Papa Leo XIV: Shirikisho la Marsodeto la Toledo: Miaka 54 ya Huduma Kwa Maskini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shirikisho la Marsodeto la Toledo, kutoka Hispania “Federazione Marsodeto, Toledo-Spagna” lilianzishwa kunako mwaka 1980 na Padre Marcelino Casas Puente likiwa na lengo la kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kupooza kwa ubongo pamoja na familia zao. Kwa sasa Shirikisho hili linahudumia familia zaidi 2, 700 na katika muktadha wa maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 45 tangu kuanzishwa kwao, Jumatatu tarehe 24 Agosti 2026 wamefanya hija ya maisha ya kiroho kwa kukutana na hatimaye, kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican, ambaye alionesha furaha kubwa kwa kukutana nao, ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka alizowajalia katika kipindi cha Miaka 45 cha maisha na utume wao na kwamba, anamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aendelee kuibariki kazi na utume huu unaosimikwa katika jitihada kubwa zisizoonekana kwa macho ya wengi, ambazo zinapata thawabu yake kutoka kwa Mwenyezi Mungu pekee.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “lakini hii ni kazi yenye kuridhisha sana unapomwona Kristo Yesu mwenyewe katika sura ya kila mtu. Kwa njia ya sadaka na majitoleo yao, wanatoa ushuhuda wa pekee kuhusu Injili: “Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” Mt 25:40. Huu ni mwaliko wa kutambua mtazamo wa Kristo Yesu unaowaalika kuzama katika maisha ya watu dhaifu, watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, inawasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukua kama jamii ya Kibinadamu na Kikristo. Ushuhuda unaonesha jinsi ambavyo Shirikisho hili linavyowashughulikia watu wenye ulemavu wa akili na ulemavu wa kupooza kwa ubongo (cerebral palsy). Kwa hakika huu ni mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika utetezi wa utu wa binadamu, na ushirikishwaji kamili.
Ni katika muktadha huu wa huduma, Shirikisho hili limepata nafasi ya kuungwa mkono na ujumbe wa Taasisi ya Serikali, ulioambatana pamoja nao, kama ushuhuda wa sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV anapoiangalia historia yao, huko walikotoka, anasema, wanapaswa kweli kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo na huduma ya Padre Marcelino Casas Puente, ambaye takribani miaka arobaini na tano iliyopita alianzisha Shirikisho hili ambalo wakati ule lilikuwa kama “ndoto ya mchana” lakini kwa sasa ni uhalisia unaotangazwa na kushuhudia kwamba, hakuna familia hata moja yenye mwanafamilia mwenye ulemavu wa akili inayopaswa kuachwa ijitegemee yenyewe.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “Leo hii, Shirikisho hili linaweza kujivunia kuwafikia watu wengi na kutimiza uhalisia wa yale niliyopata fursa ya kuyakumbusha wakati wa hija yangu yangu ya kitume hivi karibuni nchini Hispania yaani “Maana, upendo wa Kristo watubidisha.” 2Kor 5:14. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka wanachama wa Shirikisho la Marsodeto la Toledo, kutoka nchini Hispania, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aendelee kuandamana pamoja nao katika maisha na utume wao. Bikira Maria awatie moyo katika nyakati za shida na changamoto kubwa, na kuwaongoza kuelekeza macho yao daima kwa Kristo Yesu, ili Shirikisho hili liendelee kuwa ni kielelezo na ushuhuda wa kweli katika Kanisa na medani mbalimbali za kijamii. Hatimaye, Baba Mtakatifu akawapatia wajumbe wote baraka zake za kitume!
