Tafuta

Papa Leo XIV anasema: Wakristo wanaitwa kutoa ushuhuda wa pamoja kuhusu uhuru wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Papa Leo XIV anasema: Wakristo wanaitwa kutoa ushuhuda wa pamoja kuhusu uhuru wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.  (Agenzia Nev, uff stampa)

Papa Leo XIV Kwa Wajumbe wa Sinodi ya Waldensiani na Wamethodisti: Ushuhuda

Teknolojia ya akili unde ni kiini cha Maadhimisho ya Sinodi hii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ili kuweza kukabili kikamilifu Mapinduzi ya Kidijitali yanayoonekana kutaka kuvuka mipaka ya ubinadamu, kuna haja ya kuzingatia kwamba, Wakristo wanaitwa kutoa ushuhuda wa pamoja kuhusu uhuru wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; anakazia umuhimu wa kuruhusu teknolojia kustawi bila kusababisha moyo wa binadamu kurejea nyuma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa la Waldensiani lilianzishwa na Peter Waldo (Valdes), Mfanya biashara tajiri kwenye Karne ya 12 yaani kati ya Mwaka 1170–1173 BK huko Lyon, nchini Ufaransa.  Mfanyabiashara huyu aliacha mali zake zote na kuanza kuishi maisha ya ufukara akitangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni Kanisa lililoanza kama vuguvugu la uamsho na ufuasi wa maisha ya Mitume wa Kristo Yesu badala ya Kanisa la mwanzo. Walihimiza usomaji wa Biblia Takatifu kwa lugha ya kawaida na kukataa baadhi ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki wakati huo na wakatengwa na Kanisa kama wazushi na Papa Lucius III mnamo mwaka 1184 kwa njia ya Tamko linalojulikana kama “Ad Abolendam.” Kwa upande mwingine, Kanisa la Wamethodisti lilianzishwa kunako karne ya 18 na hasa Mwaka 1729 likiwa kama klabu ya masomo huko Oxford na kupata mwamko rasmi mwaka 1738 chini ya uongozi wa John Wesley. Muungano wa Kanisa la Waldensiani na Kanisa la Wamethodisti nchini Italia (Union of Methodist and The Waldensian Evangelical Church” ulianzishwa kunako mwaka 1975 kupitia Mkataba wa Ushirikiano; “Patto di Integrazione” na unaendesha shughuli nyingi za maisha ya kiroho, kijamii, kielimu na kitamaduni.

Waamini wa Muungano wa Makanisa ya Waldensiani na Wamethodisti
Waamini wa Muungano wa Makanisa ya Waldensiani na Wamethodisti   (ANSA)

Muungano wa Kanisa la Waldensiani na Kanisa la Wamethodisti nchini Italia, kuanzia Jumamamosi tarehe 22 hadi Jumatano tarehe 26 Agosti 2026 unaadhimisha Sinodi huko Torre Pellice, mkoani Torino, Kaskazini mwa Italia. Hii ni Sinodi inayojadili pamoja na mambo mengine kuhusu: Amani na haki jamii; Majadiliano ya kiekumene; Haki msingi za binadamu; Ulinzi na utunzaji wa watu dhaifu ndani ya jamii; maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; changamoto na majibu ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo katika Ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuguswa na umuhimu wa Maadhimisho ya Sinodi Muungano wa Kanisa la Waldensiani na Kanisa la Wamethodisti nchini Italia, katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa wajumbe wa Sinodi kupitia kwa Askofu Derio Olivero wa Jimbo Katoliki Pinerolo, Kaskazini mwa Italia anawatakia kheri na baraka katika maadhimisho ya Sinodi hii.

Sinodi ya Shirikisho la Makanisa ya Kiprotestanti
Sinodi ya Shirikisho la Makanisa ya Kiprotestanti   (Chiesa Evangelica Valdese - Unione delle chiese metodiste e valdesi)

Teknolojia ya akili unde ni kiini cha Maadhimisho ya Sinodi hii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ili kuweza kukabili kikamilifu Mapinduzi ya Kidijitali yanayoonekana kutaka kuvuka mipaka ya ubinadamu, kuna haja ya kuzingatia kwamba, Wakristo wanaitwa kutoa ushuhuda wa pamoja kuhusu uhuru wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV akirejea katika Waraka wake wa kwanza wa Kitume: “Magnifica humanitas” yaani: “Utu wa kupendeza" Juu ya Hifadhi ya Mwanadamu Katika Enzi ya Teknolojia ya Akili Unde” anakazia umuhimu wa kuruhusu teknolojia kustawi bila kusababisha moyo wa binadamu kurejea nyuma. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa na matamanio haya moyoni mwake, anawaombea wajumbe karama za Roho Mtakatifu na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu ziwashukie na kukaa na wajumbe wa Sinodi hii.

Sinodi
25 Agosti 2026, 15:01