Toleo la XII la masaa 24 kwa ajili ya Bwana tarehe 28-29 Machi 2025!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Mwaka huu wa Jubilei, toleo la XII la Masaa 24 kwa Bwana, ambao ni mpango wa Kwaresima, unaojikita kwa sala na upatanisho ulioanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko, litaadhimishwa katika majimbo Ulimwenguni kote. Kama ilivyokuwa katika matoleo yaliyotangulia, tukio litafanyika usiku wa kuamkia Dominika ya Nne ya Kwaresima, kuanzia Ijumaa tarehe 28 Machi hadi Jumamosi tarehe 29 Machi 2025. Kwa toleo hili, ndani ya Jubilei kuu ya mwaka 2025, iliyojitolea hasa ajili ya Tumaini, kauli mbiu iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu ilichukuliwa kutoka katika maneno ya Mtunga Zaburi, “Wewe ni tumaini langu” (Zab. 71:5).
Kila Jubilei ina maana yake
Kila Jubilei ina namna yake maalum ya kuishi, kwa sababu ya muktadha wa kihistoria na kwa sababu ya hali ya kina ya maudhui yake na njia madhubuti ya kuitambua kulingana na nia ya Baba Mtakatifu, ambayo inaoneshwa hasa katika Hati ya Kutangaza Jubilei kuu. Jubilei ya 2025 imewekwa katika nuru ya Kauli mbiu isemayo , “Spes non confundit,” yaani “Tumaini halikatishi tamaa,” kutoka katika Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Warumi. Kwa hiyo Mwaka huu Mtakatifu ni Jubile ya Matumaini, ambapo kila mtu, popote alipo ulimwenguni, anaalikwa kuwa “Mhujaji wa Matumaini.” Katika kufanikisha maandalizi ya Toleo hili la Masaa 24 kwa Bwana, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Unjilishaji,, Askofu Mkuu Rino Fisichella aliandika mwongozo wa kuwaongoza kila mtu ajiandae vema kupokea sakramenti ya kitubio, ambapo katika maoni yake alisema kuwa “mwongozo huo umekusudiwa kutoa mapendekezo ya kusaidia parokia na jumuiya za Kikristo ulimwenguni kote kujiandaa kukabiliana na mpango huu. Bila shaka, haya ni mapendekezo yanayoweza kubadilishwa kulingana na mahitaji na desturi za mahalia.” Askofu Mkuu Fisichella alisema kuwa “Kusudi la tukio ni kuweka sakramenti ya upatanisho katikati ya maisha ya kichungaji ya Kanisa, na kwa sababu hiyo, ya jumuiya zetu, parokia, na ukweli wote wa kikanisa. Na hicho ndicho ndicho kiini cha ujumbe wa Injili: Huruma ya Mungu, ambayo inatupatia uhakika kwamba mbele za Bwana hakuna mtu atakayemkutana hakimu, bali atapata Baba ambaye anamkaribisha, kumfariji na pia kumwonesha njia ya kujipyaisha.”
Vifungu vya KKK kuelezea Sakramenti ya kitubio
Katika maandalizi ya Dominika ya Pasaka, Ijumaa jioni na siku nzima ya Jumamosi, inapendekezwa kwamba jumuiya za kikanisa ziandae makanisa yote ili kuwapa waamini nafasi ya kusimama wakati wowote katika ibada na nafasi ya kuungama. Hata hivyo ili kufafanuliwa zaidi, tunaweza kusoma katika Mafundisho ya Kanisa. Sakramenti ya uponyaji, sakrameti ya toba na ya upatasho inavyoelezwa kutoka katika Hati ya katekesimu ya Kanisa Katoliki (KKK), kifungu cha 1422 kwamba “Wale wanaoikaribia Sakramenti ya Kitubio wanapokea kutoka katika huruma ya Mungu msamaha wa makosa waliyotendewa na wakati huo huo wanapatanishwa na Kanisa, ambalo wamelitia jeraha la dhambi na ambalo linashirikiana katika kuongoka kwa upendo, mfano na sala”
Sakramenti hii inaitwaje?
