Tafuta

Papa Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ebola sanjari na wale wote walioathirika nchini DRC. Papa Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ebola sanjari na wale wote walioathirika nchini DRC. 

Papa Leo XIV Aguswa na Wagonjwa Ebola DRC & Vifo vya Watu 107 Zamboye Afrika ya Kati

Papa Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 23 Agosti 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliyaelekeza mawazo na sala zake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, akiwakumbuka na kuwaombea watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ebola sanjari na wale wote walioathirika na kwamba, kwa sasa hali inazidi kuwa tete kwa kusababisha idadi ya vifo na maambukizi kuongezeka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hali inazidi kuwa tete zaidi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC huku idadi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola ikifikia 5,515 na vifo 2,642. Na wagonjwa wapya 51 wako katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, kulingana na taarifa zilizotolewa na Serikali ya DRC mapema, Jumatatu tarehe 24 Agosti 2026. Serikali inasema kwamba, kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa wa Ebola kinazidi kuongezeka kwa kasi kubwa kutoka asilimia 20% mwezi Juni hadi kufikia asilimia 48%, mwezi Agosti ambapo yamkini mtu mmoja kati ya wawili wanaoambukizwa hufariki dunia.  Ijumaa tarehe 21 Agosti 2026 DRC ilipokea dozi 16,000 za chanjo ya Everbo za kuzuia maambukizi ya Ebola kutoka kwa Shirika la Afya Duniani, WHO, ikiwa sehemu ya dozi 70,000 zinazotarajiwa kuwasilishwa kufikia mapema mwezi Septemba 2026.

Hali ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC inazidi kuwa ni tete sana.
Hali ya ugonjwa wa Ebola nchini DRC inazidi kuwa ni tete sana.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 23 Agosti 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameyaelekeza mawazo na sala zake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, akiwakumbuka na kuwaombea watu waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ebola sanjari na wale wote walioathirika na kwamba, kwa sasa hali inazidi kuwa tete kwa kusababisha idadi ya vifo na maambukizi kuongezeka. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii, kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia DRC kuzuia maambukizi mapya, sanjari na kuwashirikisha watu mahalia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu wa hatari, ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaoendelea kufariki dunia.

Watoto wakipatiwa chanjo ya ugonjwa wa Ebola
Watoto wakipatiwa chanjo ya ugonjwa wa Ebola

Wakati huo huo, habari zinasema kwamba, zaidi ya watu 107 wamefariki dunia baada ya mgodi mdogo wa dhahabu kuporomoka katika kijiji cha Zamboye, Magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, tarehe 18 Agosti 2026. Maporomoko ya ardhi yamesababishwa na mazingira magumu na hatarishi ya wachimbaji wadogowadogo na ukosefu wa viwango vya usalama. Waokoaji walifanikiwa kutoa zaidi ya miili 107 na kwamba idadi kamili ya watu waliokuwa mgodini wakati wa tukio hilo bado haijajulikana. Ajali za migodi midogo zimekuwa zikijitokeza katika maeneo mbalimbali Barani Afrika kutokana na ukosefu wa viwango vya kutosha vya usalama, huku ukosefu wa ajira ukiwasukuma watu wengi kujihusisha na uchimbaji huo wa madini.

Watu 107 wamefariki dunia huko Zamboye, Jamhuri ya Afrika ya Kati
Watu 107 wamefariki dunia huko Zamboye, Jamhuri ya Afrika ya Kati   (ANSA)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 23 Agosti 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliwakumbuka na kuwaombea, wachimba madini wadogo wadogo waliopoteza maisha yao kutokana na kuporomoka kwa mgodi mdogo wa dhahabu. Baba Mtakatifu Leo XIV anamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwapokea na kuwajalia maisha na uzima wa milele wote waliopoteza maisha katika maporomoko hayo. Baba Mtakatifu anamwomba, Mwenyezi Mungu kuwasaidia wale wote wanaoendelea kujizatiti zaidi katika kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na usalama machimboni na kwamba, sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji wa madini zinafuatwa kikamilifu.

DRC Ebola
24 Agosti 2026, 14:47