Tafuta

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, tarehe 12 Julai 2022 amepata fursa ya kuwahutubia wajumbe wa AMECEA, Jijini Dar es Salaam Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, tarehe 12 Julai 2022 amepata fursa ya kuwahutubia wajumbe wa AMECEA, Jijini Dar es Salaam 

Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA: Hotuba ya Rais Samia S. Hassan

Katika hotuba yake amekazia ushirikiano wa Serikali na wadau wa utunzaji bora wa mazingira na kwamba, Papa Francisko anatoa kipaumbele kwa mazingira. Dar es Salaam inazidi kung’aa kwa usafi Barani Afrika. Tanzania imezindua sera mpya ya mazingira. Utunzaji wa mazingira ni tema ambayo imejadiliwa kwa kina na mapana katika Vitabu vitukufu; Magonjwa, Amani na Mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tanzania ni mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA uliofunguliwa rasmi Dominika tarehe 10 Julai 2022 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali John Njue, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Nairobi, Kenya na mahubiri kutolewa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam. Mkutano unanogeshwa na kauli mbiu: “Utunzaji wa Mazingira kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu.” Hii ni kauli mbiu inayochota maudhui na utajiri wake kutoka katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Jumanne, tarehe 12 Julai 2022, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewahutubia wajumbe wa AMECEA katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Jijini Dar Es Salaam. Katika hotuba yake amekazia ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau mbalimbali katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Utunzaji bora wa mazingira ni kati ya vipaumbele vinavyotolewa na Papa Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Dar es Salaam inazidi kung’aa kwa usafi Barani Afrika. Serikali ya Tanzania imezindua sera mpya za mazingira. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni tema ambayo imejadiliwa kwa kina na mapana katika Vitabu Vitukufu kwa Dini, Maradhi mapya na hatimaye, umuhimu wa kudumisha amani kama sehemu ya uwajibikaji na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Rais Samia Suluhu Hassan Akihutubia Wajumbe wa AMECEA
Rais Samia Suluhu Hassan Akihutubia Wajumbe wa AMECEA

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwanza kabisa amewakaribisha wajumbe wa AMECEA nchini Tanzania na kwamba baada ya kazi ngumu kwa wale wageni waliotoka nje ya mipaka ya Tanzania watakuwa na muda wa kuzunguka na kuiona vema Tanzania. Waheshimiwa Maaskofu, Wajumbe wa kutano huu, Mabibi na Mabwana nimejulishwa kuwa mnakutana hapa Dar es Salaam – Jiji letu la kibiashara, linalojulikana kama jiji la amani kujadili mambo ya mazingira ya nchi zetu mbalimbali chini ya kaulimbiu ya “Athari za Mazingira Katika Maendeleo ya Binadamu” yaani “Environmental Impact on Intergral Human Development.” USHIRIKIANO NA SERIKALI: Natoa pongezi kwenu kwa kuchagua mada hii muhimu kwa mataifa yetu na kwa utayari wenu kwa kushirikiana na serikali duniani kote katika kupambana na tabianchi na uchafuzi wa mazingira. Vita hii si ya mmoja kwani mazingira yakichafuka ni majanga kwa viumbe wote na ulimwengu mzima kwa ujumla. Kama alivyosema Askofu Kasonde hapa, na nilikuwa nam-quote katika matamshi yake ambaye naye pia ali-quote pengine, alisema: “Kila kitu kwenye Dunia hii ni kiumbe cha Mungu, tukiheshimu na tukitunze”. Na huu ndiyo utunzaji. Lakini niwapongeze kuwa mmechagua kujadili na kutekeleza kwa vitendo mambo ambayo tumeamrishwa na ulimwengu kupitia Maendeleo Endelevu ya Dunia – yale malengo 17. Lengo la 17 ambalo ndiyo ninawapongeza zaidi linasema Partnership for the Goals. Tufanye umoja katika kutekeleza haya malengo tuliyojiwekea.

DUNIA NI NYUMBANI KWETU SOTE: Mimi niwashukuru sana kwa kufikiria na mkifika hapa mnakwenda kuendeleza kwa vitendo malengo ya dunia lakini malengo yetu Umoja wa Afrika. Kwa hiyo hongereni sana Makardinali na Viongozi wote wa Dini. Aidha inatiatia moyo sana kuona hata Baba Mtakatifu Francisko ameona inafaa suala la utunzaji wa mazingira kuwa sehemu ya ujumbe na mpango mkakati wenu ili lipate msukumo zaidi na kama alivyoeleza Baba Mtakatifu, Dunia ndiyo nyumba yetu sote, yaani “Earth is our common home.” Hakika sisi hapa Tanzania tunathamini maisha ya kijamii (community life) yanayoendana na mkakati huo wa Kanisa Katoliki, kwamba sasa tuijenge nyumba yetu sote.

Waamini walioshiriki katika Ibada ya Ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa AMECEA
Waamini walioshiriki katika Ibada ya Ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa AMECEA

DAR ES SALAAM YA SITA KWA USAFI BARANI AFRIKA: Ndugu zangu Viongozi wa Dini, Watanzania tumetiwa moyo sana kwamba jiji la Dar es Salaam limetangazwa na Jarida la “African Tour Magazine” kuwa jiji la sita kwa usafi barani Afrika. Na tumetoka mbali; kwa wale wanaoikumbuka Tanzania miaka kidogo ya nyuma tulikuwa na vijibanda na vimwamvuli kwenye kila street. Lakini kwasababu ya kutekeleza malengo tuliyowekewa na Umoja wa Afrika na Dunia tumeweza kuisafisha Dar es Salaam na vivyo hivyo tunasafisha majiji mengine kama Mwanza, Mbeya, Dodoma na kwingine kote pamoja na Ausha. Kwa wale waliopita Arusha, tupo kwenye jitihada za kusafisha majiji yetu. Nimefurahi sana kuwa mkutano huu unafanyika katika jiji la Dar es Salaam.