Kifungu cha 1423 kinaeleza kuwa “Inaitwa sakramenti ya Uongofu kwa sababu inatambua kisakramenti wito wa Yesu wa uongofu, safari ya kurudi kwa Baba ambaye tumejitenga naye kupitia dhambi. Inaitwa sakramenti ya Kitubio kwa sababu inaweka wakfu safari ya kibinafsi na ya kikanisa ya wongofu, toba na kuridhika kwa Mkristo mwenye dhambi. Na Kifungu cha 1424, kinabainisha kuwa “ Inaitwa sakramenti ya Kuungama kwa sababu shtaka, ungamo la dhambi mbele ya kuhani ni kipengele muhimu cha sakramenti hii. Kwa maana ya kina pia ni “maungamo”, utambuzi na sifa ya utakatifu wa Mungu na huruma yake kwa mwanadamu mwenye dhambi. Inaitwa sakramenti ya Msamaha kwa sababu, kwa njia ya msamaha wa sakramenti ya kuhani, Mungu huwapa wale wanaotubu “msamaha na amani.” Inaitwa sakramenti ya Upatanisho kwa sababu inampa mwenye dhambi upendo wa Mungu anayepatanisha: “Patanishwani na Mungu” (2Kor 5:20). Anayeishi kwa upendo wa huruma wa Mungu yuko tayari kuitikia mwaliko wa Bwana: “Nenda kwanza ukapatane na ndugu yako” (Mt 5:24).
Na kwa nini iwe toba ya ndani?
Ili kuweza kujibu swali hili, tusaidiwe tena na Hati ya mafundisho ya Katekisimu ya Kanisa katoliki(KKK) kwamba, katika kufungu cha 1430 kinabainisha “Kama katika manabii, mwito wa Yesu wa kuongoka na kutubu hauhusu hasa kazi za nje, “magunia na majivu,” kufunga na kujitia moyo, bali wongofu wa moyo, toba ya ndani. Bila hivyo, matendo ya toba yanasalia kuwa tasa na yenye kuleta madhara; ubadilishaji wa mambo ya ndani badala yake hutusukuma kueleza mtazamo huu katika ishara zinazoonekana, ishara na matendo ya toba.” Kadhalika kifungu cha 1431: “Toba ya ndani ni mwelekeo mpya wa maisha yote ya mtu, kurudi, uongofu kwa Mungu kwa moyo wake wote, kuvunja dhambi, kuchukia maovu, pamoja na kukataliwa kwa matendo maovu ambayo tumefanya. Wakati huo huo, inahusisha hamu na azimio la kubadilisha maisha ya mtu kwa matumaini katika rehema ya Mungu na kutumaini msaada wa neema yake. Uongofu huu wa moyo unaambatana na maumivu na huzuni, ambayo Mababa waliita "animi cruciatus yaani ‘uchungu wa roho’, (‘compunctio cordis’; ‘contrition of the heart.’)
Kifungu cha 1432: Moyo wa mwanadamu ni mzito na mgumu. Mungu lazima amjalie mwanadamu moyo mpya. Uongofu kwanza kabisa ni kazi ya neema ya Mungu inayofanya mioyo yetu imrudie: “Uturudishe kwako, Ee Bwana, nasi tutarudi” (Maombolezo 5:21). Mungu anatupa nguvu ya kuanza upya. Ni kwa kugundua ukuu wa upendo wa Mungu ndipo mioyo yetu inatikiswa na utisho na uzito wa dhambi na kuanza kuogopa kumkosea Mungu kwa dhambi na kutengwa naye. Moyo wa mwanadamu unaongoka kwa kumtazama yule aliyechomwa na dhambi zetu. “Na tuweke macho yetu juu ya damu ya Kristo, na tufikiri jinsi ilivyo ya thamani kwa Mungu, Baba yake; kwa kweli, akimiminwa kwa ajili ya wokovu wetu, aliutolea ulimwengu wote neema ya uongofu.” Hatimaye kifungu cha 1433 kinaeleza kuwa “ Baada ya Pasaka, ni Roho Mtakatifu anayesadikisha ulimwengu kuhusu dhambi, yaani, ulimwengu haukumwamini yule ambaye Baba amemtuma. Lakini Roho huyuhuyu, afunuaye dhambi, ndiye Mfariji24 anayeupa moyo wa mwanadamu neema ya toba na wongofu.”