Tafuta

Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” 

Mkutano Mkuu wa 20 AMECEA: Ibada ya Misa Ufunguzi DSM, Tanzania: Ujirani wa Mungu

Kardinali Tagle katika mahubiri yake amekazia kuhusu dhamiri nyofu, upendo na ukaribu wa Mungu kwa waja wake, mwaliko kwa familia ya Mungu AMECEA kudumisha ujirani mwema, ili kutangaza Habari Njema inayosimikwa katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wasimame kidete kalinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote, kwa mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA unaonogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote ndiyo mada kuu inayoongoza mkutano wa AMECEA kwa mwaka 2022 uliofunguliwa rasmi, Dominika tarehe 10 Julai 2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Nairobi na mahubiri kutolewa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na bahari ya watu kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kimsingi Waraka “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”  unazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Umuhimu wa kuenzi Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa kiikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi. Baba Mtakatifu anagusia njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni umuhimu wa elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho.

AMECEA inasema mambo makuu matatu yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle aliyemwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya katika mahubiri yake amekazia kuhusu dhamiri nyofu, upendo na ukaribu wa Mungu kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu katika Ukanda wa AMECEA kujenga na kudumisha ujirani mwema, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini wasimame kidete kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya Msamaria mwema.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili na kiutu.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili na kiutu.

Wanaitwa na kutumwa kuwaganga kwa mafuta ya faraja wale waliovunjika na kupondeka moyo; kwa kuwanywesha divai ya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika Kristo Yesu ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye aweze kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu azizi ya Msalaba wake, kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni. Rej. Kol 1:15-20. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle amewasalimia watu wa Mungu, huku akiwatakia amani na matshi mema kutoka Baba Mtakatifu Francisko, anayependa kuwaonesha upendo na uwepo wake wa karibu katika maisha na utume wao. Kwa watu wa Afrika Mashariki ni wenye huruma, bila shaka wamemhurumia kwa sababu ametoa mahubiri yake kwa Lugha ya Kiingereza. Amefafanua umuhimu wa kujenga dhamiri adilifu ambayo ni sheria ya Mungu iliyowekwa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu. Inamwamuru, wakati ufaao, kutenda mema na kuepuka mabaya. Yahukumu pia uchaguzi mmoja mmoja, ikithibitisha ulio mzuri na kulaumu ule mbaya. Hushuhudia mamlaka ya kweli kuhusu Uzuri wa juu kabisa ambako mwanadamu avutiwa; huzipokea amri. Anaposikiliza dhamiri yake, mtu mwenye busara aweza kumsikia Mungu anaposema. Kimsingi dhamiri ni sheria ya roho. Rej KKK 1776-1782.

Uchafuzi wa mazingira unaendelea kusababisha uharibifu mkubwa katika kazi ya Uumbaji na matokeo yake ni kukosekana kwa upendo na vita kutawala. Watu wa Mungu kutoka Ukanda wa AMECEA, wamekushanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayosimikwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, mwaliko kwa waamini kushuhudia uwepo na ujirani wa Mungu katika maisha yao. Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini dhamiri adilifu, ili kutambua mapenzi ya Mungu na kuyatekeleza katika maisha yao. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle anasema Kristo Yesu ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika Kristo Yesu ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye aweze kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya amani kwa damu azizi ya Msalaba wake, kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo ju ya nchi, au vilivyo mbinguni. Uumbaji ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, inayoonesha ile chapa ya Mungu katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Na kwa mtazamo huu, Kristo Yesu anakuwa ni njia inayowaongoza waamini kwa Baba wa milele. Wanandoa hata katika shida, magumu na changamoto za maisha yao, wajitahidi kumwona Kristo Yesu kati pamoja nao, kama kielelezo cha uwepo na ukaribu wa Mungu katika maisha yao.

Uchafuzi wa mazingira ni chanzo cha vita, maafa na majanga katika maisha ya mwanadamu
Uchafuzi wa mazingira ni chanzo cha vita, maafa na majanga katika maisha ya mwanadamu

Kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, hata waamini wanapaswa wajitahidi: kuona, kuhurumia, kukaribia na kuwahudumia jirani zao waliojeruhiwa. Wamwone, Kristo Yesu kati ya watu waliojeruhiwa kiroho na kimwili. Kwa hakika, yule mtu aliyejeruhiwa ni Kristo Yesu, mwenyewe. Na kwamba, jirani ni mtu yeyote aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, maskini na mtu ambaye anahitaji kuonjeshwa huruma na upendo. Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni Wasamaria wema, kwa kuonesha ukaribu wa Mungu kwa waja wake na kamwe wasiwageuzie watu kisogo. Wawe na huruma kwa maskini na wahitaji kwani huu ndio msingi wa Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya ujirani mwema na ujenzi wa urafiki na udugu wa kibinadamu kwa watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA, Afrika na katika Ulimwengu mzima. Mwenyezi Mungu daima anapenda kuonesha ukaribu kwa waja wake. Kumbe, huruma na upendo, viwe ni vielelezo vya uwepo na ukaribu wa Mungu kwa watu wake.

Kwa upande wake, Kardinali John Njue, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Nairobi katika utangulizi, amewaombea watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA mwanga wa ukweli, ili waweze kurejea katika njia ya haki. Wakristo wayakatae mambo yote yanayopingana na Ukristo wao na kufuata yale yanayopatana na jina hilo. Wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia nguvu ya kutosha kuwashughulikia watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA. Naye Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amewakaribisha watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa Mkutano wa Mkuu wa 20 wa AMECEA, ambayo imehudhuriwa na kufuatiliwa na bahari ya waamini kutoka ndani na nje ya Ukanda wa AMECEA. Hii ni Ibada ya Misa Takatifu ambayo imepiga chapa kumbukumbu ya kudumu katika maisha na utume wa watu wa Mungu Ukanda wa AMECEA kutokana na dhamira yake inayowataka watu wa Mungu kusimama kidete: Kulinda, kutetea na kuhifadhi mazingira nyumba ya wote, ili mwanadamu aweze kupata maendeleo ya kweli yanayogusa mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili.

AMECEA 2022: Misa Ufunguzi

 

10 July 2022, 14:48