Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 17 Novemba 2026 anatarajiwa kufanya Hija ya Kitume nchini Uruguay, Argentina na Peru. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 17 Novemba 2026 anatarajiwa kufanya Hija ya Kitume nchini Uruguay, Argentina na Peru.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Kufanya Hija ya Kitume Amerika ya Kusini Kuanzia tarehe 6Hadi 17 Novemba 2026

Papa Leo XIV amekubali kwa taadhima kubwa wito na mwaliko wa wakuu wa nchi na Maaskofu kutoka Uruguay, Argentina na Perù kuzitembelea nchi zao. Kumbe, Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 17 Novemba 2026 anatarajiwa kufanya Hija ya Kitume nchini Uruguay, Argentina na Peru kwa kutembelea miji mikuu kumi. Hii ni Hija ya kihistoria kwani itamsaidia kuzitembelea nchi ambazo zina mwamko kidogo wa kidini, huko Amerika ya Kusini, hadi Argentina.

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume na Kichungaji zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ndani na nje ya Italia zinalenga pamoja na mambo mengine kuwaimarisha waamini katika fadhila ya imani, matumaini, mapendo na mshikamano, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu chimbuko la maisha na uzima wa milele. Kwa Baba Mtakatifu ziara hizi zinakuwa ni fursa ya kukutana mubashara na watu wa Mungu katika maeneo yao, ili kuhamasisha na kuragibisha mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu; ustawi, maendeleo sanjari na haki msingi za binadamu. Hii pia ni nafsi ya kuangalia changamoto na fursa zinazopatikana katika maeneo husika tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbata maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV amekubali kwa heshima na taadhima kubwa wito na mwaliko wa wakuu wa nchi na Maaskofu kutoka Uruguay, Argentina na Perù kuzitembelea nchi zao.

Papa Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba anatembelea Uruguay.
Papa Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 8 Novemba anatembelea Uruguay.

Kumbe, Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 17 Novemba 2026 anatarajiwa kufanya Hija ya Kitume nchini Uruguay, Argentina na Peru kwa kutembelea miji mikuu kumi. Hii ni Hija ya kihistoria kwani itamsaidia kuzitembelea nchi ambazo zina mwamko kidogo wa kidini, huko Amerika ya Kusini, hadi Argentina, nchi aliko zaliwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa bahati mbaya, hakuweza kuitembelea hata mara moja wakati wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV atarejea nchini Peru, mahali alikowahi kufanya utume wake kama mmisionari wa Shirika la Mtakatifu Augustino, OSA na baadaye akateuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Chiclayo. Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kutembelea nchi za Amerika ya Kusini tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki Ulimwenguni tarehe 8 Mei 2025 na hivyo kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kuanzia kwa Mtakatifu Petro, Mtume.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kutoka Uruguay.
Baraza la Maaskofu Katoliki Kutoka Uruguay.

Askofu Milton Tróccoli, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uruguay, amesema Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uruguay kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 8 Novemba 2026 itasaidia sana kupyaisha na kuimarisha imani ya watu wa Mungu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kwamba, hii itakuwa ni zawadi kubwa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, hija hii ya kitume, itawasaidia watu wa Mungu nchini Uruguay kuzamisha mizizi ya tamaduni zao katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya amana na urithi wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, leo hii imani haina budi kutangazwa, kushuhudiwa na kutamadunishwa kwani huu ni mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na uzoefu wa watu mahalia. Hija hii inatarajiwa kujenga na kuimarisha umoja na ushirika miongoni mwa watu wa Mungu nchini Uruguay. Hii ni fursa ya kuwaimarisha waamini katika imani, matumaini na mapendo, tayari kukita maisha yao katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anakuwa ni Papa wa pili kufanya Hija ya Kitume nchini Uruguay.

Papa Leo XIV anatembelea Argentina kuanzia tarehe 8hadi 11 Novemba 2026
Papa Leo XIV anatembelea Argentina kuanzia tarehe 8hadi 11 Novemba 2026   (@VATICAN MEDIA)

Askofu mkuu Marcelo Daniel Colombo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina anasema, watu wa Mungu nchini Argentina wanayo shauku kubwa ya kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Argentina kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Shuhuda wa Kristo Yesu na Mjumbe wa amani anayekwenda nchini mwao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, chemchemi ya furaha ya Injili kuanzia tarehe 8 hadi 11 Novemba 2026. Hija hii inahitaji maandalizi maalum kwa kujikita katika shughuli za kichungaji kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha na utume wa Kanisa nchini Argentina. Baba Mtakatifu Leo XIV ni mjumbe wa haki na amani, mambo msingi katika kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka kwa Kanisa nchini Argentina kujikita kikamilifu katika mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wake kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa Kanisa na Kimisionari na Kisinodi. Watu wa Mungu nchini Argentina, watakuwa na furaha ya pekee kwa kuungana na Baba Mtakatifu Leo XIV kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Lujàn, mahali ambapo Hayati Baba Mtakatifu Francisko alipendelea sana kwenda kusali. Itakumbukwa kwamba, mwaka 1987 Mtakatifu Yohane Paulo II alifanya Hija ya Kitume nchini Argentina.

Watu wa Mungu kutoka Peru wanamsubiri kwa hamu Papa Leo XIV.
Watu wa Mungu kutoka Peru wanamsubiri kwa hamu Papa Leo XIV.

Askofu Carlos Enrique García Camader wa Jimbo Katoliki Lurín nchini Peru ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Peru anasema, watu wa Mungu nchini Peru wamepokea kwa furaha na bashasha kubwa taarifa ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Peru kuanzia tarehe 11 hadi 17 Novemba 2026. Hija hii ya kitume ni muda muafaka kwa watu wa Mungu nchini Peru kujikita katika ujenzi wa haki, amani, upatanisho, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wote wa Mungu nchini Peru.

Hija ya Kitume Amerika ya Kusini
20 Agosti 2026, 11:37