Tafuta

Jimbo la Kijeshi nchini Ureno limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya kiroho na uelewa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kielelezo cha ushirikiano wenye tija, ustawi na maendeleo ya wengi kati ya Serikali na Kanisa Jimbo la Kijeshi nchini Ureno limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya kiroho na uelewa tunu msingi za maisha ya Kikristo, kielelezo cha ushirikiano wenye tija, ustawi na maendeleo ya wengi kati ya Serikali na Kanisa  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV: Jimbo la Kijeshi Nchini Ureno: Huduma ya Kiroho Kwa Wanajeshi

Jimbo la Kijeshi Ureno limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya kiroho na uelewa wa tunu msingi za maisha ya Kikristo na kwamba, Jimbo hili ni kielelezo cha ushirikiano wenye tija, ustawi na maendeleo ya wengi kati ya Serikali mbalimbali na Majimbo ya Kijeshi. Papa Leo XIV anasema, hija hii ya maisha ya kiroho kwa waamini ni fursa ya kupyaisha maisha ya mtu binafsi kwa kutambua nafasi na ukuu wa Mungu katika maisha; ni fursa ya kuimarisha imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jimbo la Kijeshi la Kanisa Katoliki nchini Ureno (Ordinariato militar de Portugal) lilianzishwa kunako tarehe 29 Mei 1966 baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kutoa huduma ya maisha ya kiroho kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama, familia zao, wafanyakazi wanaoishi kwenye kambi za kijeshi au taasisi za kijeshi nchini Ureno. Tarehe 21 Aprili 1986 Mtakatifu Yohane Paulo II katika Katiba yake ya Kitume: “Spirituali Militum Curae” Yaani Huduma ya Kiroho kwa Wanajeshi” alipyaisha na kuunganisha huduma za kichungaji zinazotolewa na Kanisa Katoliki kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama na kuipatia hadhi ya Majimbo. Katiba hii ya Kitume, inaruhusu pamoja na mambo mengine, Mapadre wa Majimbo na Watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kushirikiana katika kutekeleza utume huu kama Mapadre wa Kijeshi wenye sifa zinazohitajika.  Ni katika muktadha huu, tarehe 24 Novemba 2024 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Monsinyo Sérgio Manuel Ribeiro Dinis kuwa Askofu wa Jimbo la Kijeshi nchini Ureno. Mapadre wa Jimbo la Kijeshi kutoka nchini Ureno, Jumatatu tarehe 24 Agosti 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican.

Jimbo la Kijeshi la Vikosi vya Ulinzi na Usalama Nchini Ureno
Jimbo la Kijeshi la Vikosi vya Ulinzi na Usalama Nchini Ureno   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amewakaribisha Wanajeshi wote wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama kutoka nchini Ureno, huku akiwakumbuka na kuwaombea askari wawili waliopoteza maisha yao, Ijumaa tarehe 22 Agosti 2026, wakiwa katika harakati za kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi, kama kielelezo cha Wasamaria wema. Baba Mtakatifu ameziweka roho zao mikononi mwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, pamoja na kutoa faraja kwa familia zao. Hii ni hija ya maisha ya kiroho inayofanya kumbukizi kwa kuanzishwa kwa kwa Vikarieti ya Kijeshi na hatimaye, Jimbo Katoliki la Kijeshi mwaka 1980 kuwa na Askofu wake wa Jimbo la KijeshiJimbo la Kijeshi nchini Ureno limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya kiroho na uelewa tunu msingi za maisha ya Kikristo na kwamba, Jimbo hili ni kielelezo cha ushirikiano wenye tija, ustawi na maendeleo ya wengi kati ya Serikali mbalimbali na Majimbo ya Kijeshi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hija hii ya maisha ya kiroho kwa waamini ni fursa ya kupyaisha maisha ya mtu binafsi kwa kutambua nafasi na ukuu wa Mungu katika maisha; ni fursa ya kujenga na kuimarisha imani kwa njia ya Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu sanjari na kutembelea Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani. Vikosi vya Ulinzi na Usalama vinabeba dhamana nyeti na tete ya kulinda uhuru wa nchi na utawala wa sheria, kuhakikisha usalama wa raia na kuwalinda dhidi ya dhuluma. Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi hawa wawe imara katika Bwana, wasimame imara, huku wakiwa wamejifunga kweli viunoni mwao kwa kuvaa vazi la haki, na viatu vya utayari wa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani. Rej. Efe 6:10; 14-15.

