Tafuta

Akisukumwa na upendo wa pekee wa Kristo Msulubiwa aliyemtazama katika sura za watu fukara na wagonjwa, alianzisha Shirika la Watawa wa Mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristo (Wapasionisti). Akisukumwa na upendo wa pekee wa Kristo Msulubiwa aliyemtazama katika sura za watu fukara na wagonjwa, alianzisha Shirika la Watawa wa Mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristo (Wapasionisti).   (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 250 Tangu Afariki Dunia Mtakatifu Paulo wa Msalaba

Akisukumwa na upendo wa pekee wa Kristo Msulubiwa aliyemtazama katika sura za watu fukara na wagonjwa, Mtakatifu Paulo wa Msalaba alianzisha Shirika la Watawa wa Mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristo (Wapasionisti). Papa Pius IX alimtangaza Mwenye heri tarehe 1 Mei 1853 na Mtakatifu tarehe 29 Juni 1867. Mwaka 2025 Wapasionisti kwa furaha wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 250 tangu Mtakatifu Paulo wa Msalaba alipoitupa mkono dunia! Shujaa wa Msalaba!

Na Padre Octavian O. Hinju, CP…Kola Hills-Morogoro, Tanzania.

Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” napenda kwanza kumshukuru Baba Mwanzilishi wetu kwa mfano wake wa utakatifu na imani, uvumilivu wake na unyenyekevu mkubwa, kwa maisha yake ya kiroho na mfano mwema wa mang’amuzi ya kiuongozi yanayo endelea kulipatia shirika letu mwelekeo chanya hata sasa.” Ndugu Msikilizaji wa Radio Vatican, Kila mwaka ifikapo tarehe 19 Oktoba Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, ambaye ni Padre na Baba mwanzilishi wa shirika la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu, aliyefahamika pia kama Mwindaji wa Roho. Hivyo basi leo tuna kila sababu ya kufurahia na kusheherekea, kwanza kwa sababu mwaka 2025 ni mwaka wa kipekee unaobeba tukio muhimu la kikanisa la Jubilei kuu ambayo hayati Baba Mtakatifu Francisko alitangaza katika waraka wake unao tambulika kwa Kilatini kama “Spes Non Confundit” yaani “Tumaini halitahayarishi” (Rum. 5:5). Pili, mwaka huu sisi kama wapasionisti tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 250 tangu kuitwa kwake mbinguni mtumishi huyu aliyetolea maisha yake kiaminifu kwa fumbo la Msalaba ili kumpatia tena Kristu roho zilizo potea katika dhambi. Kumbe, kwetu sisi na Kanisa la kiulimwengu mwaka 2025 ni mwaka wa kipekee wenye kutuletea neema na Baraka tele za Kristu Mshindi. Mt. Paulo wa Msalaba alizaliwa kama Paolo Francesco Danei huko Ovada nchini Italia mnamo tarehe ya 3 ya Januari 1694. Alifariki huko jijini Roma, tarehe 18 Oktoba 1775. Alikuwa Padri hodari ambaye tangu ujanani aling’aa kwa roho ya toba na ari ya utume kwa watu maskini.

Miaka 250 tangu Mt. Paulo wa Msalaba afariki dunia
Miaka 250 tangu Mt. Paulo wa Msalaba afariki dunia

Akisukumwa na upendo wa pekee wa Kristo Msulubiwa aliyemtazama katika sura za watu fukara na wagonjwa, alianzisha Shirika la Watawa wa Mateso ya Bwana Wetu Yesu Kristo (Wapasionisti). Papa Pio IX alimtangaza Mwenye heri tarehe 1 Mei 1853 na Mtakatifu tarehe 29 Juni 1867. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, Sikukuu ya mwaka huu ni ya kipekee kwetu sote kama familia ya Watawa wa mateso kwa sababu inaangukia katika tarehe ile ile ya 18 Oktoba 1775 jioni tukufu aliyoitwa Baba Mwanzilishi wetu huko mbinguni kuungana na muumba wake; tukio ambalo lilitokea katika makao makuu ya shirika letu jijini Roma, nchini Italia. Ni katika muktadha huo tukiwa na tumaini la kuungana naye siku moja tunakusanyika kwa furaha ili kusherehekea maadhimisho ya miaka 250 tangu kifo cha shujaa wa Msalaba aliyetoa uhai wake kwa ajili ya kutangaza pendo la Kristu Msulubiwa kwa watu wote. Akiwaandikia wanafamilia ya kipasionisti na taifa la Mungu ulimwenguni kote katika kuelekea maadhimisho ya mwaka huu, Mkuu wa Shirika letu duniani Mheshimiwa sana Padre Giuseppe Adobati Carrara, CP. Ana tanabaisha kwamba, “katika maadhimisho ya mwaka huu Mtakatifu wa Jubilei yenye kubeba kauli mbiu kwamba: “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” napenda kwanza kumshukuru Baba Mwanzilishi wetu kwa mfano wake wa utakatifu na imani, uvumilivu wake na unyenyekevu mkubwa, kwa maisha yake ya kiroho na mfano mwema wa mang’amuzi ya kiuongozi yanayo endelea kulipatia shirika letu mwelekeo chanya hata sasa.”