SERA MPYA YA MAZINGIRA: Hivi karibuni tumezindua Sera mpya ya Mazingira chini ya Wizara yenye dhamana. Maeneo makubwa yaliyotiliwa makazo ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji na misitu. Lakini pia upandaji miti na kuhakikisha kuwa miji yoye ina mpango wa usafishaji mazingira kwa kila wiki na hasa katika makaziya watu, ya viwanda pamoja na maeneo ya biashara. Nataka niwashukuru sana viongozi wa dini. Tumekuwa tukifanya kazi pamoja hasa kwenye maeneo ya kulinda vyanzo vya maji, misitu na upandaji wa miti. Kila ninapotembea kwenye taasisi za dini najionea kwa macho yangu. Waheshimiwa Viongozi wa Dini, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifuata siasa ya maendeleo jumuishi – “Inclusive Development Policy.” Hii ina maana tupo tayari wakati wote kuzipokea taasisi zisizo za kiserikali kama taasisi za kidini lakini taasisi za kijamii likiwemo Kanisa la Katoliki na kufanya kazi nalo.

Wajumbe wa AMECEA wakisikiliza hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan
Wajumbe wa AMECEA wakisikiliza hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan

VITABU VYA DINI NA UTUNZAJI BORA WA MAZINGIRA: Mwenyezi Mungu ameumba kila kwa kipimo, na tunapoharibu kipimo kile tunaharibu maisha yetu. Tunapokwenda kutunza vipimo alivyotuumbia tunatunza maisha yetu wenyewe. Na tunaona mifano hai; tunakata misitu, joto alilotuumbia Mwenyezi Mungu limebadilika sasa limeongezeka kwa sentigredi 2 kwasababu tumekata misitu bila kupanda mingine. Kina cha bahari nacho kimepanda, hakipo kama vile Mwenyezi mungu ametuumbia. Mwenyezi Mungu ametuumbia kila kitu kwa pimo ili tuvitumie na tusidhurike. Quran Tukufu pia inasema: Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwishatengenezwa. Mungu alishatutengenezea na kututaka tusifanye uharibifu katika nchi. Lakini, papo hapo ametutuma tutumie alivyoviumba lakini tusifanye uharibifu. Kuna maradhi ambayo huko nyuma hayakuwepo lakini kwakuwa tunaharibu misitu vile viumbe ambavyo ilikuwa vihifadhiwe huko misituni sasa vinasambaa vinakuja kwa wanadamu. Kuna kila aina ya maradhi mapya yanazuka hambayo hatukuwa nayo.

MARADHI MAPYA: Nilikuwa nazungumza na Waziri Mkuu juzi, ametoka ziara Mikoa ya Kusini Lindi, ameniambia ameona maradhi mapya yameingia, watu wanatokwa na damu za pua na wanadondoka chini. Hatujui ni kitu gani, wanasayansi wamehamia huko kwa uchunguzi zaidi kwa kuwa ni watu wengi wanaougua kwa mfululuzo, na yote ni kwa sababu tunaharibu makazi ya viumbe kule walikowekwa na Mungu, tunawasogeza kwetu wanatuletea maradhi.

Vita, migogoro na kinzani ni vyanzo vikuu vya uharibifu wa mazingira duniani.
Vita, migogoro na kinzani ni vyanzo vikuu vya uharibifu wa mazingira duniani.

AMANI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA: Waheshimiwa Viongozi wa Dini, bila shaka sote tunatambua umuhimu wa amani katika kutunza mazingira. Vita na migogoro vinachangia sana katika uharibifu wa mazingira. Kunapotokea vita, hakuna mtu anajali atunze msitu. Kama ni mbio msituni, ni mbio msituni. Watu wangapi, tutaelemea hukohuko. Tunapaswa kuhakikisha tunakuwa na amani katika maeneo yetu wakati wote ili tusiende kuharibu mazingira. Ni jukumu letu Viongozi wa Dini, wa Kisiasa na wa Kimila - sote kwa pamoja kuyaombea mataifa yetu na kuyakabidhi mataifa yetu mikononi mwa Mungu ili amani iweze kutawala na kutusaidia kuhifadhi ikolojia yetu nzuri ambayo Mungu ametuumbia au ameturuzuku.

TUKISIMAMA PAMOJA TUTAFIKA TUNAPOTAKA: Vilevile nitumie majukwaa yetu ya kiroho kuwahimiza waumini na wao kuendelea kutunza mazingira yao. Waheshimiwa Viongozi wa Dini, nina hakika endapo tutasimama pamoja katika kusimamia mazingira yetu basi kwa jitihada hizi zinatusaidia kufikia mustakabali mwema wa maisha na maendeleo ya mwanadamu. Niwaombe, serikali yenu ni sikivu, ni serikali inayopokea. Leteni maoni yenu kwenye utunzaji wa mazingira, tukae kwenye vikao. Leo mmekaa wenyewe kuhusu suala la mazingira, tungependa kupata maazimio yenu tukaona tunayameza vipi kwenye sera zetu na Mh. Waziri yupo hapa. Halafu sote tukaenda kutekeleza ili kulinda hazina yetu, tunu yetu, nyumba yetu ambayo Mungu ametuumbia. Baada ya kusema hayo, nimseme Mungu aibariki AMECEA, Mungu aibariki Tanzania, Mungu alibariki eneo letu hili Mashariki mwa Afrika, aibariki Afrika yote na Dunia.

AMECEA 2022: Rais Samia
12 July 2022, 17:07