Tafuta

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26, Glasgow: 31 Oktoba hadi 12 Novemba 2021: Kardinali Pietro Parolin anaongoza ujumbe wa Vatican. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26, Glasgow: 31 Oktoba hadi 12 Novemba 2021: Kardinali Pietro Parolin anaongoza ujumbe wa Vatican. 

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26!

Katika mahojiano maalum na Vatican Media Kardinali Pietro Parolin, anazungumzia lengo la Vatican kuhudhuria mkutano huu, changamoto ya kitamaduni, dharura zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2015 sanjari na wongofu wa kiikolojia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland, kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 12 Novemba 2021 unafanikiwa. Hizi ni juhudi za Umoja wa Mataifa katika harakati za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lengo ni kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na hivyo kupunguza kiwango cha joto duniani. Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican ndiye anayewakilisha ujumbe Vatican kwenye mkutano huu. Katika mahojiano maalum na Vatican Media anazungumzia lengo la Vatican kuhudhuria mkutano huu, changamoto ya kitamaduni, dharura zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi sanjari na wongofu wa kiikolojia!

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland, kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 12 Novemba 2021 ni mkutano wa kwanza kufanyika baada ya maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi. Bado kumekuwepo na ugumu wa kutekelezwa kwa maazimio ya mkutano huu. Kumekuwepo na dalili za kutaka kubadili mfumo wa uchumi unaozingatia teknolojia rafiki kwa mazingira. Changamoto kubwa ni utekeleza malengo yaliyofikiwa kadiri ya muda uliopangwa. Vatican inapenda kukazia mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa na utekelezaji wake unaopaswa kufanywa kwa vitendo na nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anasema kwamba ingawa katika historia zama za viwanda zinaonekana kuwa ni zama ambazo hazikuwajibika kuhusiana na suala la mazingira, hata hivyo ipo kila sababu ya kuleta matumaini kuwa katika karne ya ishirini na moja binadamu atakumbukwa kwa majukumu makubwa aliyoyafanya kuhusiana na mazingira. Rej. Laudato si 165. Hii ndiyo changamoto ya kitamaduni anasema Kardinali Pietro Parolin inayopaswa kusaidia kuchangamotisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kulinda mazingira nyumba ya wote, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni ma jamii.

Huu ni mchakato unaopaswa kujikita katika wongofu wa kiikolojia, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mazingira nyumba ya wote; kwa kuwajali na kuwahudumia maskini sanjari na kuhakikisha kwamba, amani ya kweli inapatikana kwani hili ni jina la pili la maendeleo. Kwa ufupi, wongofu wa kiikolojia unapaswa kusimikwa katika misingi ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani kila kitu kinahusiana na kingine, na binadamu wameungana kama ndugu wamoja na kwamba, maisha yao na mazingira ni sawa na chanda na pete! Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, Nchi changa duniani zinajengewa uwezo ili kupambana na athari za uchafuzi mkubwa wa mazingira sanjari na mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Oktoba 2021 alikutana na viongozi wa kidini pamoja na wanasayansi ili kutoa Wito wa Pamoja, ili kutenda kwa uwajibikaji endelevu na fungamani. Kumbe, kuna haja kwa watu wote kujizatiti katika kutekeleza mabadiliko ya mwelekeo huu, huku wakiwa wanaungwa mkono na imani na tasaufi za dini zao. Kuna haja ya kutenda kwa kuwajibika ili kutengeneza utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kufyekelea mbali mbegu za uchoyo, ujinga, hofu, ukosefu wa haki, usalama, vurugu na vita! Yote haya yanapaswa kupata chimbuko lake katika mapambano dhidi ya kumong’onyoka kwa amali na tunu msingi za maisha ya kijamii. Umefika wakati wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na kuanza kujielekeza katika utamaduni wa kutunza mazingira kama njia muafaka ya utekelezaji wa Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2015.

Baba Mtakatifu anakazia mchakato wa wongofu wa kiikolojia kwani takwimu za Umoja wa Mataifa hazitoi matumaini makubwa mintarafu utekelezaji Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2015. Lakini jambo hili ni la dharura na linapaswa kutekelezwa haraka iwezekanavyo, ili vizazi vijavyo, visirithishwe majangwa. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland, kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 12 Novemba 2021 ni mkutano muhimu sana kwa mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa!

Parolin COP26
30 October 2021, 16:01