Wapasionisti wakikutana na Hayati Papa Francisko.
Wapasionisti wakikutana na Hayati Papa Francisko.   (ANSA)

Ili kuweza kumuelewa Mt. Paulo wa Msalaba, utume na maisha yake pamoja na urithi alioliachia Shirika na Kanisa la Mungu basi ni lazima tuwe tayari siku zote kujifunza kutoka kwake kwanza uvumilivu mkuu uliomuwezesha kuliongoza na kulisimamia shirika mpaka kufa hata kama afya yake iliendelea kuzorota siku hata siku. Katika hali ya ugonjwa ama uzee, ni kawaida kwa mtu kuomba pengine kupumzika au kutafuta usaidizi kutoka kwa mtu au mahali pengine. Lakini hali ilikuwa tofauti kwa Mtakatifu Paulo wa Msalaba. Yeye aliyatoa mateso na maumivu ya mwili wake ili yawe kweli sadaka yenye maana machoni pa Mungu kwa ajili ya Kristu na watu wake. Ni wito na mwaliko kwetu sote kama waamini wabatizwa kujizamisha katika fumbo takatifu la msalaaba ili tuweze kujichotea fadhila ya uvumilivu hasa katika shida, magumu, mahangaiko na dhiki za maisha yetu ya kila siku. Uvumilivu hutuongoza daima kuielekea njia ya Kristu. Njia ya Kristu ni njia ya Msalaba, yenye uchungu mwingi, maumivu makali na magumu yasiyo koma lakini ni njia yenye uhakika na uzima wa milele, Kisha akawaambia watu wote, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate. Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayaokoa. Je, kuna faida gani mtu kuupata utajiri wote wa dunia kwa kujipoteza au kujiangamiza yeye mwenyewe? Mtu akinionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu,” (Yoh. 9:23-26).

Mtakatifu Paulo wa Msalaba Shujaa wa Mateso
Mtakatifu Paulo wa Msalaba Shujaa wa Mateso   (ANSA)

Ndugu Msikilizaji na msomaji wa Radio Vatican, Ni dhahiri kwamba mwanadamu hapendi kuteseka lakini ni katika kumwiga Kristu Yesu ndipo nasi tunaweza pasi na shaka kuiendea njia ile ya Yesu. Njia ya Yesu ni njia ya mateso na msalaba. Ni njia yenye uchungu na maumivu lakini tofauti na njia nyingine za kibinadamu, njia hii huleta wokovu, huleta ushindi, huleta furaha idumuyo hata milele, “Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu, (Flp. 3:8-11) Naye Mtakatifu Paulo wa Msalaba alipo yatafakari hayo yote alifundisha akisema kwamba “Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu ni kama bahari yenye kina kirefu, mwombe Kristu akupe ujasiri wa kuogelea katika kina cha bahari hiyo.” Kumbe mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kabla ya kuogelea katika kina cha bahari ya mateso ya Kristu, mwombe kwanza akuongezee imani (Lk. 17:5) ili kwa zawadi hiyo ya imani uwe na ujasiri wa kusafiri nae katika njia yake kama wale wanafunzi wawili kuelekea kijijini Emau (Lk. 24:13-35).

Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya uzima wa milele
Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni chemchemi ya uzima wa milele   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika Wosia wake wa Kitume “Dilexi te yaani “Nimekupenda” Kuhusu Upendo kwa Maskini (Ufu 3:9) uliotiwa saini, tarehe 4 Oktoba 2025 katika kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, na kuzinduliwa rasmi tarehe 9 Oktoba 2025, kama sehemu ya mwendelezo wa Waraka wa Kitume ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko “Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo, akiongozwa na tasaufi ya Kifranciskani, Baba Mtakatifu Leo XIV anafundisha akisema kwamba, “Nina shawishika kuamini kwamba mafungamano, chaguo na pendo kwa maskini ni chanzo cha upyaisho wa ajabu kwa Kanisa na kwa jamii, ikiwa tunaweza tu kujiweka huru kutoka katika ubinafsi wetu na kufungua masikio ya mioyo yetu ili kusikiliza kilio chao.” (Dexile te, n. 7). Uvumilivu kama tunu msingi ya kikristu humfanya mtu aachilie nafsi ya hata ipatwe na magumu ili kumfuasa Kristu kwa moyo radhi wa ibada na shukrani. Pia ni nyenzo nzuri ya ibada na huruma kwa jirani kiasi cha kutojifikiria yeye mwenyewe kama anavyo tutafakarisha Baba Mtakatifu Leo wa XIV. Kumbe roho hii ilionyeshwa kwetu pia na Baba Mwanzilishi wetu Mtakatifu Paulo wa Msalaba pale alipojitoa kushiriki kama Baba Mwanzilishi wa shirika na kiongozi mkuu hata kama alikuwa tayari amechoka kutokana na maradhi yatokanayo na uzee kiasi cha kupigiliwa misumari katika kitanda chake. Tendo hili la kuyavumilia yale yanayo tuumiza litupe hamasa nasi kuwa tayari kukwepa kasumba ya kulalamika pale tunapoitwa kushiriki mateso ya Kristu kwa namna ya utume na maisha yetu ya kila siku kama waamini wabatizwa. Ni wazi kuwa tunayaonja mateso kila siku katika maisha yetu ya kila siku ya ndoa, imani na kazi zetu, na tuyatoe kwa Kristu ili ayageuze kuwa kwetu chanzo neema na Baraka.

