Mahubiri ya Kipindi Cha Kwaresima 2025: Nanga Ya Matumaini Katika Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu.
Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na kunogeshwa na kauli mbiu “Kutia nanga katika Kristo” Kukita mizizi na kusimikwa katika tumaini la maisha mapya.” Mahubiri haya ni kwa ajili ya waamini wote wanaojisikia kutaka kuboresha maisha yao ya kiroho na yanaanza saa 3:00 kwa Saa za Ulaya. Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., katika mahubiri yake ya kwanza kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2025, Mwaka wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 anawahimiza waamini kutia nanga ya matumaini katika Kristo Yesu, kwa toba na wongofu wa ndani, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa huduma kwa jirani, majaribu jangwani kwa muda wa siku arobaini, akajiaminisha mbele ya Baba yake wa mbinguni, mwaliko kwa waamini kukita matumaini yao kwa Kristo Yesu anayesema: “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, mwanzo kabisa mwa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, waamini wanaalikwa kumwangalia Kristo Yesu kama nanga ya matumaini yao, huku wakiendelea kujikita katika kutekeleza lengo waliloitiwa, yaani maisha ya mbinguni. Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanatiwa nanga ndani ya Kristo Yesu aliyeingiza ubinadamu katika patakatifu pa mbinguni mbele ya Baba yake wa milele, ambako daima anawaombea waja wake, changamoto ni kuendelea kujikita katika toba na wongofu kwa tunu msingi za Kiinjili na hivyo kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aendelee kuwaongoza, ili wawe imara katika tumaini linalobubujika kutoka katika Injili ya Kristo! Rej. Kol 1:22-23; 1Kor 3:10-11; Gal 1:6. Jambo la msingi ni toba na wongofu katika kufikiri na kutenda. Ubatizo ni tukio linalofungua maisha na utume wa Kristo Yesu hadharani, kielelezo cha upendo na mshikamano na binadamu mdhambi; chemchemi ya matumaini mapya na upendo usiokuwa na kifani kwa jirani na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Kristo kwa binadamu, kiasi hata cha kujinyima muda wa mapumziko kwa ajili ya huduma, kielelezo cha mshikamano, huruma na mapendo. Rej Mk 1:9, Mt 3:12, Lk 3:17; Mk 6:31-34.
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, baada ya Kristo Yesu kubatizwa Mtoni Yordani, wakashuhudia sauti kutoka mbinguni, akaongozwa na Roho Mtakatifu jangwani kwa muda wa siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani, Ibilisi, na akaendelea kujiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni. Mk 1: 12-13. Kristo Yesu akajaribiwa katika: Chakula, Utajiri na Mamlaka, mwaliko kwa waamini kuupokea na kuukumbatia Msalaba wa maisha yao, daima wakimwomba Mwenyezi Mungu asiwaache kishawishini bali awaokoe na yule Mwovu, Shetani, Ibilisi. Katika Kipindi cha Siku Arobaini alijiaminisha mbele ya Baba yake wa mbinguni, akawa tayari kutekeleza mapenzi yake, akajiimarisha katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi na kuendelea kutunza amani na utulivu wa ndani, tayari kuwatuma wafuasi wake kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, katika hali ya unyenyekevu. Rej Mk 6: 8-11. Kumbe, mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu unafumbatwa katika: Huruma, Ukarimu na Upendo. Mk 1: 14-15. Unaobubujika kutoka katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu na ujumbe huu kadiri ya Mwinjili Yohane unatangazwa na Kristo Yesu wakati akifanya Ishara yake ya kwanza kwenye arusi ya Kana ya Galilaya, alipogeuza maji kuwa divai, watu wakanywa na kufurahi, lakini huu ni mwaliko wa kufanya toba na wongofu wa ndani.
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anahitimisha tafakari yake ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 kwa kutoa mwaliko kwa waamini kubaki imara ndani ya Kristo Yesu, ili kubaki wakiwa na kumbukumbu imara na thabiti; kwa kuendelea kushikamana katika Injili ya matumaini tayari kuvuka Lango la huruma ya Mungu, ili kuzama zaidi katika fumbo la maisha ya Kikristo. Ubatizo wa Kristo Yesu ni ishara inayoangazia maisha na utume wake kwa kuwa makini na matumizi ya madaraka; kwa kujenga na kudumisha ushirika wenye changamoto nyingi; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kuona, kuhukumu na kupenda kama Kristo alivyopenda na kuhudumia. Waamini waendelee “kujichimbia” katika ukweli bila kuuepuka wala kuupunguza. Ubatizo wa Kristo Yesu ni mwaliko kwa waamini kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha kwa kujiaminisha mbele ya Mungu ambaye hubaki nao daima. Sala: Ee Mungu Baba Mtakatifu katika Ubatizo wa Mwanao mpendwa, ulidhihirisha wema wako kwa wanadamu, uwajalie wale waliofanywa upya kwa maji na katika Roho, kuishi kwa utauwa na haki katika Ulimwengu huu uliopokea uzima wa milele kama urithi. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Yesu, Bwana wetu!