Tafuta

Idara ya Toba ya Kitume "Penitenzieria Apostolica" Imetoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili kwa Mwezi Novemba 2021 kwa waamini watakaofuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa. Idara ya Toba ya Kitume "Penitenzieria Apostolica" Imetoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili kwa Mwezi Novemba 2021 kwa waamini watakaofuata masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa. 

Mama Kanisa Anatoa Rehema Kamili Kwa Mwezi Novemba 2021

Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Kanisa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi UVIKO-19 tarehe 22 Oktoba 2020 inaendelea pia katika kipindi cha Novemba mwaka 2021. Huu ni mwendelezo wa huruma na ukarimu wa Mama Kanisa, kwa ajili ya waamini wanaotaka kuchota neema na baraka kutoka katika visima vya maisha ya kiroho, huku wakiwa wameungana na Papa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake. Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda kutokana kwamba inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili.

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama "Penitenzieria Apostolica" anafafanua: Tamko Kuhusu Rehema Kamili inatolewa na Mama Kanisa katika kipindi cha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 tarehe 22 Oktoba 2020 inaendelea pia katika kipindi cha Novemba mwaka 2021. Huu ni mwendelezo wa huruma na ukarimu wa Mama Kanisa, kwa ajili ya waamini wanaotaka kuchota neema na baraka kutoka katika visima vya maisha ya kiroho, huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, msingi na mchungaji mkuu wa Kanisa Katoliki. Tamko hili hasa linawalenga wagonjwa, wahudumu katika sekta ya afya, familia na wale wote watakaokimbilia huruma na upendo wa Mungu, wakimwomba, asitishe janga hili ambalo limetikisa watu kutoka katika undani wa maisha yao. Kristo Yesu analitaka Kanisa katika: sala, maisha, utume na utendaji wake, liwe ishara na chombo cha msamaha na upatanisho ambao amemstahilisha mwanadamu kwa gharama ya Damu yake azizi. Kardinali Mauro Piacenza anasema kwamba, hali ni tete sana katika baadhi ya nchi kiasi kwamba, hospitali hazina tena nafasi ya kuwapokea na kuwatunza wagonjwa.

Wagonjwa wametengwa na kuwekwa chini ya karantini na wengi wao wanaitupa mkono dunia bila ya kupata faraja kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki zao. Watu wanafariki dunia bila hata ya kupewa Sakramenti za Kanisa. Kwa hakika, hiki ni kipindi kigumu cha ukavu wa maisha ya kiroho. Kuna miji ambayo imewekwa chini ya karantini, hakuna kutoka wala kuingia humo ili kudhibiti maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ukubwa wa janga hili umelisukuma Kanisa ambalo kwa nguvu ya uweza wa kufunga na kufungua, lililopewa na Kristo Yesu, huingia katika manufaa ya Mkristo na hufungua hazina ya mastahili ya Kristo na ya watakatifu ili kupata kutoka kwa Mwenyezi Mungu huruma na msamaha wa adhabu zinazotokana na dhambi zao. Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba, watu wote wenye nia njema wanaonja huruma na upendo wa Mungu katika shida na mahangaiko yao ya ndani.

Ni kutokana na muktadha huu, Idara ya Toba ya Kitume: "Penitenzieria Apostolica", kwa maelezo ya Baba Mtakatifu Francisko imeagizwa kutoa Tamko Kuhusu Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Idara ya Toba ya Kitume, “Penitenzieria Apostolica” inatoa Rehema Kamili kwa watu walioshambuliwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na kwa waamini ambao wamewekwa chini ya kalantini wakiwa wamelazwa hospitalini au majumbani mwao. Ikiwa kama kutoka katika undani wa mioyo yao wataweza kutubu na hatimaye, kujiunga na vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kwa kusali Rozari Takatifu, Kufanya Njia ya Msalaba au kuhudhuria Ibada nyingine zinazotolewa na Mama Kanisa. Wajitahidi walau kusali: Kanuni ya Imani, Baba Yetu na Salam Maria kwa kutolea mahangaiko yao kwa Mwenyezi Mungu katika imani na upendo kwa jirani zao, kama njia ya kutimiza malipizi ya dhambi zao pamoja na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu, pale itakapowezekana.

Rehema hii inatolewa pia kwa wafanyakazi katika sekta ya afya na wanafamilia wote wanaowahudumia wagonjwa kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema. Rehema hii inatolewa kwa waamini watakaoweza pia kuabudu Ekaristi Takatifu, watakaoweza kusoma walau Neno la Mungu kwa muda wa nusu saa, au kusali Rozari, kufanya Njia ya Msalaba au kusali Rozari ya Huruma ya Mungu, ili kuomba huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka, ili kuwaondolea watoto wake balaa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Mama Kanisa anaendelea kusali kwa ajili ya waamini ambao hawataweza kupata fursa ya kupokea Mpako wa Wagonjwa, kwa kuwaweka chini ya huruma ya Mungu, nguvu na umoja wa watakatifu, ili hatimaye, waweze kupokea fumbo la kifo kwa amani na utulivu wa ndani. Tamko hili linawahusu wagonjwa wote kwa sababu kunahitaji zito ambalo limeletwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Sakramenti ya Kitubio inaweza kuadhimishwa kwa muundo wa adhimisho la pamoja, ambamo waamini wanajitayarisha kwa pamoja, wanaungama na hatimaye, wanamshukuru pamoja kwa ajili ya msamaha walioupokea. Hapo ungamo binafsi la dhambi na ondoleo la mmoja mmoja huingizwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, utafiti wa dhamiri, maombi ya msamaha, Sala ya Baba Yetu na Shukrani hufanywa kwa pamoja, kama kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume anaendelea kufafanua kwamba, kunapokuwepo na hitaji zito inawezekana kutumia adhimisho la pamoja; upatanisho wa pamoja, ungamo la jumla na ondoleo la jumla. Hitaji hili linaweza kujitokeza kutokana na hatari ya kifo cha ghafla. Hapa busara ya kichungaji inahitajika. Kimsingi, ungamo la mtu mmoja mmoja na kamili, pamoja na ondoleo, ndio mtindo pekee wa kawaida, ambao kwao waamini hujipatanisha na Mwenyezi Mungu, Kanisa pamoja na jirani zao. Sakramenti ya Kitubio imeundwa kwa pamoja na matendo makuu matatu yanayopaswa kutekelezwa na mwenye kutubu na ondoleo la Kuhani. Matendo ya mwenye kutubu ni toba, ungamo la dhambi au dhihirisho la dhambi mbele ya Padre na kusudi la kutimiza malipizi na kazi za malipizi.

Rehema Novemba
02 November 2021, 14:31