Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kurejea “Ad Fontem” yaani kwa Kristo Yesu, chemchemi ya uzima mpya na furaha ya kweli Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kurejea “Ad Fontem” yaani kwa Kristo Yesu, chemchemi ya uzima mpya na furaha ya kweli  

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Kimataifa Medjugorje 2026

Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kurejea “Ad Fontem” yaani kwa Kristo Yesu, chemchemi ya uzima mpya na furaha ya kweli kwa kujikita katika maisha ya sala, kwa kusikilizaji, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao na kwa ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani haya ni maeneo mahususi ya kuweza kukutana na Kristo Yesu aliye hai, tayari kumtangaza na kumshuhudia!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Katika historia ya wokovu, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amejifunua kwa njia ya Sheria, kielelezo cha utambulisho, dira na mwongozo wa watu wa Mungu. Mwenyezi Mungu amejifunua kwa njia ya Manabii wake watakatifu, waliotumwa kutangaza na kushuhudia uwepo wake angavu na endelevu katika hija ya maisha ya waja wake. Hatimaye, Mwenyezi Mungu katika nyakati hizi amejifunua kwa njia ya Kristo Yesu, Uso wa huruma na upendo wa Baba wa milele. Huyu ndiye Neno aliyekuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huu ni muhtasari wa Injili kama ilivyoandikwa na Yohane, kama tunavyousoma katika Dibaji au Utangulizi wa Injili yake. Yn 1:1-10. Hii ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu inayowaambata na kuwakumbatia watu wa nyakati zote. Ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Huyu ndiye Nuru halisi inayomtia nuru kila mtu na wala hakuna mtu awaye yote anayeweza kuikwepa nuru hii. Ndiye Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli.

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Kimataifa
Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Kimataifa

Hivi ndivyo Mama Kanisa anakiri na kuungama katika imani yake. Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima. Mtakatifu Augustino Askofu na Mwalimu wa Kanisa anasema, Kristo Yesu ni ukweli uliofanyika njia inayowapeleka watu mbinguni kwa Baba yake wa milele. Kristo Yesu, Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, alizaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba; ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu! Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba amejaa neema na kweli. Yesu mwenyewe anajitambulisha kwa kusema, “Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi” Yn. 14:6. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amekuwa njia, ukweli na uzima.

Papa anawaalika vijana kurejea tena kwenye chemchemi ya imani.
Papa anawaalika vijana kurejea tena kwenye chemchemi ya imani.   (@Vatican Media)

Hii ni KIRI ya Imani inayoshuhudia kwamba, Kristo Yesu ni njia ya wokovu wa binadamu wote: “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu waliopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo” Mdo. 4:12. Huu ni utambuzi na utume wa Wakristo wote wa kutangazwa na kushuhudiwa si tu kwa maneno, bali kwa vitendo kama kielelezo cha imani tendaji. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje, nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 6 Agosto 2026. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV umesoma mwanzo wa uzinduzi wa Maadhimisho haya na Askofu mkuu Aldo Cavalli, Msimamizi wa Kitume mwenye hadhi ya pekee kwa Parokia ya Medjugorje. Baba Mtakatifu anawaalika vijana wa kizazi kipya kurejea “Ad Fontem” yaani kwa Kristo Yesu, chemchemi ya uzima mpya na furaha ya kweli kwa kujikita katika maisha ya sala, kwa kusikilizaji, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao na kwa ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani haya ni maeneo mahususi ya kuweza kukutana na Kristo Yesu aliye hai.

Neno la Mungu ni chemchemi ya imani
Neno la Mungu ni chemchemi ya imani   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawahimiza vijana wa kizazi kipya kutafuta kwa dhati ukweli unaowaweka huru, bila kuruhusu kushawishiwa na udanganyifu wa furaha za mpito na za muda mfupi. Hakika, kwa kumfuata Yesu, kila mtu anaweza kuyapokea hata maswali magumu zaidi na misukumo ya moyo isiyotulia kama fursa za kutafakari na kukua katika imani. Aidha, Baba Mtakatifu anawasihi vijana kujiruhusu kuongozwa na Roho Mtakatifu na kujikabidhi kwa maombezi ya Bikira Maria Mama wa Mungu na wa Kanisa, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili wanaong'aa, wachochezi wa udugu wa kibinadamu, na wajenzi wa amani katika jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV amewahakikishia uwepo wake katika maadhimisho haya kwa njia ya sala na kwamba, anawaombea baraka na neema tele kutoka kwa Mungu ili ziweze kuwashukia na kukaa nao daima.

Vijana Medjugorje

 

02 Agosti 2026, 15:07