Hija hii ya kiroho iwasaidie kupyaisha maisha yao katika sala na tafakari ya Injili
Hija hii ya kiroho iwasaidie kupyaisha maisha yao katika sala na tafakari ya Injili   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “Iweni imara katika Bwana, kama yule jemadari wa Jeshi la Kirumi (senturioni) aliyemwendea Yesu huko Kapernaumu. Alizifahamu vyema tunu zinazoongoza maisha yenu: utii, nidhamu, kujitolea, uaminifu, ushirikiano, kujitoa, uwajibikaji, na ujasiri. Wakati huo huo, askari huyo alihisi hitaji la Mungu katika maisha yake; alijua kuwa wanadamu hawajitoshelezi wenyewe bali hutamani kitu kikubwa zaidi, kitu kinachopita uwezo wao wa kibinadamu. Mtumishi wake alipokuwa akiteseka sana, alimwendea Kristo Yesu, ambaye alimhakikishia kuwa angekuja kumponya. Hata hivyo, alijibu hivi: “Bwana, sistahili wewe uingie nyumbani mwangu; sema neno tu na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi, ingawa niko chini ya mamlaka ya wengine, nina askari walio chini yangu; humwambia mmoja, ‘Nenda,’ naye huenda; mwingine, ‘Njoo,’ naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ naye hufanya hivyo” Mt 8:8-9.

Jimbo la Kijeshi: Huduma za kiroho kwa wanajeshi na familia zao.
Jimbo la Kijeshi: Huduma za kiroho kwa wanajeshi na familia zao.   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika mtazamo huu, wanaweza kuona jinsi ambavyo Jemadari huyo alivyothamini mfumo wa mamlaka na jinsi kipengele hiki cha maisha yake ya kila siku kilivyounda uelewa wake kuhusu uhusiano wake na Kristo Yesu, ambaye alimtambua kama Bwana na Mungu wake. Kristo Yesu alistaajabishwa na maneno hayo na kusema: “Sijapata kuona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kubwa namna hii!” Mt. 8:10. Ingawa askari huyo alifahamu vyema mamlaka yake mwenyewe, alionesha mbele ya Mwana wa Mungu: Nguvu ya imani na ujasiri unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. Hakika, wanadamu bila kujali majukumu waliyonayo, mamlaka wanayoshikilia, au usafi wa mwenendo wao, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, sikuzote huwa na njaa ya mambo yasiyo na mwisho na kiu ya uzima wa milele. Hata hivyo, yasiyo na mwisho na uzima wa milele ni mambo yanayopatikana kwa njia ya Kristo Yesu: na kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Majimbo ya Kijeshi yaliundwa rasmi mwaka 1986
Majimbo ya Kijeshi yaliundwa rasmi mwaka 1986   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha viongozi wanaovihudumia vikosi vya ulinzi na usalama kwamba, Kanisa linawakabidhi jukumu la kukuza hali ya maisha kiroho ya wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama akisema kwamba: “Wapokeeni wote, wasikilizeni, waangazeni kwa hekima ya Neno la Mungu, simameni nao mkitenda kwa jina la Kristo Yesu mnapoadhimisha Sakramenti za Kanisa, na muwe pamoja na kila mmoja wao bila kusahau familia zao. Kutokana na utekelezaji wa huduma hii nyeti matunda yatapatikana mintarafu ukuaji wa binafsi wa mwanajeshi, katika kuishi vyema maisha ya Kikristo na kuimarika kwa moyo wa umoja, ushirika na mshikamano ndani ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama, wanavyovihudumia.” Baba Mtakatifu Leo XIV amewapongeza viongoi hawa wa Kanisa kwa ukaribu ambao kama wachungaji wema wanauonesha kwa wale wanaotekeleza huduma muhimu, ya kipekee, na yenye changamoto kubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu Mungu nchini Ureno na kwingineko. Ushuhuda wao wa upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kwa nchi yao ni kama dawa ya faraja inayoleta matumaini. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewapatia baraka zake za Kitume, akitambua mchango wao mkubwa katika Jimbo la Kijeshi. Bikira Maria wa Fátima awasindikize katika utekelezaji wa utume wao, sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, Furaha ya Kristo Yesu Mfufuka iwe ni nguvu yao.  

Jimbo la Kijeshi Ureno
24 Agosti 2026, 15:51