi ya huduma nchini Kenya na Huduma ya Shirika la Yesu kwa Wakimbizi (Jesuit Refugee Service). “Wakimbizi niliokutana nao kwa hakika ni mahujaji wa tumaini,” alisema. “Wanaacha nyumba zao katika hali za kukata tamaa, wakitafuta maisha na ulinzi kwa ajili ya familia zao. Ujasiri na uthabiti wao ni ushuhuda wenye nguvu.” Alisimulia kukutana na msichana mdogo Mnyarwanda, mwenye umri wa miaka kumi na minne tu, ambaye alikimbia na dada yake wa miaka minne baada ya baba na kaka yao kutoweka. “Walifika Nairobi na kujitahidi kuishi,” alisema. “Alijifunza kufuma vikapu na, baada ya muda, alipelekwa Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia Wakimbi(UNHCR). Baadaye alihamishwa nchini Marekani, alimaliza masomo yake, na hivi karibuni alinitumia picha ya mtoto wake wa kwanza. Historia yake ni ishara ya kile ambacho tumaini linaweza kufanikisha.”
Masista Wanafanya Kazi mahali ambapo Tumaini ni Dhaifu
Miongoni mwa wawakilishi wa UISG alikuwa ni Sista Abby, ambaye alishirikisha historia ya huduma yake dhidi ya biashara haramu ya binadamu. “Ni zaidi ya utume, ni wito wa huruma. Ninapokutana na wanawake na watoto ambao wameteseka kimwili, kiakili, na kiroho, ninatambua kwamba utume wetu ni kusindikizana nao kutoka kwenye jeraha kuelekea uponyaji na uhuru,” aliendelea. “Hata katika nyakati za kukata tamaa, tunashuhudia furaha na upyaisho. Kupitia ushirikiano, hata ishara ndogo zinaweza kutoa uhai na kufungua njia za tumaini.” Alieleza kwamba Talitha Kum inafanya kazi kama mtandao wa kimataifa unaowawezesha Masista na vijana kuongeza ufahamu, kuzuia biashara haramu, na kusaidia walionusurika. “Mchoro tuliyompa Malkia,” Sr Abby aliongeza, “ni ishara ya ushirikiano huu ukumbusho kwamba pamoja, kupitia imani na mshikamano, tunaweza kubadilisha mateso kuwa mwanzo mpya.”
Masista wengine waliokuwepo ni pamoja na Sr Patricia Murray, aliyewahi pia kuwa Katibu wa UISG; Sr Esperance Bamiriyo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Afya Katoliki ya Wau, Sudan Kusini; Sr Monica Joseph, Mkuu wa Shirika la Yesu na Msria; na Sr Maamalifar Poreku, Katibu Mwenza wa UISG. Hawa wote walishirikishana historia za wokovu, mipango ya maendeleo fungamani, mipango ya elimu, na juhudi za mazingira zinazolenga kuwawezesha wanawake na vijana. Pengo kati ya matajiri na maskini linaendelea kukua, ulimwengu unaendelea kugawanyika na vita, lakini wote walithibitisha kwamba wito wao unawaita kupeleka tumaini mahali ambapo maisha ni dhaifu zaidi.
Malkia Camilla: “Nanyenyekeshwa na Kazi Yenu”
Kwa upande wa Malkia Camilla alisikiliza kwa makini kila ushuhuda na kueleza mvuto wake kwa kujitolea kwa Masista. “Sikujua kama kulikuwa na Masista wengi kiasi hiki ulimwenguni kote wanaofanya kazi hii. Ni ajabu na inanyenyekeza sana,” alisema. Malkia aliwashukuru wanachama wa UISG kwa kile alichokielezea kama “kazi inayoleta mwanga katika maeneo yenye giza” na kwa ushuhuda wao wa kudumu wa imani na huruma.
Baadaye Masista walisema kwamba mkutano huo ulikuwa na alama ya unyofu, ukweli, na kuheshimiana. “Malkia aliguswa sana na historia hizo,” Sista Roxanne alisema, “na sisi, kwa upande wetu, tuliguswa na umakini wake na shauku yake ya kuelewa utume wetu.”
“Kushiriki Roho wa Mungu”
Akizungumza na Vatican News baada ya mkutano, Sista Roxanne alitafakari umuhimu wa mazungumzo hayo. “Nyakati kama hizi zinatualika kusimama na kutafakari utume wetu kuona mahali ambapo Roho wa Mungu anatuongoza. Wakati watu kama Malkia wanaonesha shauku na wasiwasi, inatutia moyo kuendelea na nguvu mpya.” Alielezea mkutano huo kama “kushiriki Roho wa Mungu kunatuwezesha kuendelea,” na akiongeza kuwa "kazi ya Masista inabaki na mizizi katika uwepo na usindikizaji. “Wengi wanaishi maisha ya unyofu na sala, wakati wengine wanatumikia wakiwa mstari wa mbele katika elimu, huduma ya afya, ujenzi wa amani na utume wa kichungaji.”
Akikumbuka tena uzoefu wake miongoni mwa wakimbizi, Sista Roxanne alisema historia ya mwanaume mmoja ambaye alikuwa alihama makazi kwa miaka 25. “Nilimuuliza nini kinamfanya aendelee." Yeye aliniambia: “Kwa Mkristo, daima kuna tumaini. Mungu anajua ni lini nitaweza kurudi nyumbani tena.” Juma chache baadaye, binti yake wa tisa alizaliwa na alimpatia jina Mungu Anajua.” “Ni imani na ustahimilivu huo, unaoendelea kuhamasisha utume wetu na tumaini letu," Sr Roxanne alihitimisha.