Miaka 250 Tangu alipofariki dunia Mt. Paulo wa Msalaba
Miaka 250 Tangu alipofariki dunia Mt. Paulo wa Msalaba

Kwingineko sisi kama watawa wa shirika la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu, kumbukumbu hii ya miaka 250 tangu kifo cha Baba Mwanzilishi ni nafasi ya pekee mno kwetu tulio mahujaji wenye matumaini kuona namna mateso ya Kristu yanavyo tubidiisha. Katika mtazamo wa kisinodi tunaitwa kuyatazama mateso kwa moyo wa shukrani na upendo, unabii na tumaini kama tulivyo tumwa na Mkutano wetu mkuu wa shirika wa mwaka 2018. Kama tunavyoitwa tena na tena naye Mungu mwenyewe kwa njia ya maisha ya Mt. Paulo wa Msalaba, kumuhubiri Kristu Msulubiwa, tusali daima kuomba neema ya kuielewa, kuishika nakuiishi karama ya shirika letu (Memoria Passionis) kwa maneno, matendo na mienendo yetu inayofaa machoni pa Mungu Baba mwenye huruma. Katika kuiishi karama yetu yaani “Memoria Passionis” kufanya hai kumbukumbu ya mateso ya Yesu ndipo nasi tunajitwalia utambulisho wetu kama watawa. Tunapotafakari mwaka huu juu ya fadhila ya kikristu ya uvumilivu kwa mfano wa maisha ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, tunakumbushwa ukweli kwamba ni katika kuyavumilia mateso ndipo tunaweza kutambua kusudi la kuumbwa kwetu na mpango wa Mungu ndani mwetu kama alivyo fanya Bikira Maria Mama wa mateso, “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi” (Lk. 2:34-36), “Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake” (Lk. 2:19). Fadhila ya uvumilivu katika maisha ya mkristu humsaidia kuleta mageuzo ya ndani na upyaisho wa maisha kama anavyo endelea kutufundisha hayati Baba Mtakatifu Francis katika ujumbe wake alio watumia wajumbe wa mkutano mkuu wa shirika letu mnamo mwaka 2018.

Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Shujaa wa matumaini
Mtakatifu Paulo wa Msalaba: Shujaa wa matumaini

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa kusema kwamba, “ninafahamu kwamba tafakari ya mkutano wenu mkuu inawaongoza ninyi wenyewe katika upyaisho wa utume wenu kwa kuangazia mambo makuu matatu- shukrani, unabii na matumaini. Shukrani ni uzoefu wa kukumbuka yaliyopita katika mtazamo wa magnificat-utenzi wa Mama Maria wenye shukrani na kutembea kuelekea kesho yenu kwa mtazamo wa kiekaristi.Shukrani zenu ni matokeo ya kumbukumbu hai ya mateso ya Kristu yaani “Memoria Passionis.” Wale wote wanao zama katika tafakari ya kina na kujihusisha katika kuutangaza upendo wa Kristu tuliopewa pale juu msalabani, wanauelezea ukweli huu wa kihistoria na maisha yao hujazwa furaha. Hili linawezekana kwa wale tu wanao chota nguvu katika sala kama pumzi ya maisha ya roho zao na kuvuta hewa safi ya Roho Mtakatifu katika vilindi vya mioyo yao kwa kila kiumbe.  Kumbukumbu ya mateso ya Kristu iwafanye kuwa kweli manabii wa upendo wa Msulubiwa katika ulimwengu unaondelea kupoteza hisia na maana halisi ya upendo. Tumaini ni uwezo wa kuona katika mbegu inayokufa ngano inayo chanua, inayo zalisha kiu, sitini, na nyingine mia na zaidi. Ni swala la kutambua katika parokia na jumuiya zenu za kitawa mbazo zimeanza kufifia nap engine kufa kabisa, tendo endelevu la Roho Yule anaye tuhakikishia sisi sote kwamba huruma ya Mungu haita tupungukia. Tumaini humaanisha kufurahia kilichopo badala ya kulalamikia kile tulichokikosa. Kwa hali yoyote ile, usiruhusu kupokonywa anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”,83.” Tunapo sherehekea miaka 250 tangu kifo cha Mtakatifu huyu mwema sana wa Mungu, tusali kuomba neema ya kuvumilia ili tusije tukajikuta katika shimo la lawama na manung’uniko yanaweza kututenga na neema ya Mungu. Nawatakia heri na baraka tele za sikukuu ya Mt. Paulo wa Msalaba. Mateso ya Bwana wetu Kristo Yesu yawe daima moyoni mwetu. Tumsifu Yesu Kristo.

 

18 Oktoba 2025, 16:03