Papa Leo XIV: Anauliza Swali la Msingi Kristo Yesu Ni Nani Kwako?
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 21 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, Mwinjili Mathayo katika Sura ya 16: 13-20 anamweka Mtume Petro mbele ya macho ya Mitume wa Yesu na kushuhudia kwamba kwa hakika Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai. Naye Yesu akajibu na kumwambia “Heri wewe Simon Bar-yona, kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia: Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni. Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo”. Rej. Mt. 16:13-20. Mwinjili Mathayo katika sehemu hii ya Injili anauliza swali kwa kila mwamini, kujiangalia ndani mwake mwenyewe katika safari yake ya imani, ili kujibu kwa hakika Kristo Yesu ni nani katika maisha yake! Simulizi la Injili linaonesha jinsi swali hili lilivyo la msingi kwa maisha ya ufuasi wa Kristo Yesu. Kwa hakika, ingawa Mitume wa Yesu kumi na wawili walikuwa tayari wameshiriki sehemu kubwa ya maisha na utume wa Kristo Yesu, lakini Yesu mwenyewe hakuchukulia kawaida na kwa wepesi kwamba walimfahamu kwa undani na hivyo kulielewa Fumbo la Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: kweli na uzima; ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Hivyo, Kristo Yesu baada ya kuuliza watu walimwonaje na walisemaje kuhusu Yeye, aliwageukia wao moja kwa moja na kuwaulizwa: "Nanyi mwasema mimi ni nani?" Mt 16:15.
Hii ni sehemu ya tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 21 ya Mwaka A wa Kanisa kama ilivyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 23 Agosti 2026 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huu ni wakati muhimu sana kwa wafuasi wa kila kizazi na kila mwamini binafsi, kujitaabisha kila siku kugundua Ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu na Injili yake, kuzidisha uelewa wao wa ujumbe wake na kuendelea kupyaisha maamuzi ya maisha yao ili kweli yaweze kuendana na imani wanayokiri, kuitangaza na kuishuhudia, tayari kushinda kishawishi cha kudhani kwamba, wanafahamu kila kitu na kuiishi imani yao kwa mazoe, kwani mwamini hawezi kupata imani siku moja na hiyo ikatosha. Waamini kila kukicha wanaulizwa swali la msingi! Kristo Yesu ni nani kwao na uwepo wake katika maisha yao una maana gani? Haya ni maswali muhimu sana yanayojitokeza wakati wa Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, lakini pia yanayotokeza pale mwamini anapokutana na majeraha na mahitaji ya jirani zake, au ndani ya uhusiano sanjari na hali zinazogusa na kutikisa dhamiri zao kwa kina.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa ufupi sana kwamba, katika mwenendo wa maisha ya waamini, wanaweza kutambua ikiwa kama Kristo Yesu ni mtu maarufu tu wa kihistoria, aliyesema na kutenda mambo muhimu au kwake Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, aliyetumwa na Baba wa milele kuwaingiza watu katika upendo wake na hivyo kubadilisha maisha yao na katika Ulimwengu wanamoishi. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kujifunza kutojifungia ndani ya imani na uhakika wao wa masuala ya kidini pekee, bali wawe tayari kujenga na kudumisha uhusiano binafsi na Kristo Yesu. Kamwe waamini wasiridhike na maneno ya kusikia au kuambiwa tu au yale ambayo wamerithishwa hata kama yalikuwa na nia njema. Kristo Yesu anawaita waamini kuchukua hatua binafsi, kujibidiisha kumfahamu kwa undani zaidi na hivyo kujenga na kuruhusu urafiki wao na Kristo Yesu, uweze kuwaletea mabadiliko ya kina. Tukio la kukutana na Kristo Yesu katika maisha, iwe ni fursa ya kila mara ya kujipyaisha katika imani, ili hatimaye kuweza kudiriki kutembea katika njia zisizojulikana na hivyo kuwa tayari kufanya maamuzi tofauti kabisa na yale waliyokuwa wanayatarajia. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, hii ni safari ya mtu binafsi, njia ya Kanisa na Maamuzi yake ya shughuli za kichungaji. Haya ni maneno ambayo vinginevyo waamini wangeweza kufikiri inatosha tu kuendelea kama walivyozoea kufanya kila siku. Badala yake, ni muhimu sana kwa waamini kujiuliza mara kwa mara Kristo Yesu ni nani kwao? Ni hatua gani wanayopaswa kuchukua na ni maamuzi gani wanayopaswa kufanya? Baba Mtakatifu Leo XIV anahitimisha tafakari yake kwa kutoa mwaliko kwa waamini, kumwita Bikira Maria ambaye katika maisha na utume wake, alijitahidi daima kutafuta na kuyatimiza mapenzi ya Mungu moyoni mwake, ili kwa njia ya Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu awaongoze daima katika hija ya imani.
