Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge Wakatoliki: Umuhimu wa Familia
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge Wakatoliki “International Catholic Legislators Network, ICLN” ulianzishwa kunako mwaka 2010, huko Trumau Austria na Kardinali Christoph Schönborn, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria na Bwana David Alton, Mbunge kutoka Bunge la Uingereza. Mkutano wa 17 wa Mwaka wa Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge Wakatoliki “International Catholic Legislators Network, ICLN” ulifanyika kuanzia tarehe 20 na unahitimishwa tarehe 23 Agosti 2026, jijini Roma, Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Utu wa Binadamu na Akili Unde: Changamoto, Fursa na Udhibiti.” Hii ni tema nyeti na yenye changamoto zake katika Ulimwengu mamboleo, kutokana na kuiwezesha jamii kuwa na mtazamo mpana zaidi, lakini ukiacha maswali mazito ya kimaadili na utu wema yakiendelea kuitafakarisha familia ya binadamu inayopaswa kufanya maamuzi machungu. Wajumbe wa Mtandao huu, Ijumaa tarehe 21 Agosti 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV, mjini Vatican. Mkutano huu wa siku nne, unawakutanisha: Wabunge wa Kimataifa, Maafisa wa Serikali, na Wataalamu kwa ajili ya uimarishaji wa imani, elimu fungamani na endelevu, na majadiliano yanayolenga kuwazamisha zaidi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na kuchambua changamoto za kisiasa kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kardinali Christoph Schönborn, Kardinali Béchara Boutros Raï na Kardinali Charles Maung Bo ndio walioteuliwa kuwa ni wadhamini wa Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge Wakatoliki “International Catholic Legislators Network, ICLN.”
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hivyo, zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.
Kwa ufupi kabisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakita mizizi yake katika: Utu wa binadamu, ustawi, maenndeleo na mafao ya wengi; hatima ya mali ya dunia, kanuni auni na mshikamano anasema Baba Mtakatifu Leo XIV. Kimsingi maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanapaswa kumsaidia mwanadamu kujenga na kudumisha utu wema na udugu wa kibinadamu, kwa kuwajibikiana, tayari kujenga utamaduni wa upendo na kwamba, teknolojia inakuwa ni chombo cha maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Kama wabunge, hii changamoto ni kiini cha wito wao, kwani wanawajibika kutunga sheria na sera zitakazosaidia kudhibiti matumizi ya teknolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala teknolojia haipaswi kuwa ni kikwazo cha maendeleo, bali chombo kinachomwongoza mwanadamu kwa hekima na busara. Kumbe, wabunge katika shughuli zao wanapaswa kuwatia moyo wanasayansi ili waendelee kuwajibika na kuwa wagunduzi, huku wakikazia haki msingi za binadamu na uhuru wake. Sera hizi ziwalinde walaji, ili wasinyonywe; zilinde uhuru wa mtu binafsi sanjari na kuhakikisha kwamba, ukweli na uwazi vinalindwa na kudumishwa na kwamba, sera hizi zinaendelea kuziimarisha taasisi za kidemokrasia. Ili kufikia lengo hili, "kunahitajika mifumo imara ya kisheria, usimamizi huru, watumiaji wenye uelewa, na mfumo wa kisiasa usioacha kutekeleza wajibu wake" (Magnifica humanitas, nambari 106). Usimamizi wa namna hiyo unaweza kufanyika katika ngazi mbalimbali za ndani, Kitaifa na Kimataifa kwa kunogesha majadiliano ya wazi kuhusu "mifumo ya kimaadili inayohusika na kuiweka chini ya viwango vya pamoja vya haki ya kijamii" (nambari 107), ili hatimaye, kuhakikisha kwamba hakuna itikadi au maslahi yoyote mahususi yanayoamua maadili yaliyojengwa ndani ya mifumo ya teknolojia ya Akili Unde.
Wakati huo huo, maendeleo ya haraka ya teknolojia ya Akili Unde yana hatari ya kuleta aina mpya za utegemezi wa kiteknolojia, huku Mataifa maskini yakizidi kutegemea Mataifa tajiri zaidi ulimwenguni. Baba Mtakatifu Leo XIV anaonya kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa waangalifu, ili uvumbuzi wa teknolojia ya Akili Unde usije ukawa ni njia nyingine ya kuwatambukiza watu katika ukoloni wa kiitikadi au kiuchumi. Rej. nambari 178-179). Kwa masikitiko makubwa anasema Baba Mtakatifu Leo XIV binadamu katika Ulimwengu mamboleo anakabiliana na aina fiche ya utawala ambapo algoriti huamua nani anaonekana na nani anabaki asiyeonekana, ambapo majukwaa ya kidijitali huunda mijadala ya umma bila uwajibikaji, na ambapo utu wa wafanyakazi huwekwa chini ya ufanisi wa mifumo (Rej. nambari 95, 150, 171). Maendeleo kama haya yanafunua sura mpya ya jaribu la zamani la kutaka kutawala na kumiliki bila kutoa huduma. Kinyume na utamaduni huu wa uchu wa madaraka, Mtakatifu Paulo VI alipendekeza kwa Kanisa kujikita katika ujenzi wa "ustaarabu wa upendo.” Rej. Pope Paulo VI, Regina Caeli, 17 Mei 1970; Rej. Magnifica humanitas, n. 186. Huu ni ustaarabu utakaosimamia teknolojia ya Akili Unde kwa hekima na busara na hivyo kulea mioyo yenye uwezo wa upendo wa dhati, huruma na uwajibikaji. Katika jamii ya namna hiyo, shule ya kwanza ya ubinadamu ingekuwa familia. Kwani ndani ya familia ndipo mtu anapojifunza kwanza kuaminiana kabla ya kufanya hesabu za faida na hasara; Ukarimu kabla ya ushindani; Majadiliano kabla ya kinzani na migawanyiko; na upendo kabla ya uchu wa madaraka. Teknolojia ya Akili Unde haipaswi kamwe kuruhusiwa kudhoofisha familia ambayo ni msingi wa jamii iwe kwa kupunguza thamani ya watu na uhusiano na kuwa takwimu na maagizo tu; kwa kujaza akili za vijana maudhui yanayopotosha matamanio yao halali, au kwa mifumo ya kiuchumi inayofanya maisha ya familia kuwa hatarini kiuchumi.
Kwa sababu hiyo, Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kuwahimiza Wajumbe wa Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge Wakatoliki kuimarisha sera sanjari na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, zinazowasaidia wazazi na walezi kutekeleza barabara jukumu lao la kulea na kuelimisha; na zinazowawezesha vijana kuwa na matumaini kwa siku za usoni. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV Ulimwengu hauhitaji teknolojia ya Akili Unde inayodhoofisha ubinadamu; badala yake, unahitaji akili ya kibinadamu iliyoangaziwa na hekima na busara; Mamlaka ya kisiasa inayoongozwa na dhamiri hai sanjari, na uvumbuzi wa kiteknolojia unaoongozwa na upendo wa dhati. Hapo ndipo teknolojia ya Akili Unde itakapokuwa si mpinzani wa ubinadamu bali mhudumu wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, majadiliano yao katika mkutano wao yatazaa matunda tele kwa Mataifa yao na kwa familia nzima ya mwanadamu. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka Wajumbe wa Mtandao wa Kimataifa wa Wabunge Wakatoliki chini ya ulizni na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Shauri Jema, ili aweze kufuatana na kuambatana nao daima, mwishoni amewatakia heri na baraka tele kwa ajili yao, familia zao na watu wote wanaowahudumia.
