Kardinali Robert Sarah Ang'atuka Kutoka Madarakani mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa la kutaka kung’atuka kutoka madarakani. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa alizaliwa tarehe 15 Juni 1945 huko Ourous, Wilaya ya Koundara, nchini Guinea. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 20 Julai 1969 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre.
Tarehe 13 Agosti 1979 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu na hatimaye, kumweka wakfu tarehe 8 Desemba 1979. Tarehe 1 Oktoba 2001 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Tarehe 7 Oktoba 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Misaada ya Kiutu, Cor Unum. Tarehe 23 Novemba 2014 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Katika kipindi hiki cha uongozi wake, amepambana sana na changamoto kuhusu: Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, akajitahidi kusimamia Mapokeo ya Kanisa. Tarehe 20 Februari 2021, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani. Kumbe, ameng’atuka kutoka madarakani akia na umri wa zaidi ya miaka 75.