Askofu Mkuu Giancarlo Dellagiovanna Balozi wa Vatican Nchini Burkina Faso
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 15 Machi 2025 amemteuwa Monsinyo Giancarlo Dellagiovanna kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Burkina Faso na kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu mteule Giancarlo Dellagiovanna alikuwa ni mshauri wa Balozi za Vatican kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Giancarlo Dellagiovanna alizaliwa tarehe 18 Septemba 1961 huko Voghera, Jimbo Katoliki la Tortona, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 5 Juni 1999 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa jimbo Katoliki la Tortona na kwamba, ana shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa.
Kunako tarehe Mosi, Julai 2005 alianza utume wake kwa diplomasia ya Kanisa na hivyo kubahatika kutoa huduma katika Balozi za Vatican nchini Mexico, Jamhuri ya Watu wa Dominican, Italia na hatimaye kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, Kitengo cha Masuala ya Jumla, Uholanzi na hatimaye kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Ni mbobezi katika lugha ya Kiingereza, Kihispania na Kifaransa, bila kusahau Kiitalia kama lugha mama!