Hija ya Kichungaji ya Papa Leo XIV Nchini San Marino na Rimini
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Hija za Kitume na Kichungaji zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ndani na nje ya Italia zinalenga pamoja na mambo mengine kuwaimarisha waamini katika fadhila ya imani, matumaini, mapendo na mshikamano, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu chimbuko la maisha na uzima wa milele. Kwa Baba Mtakatifu ziara hizi zinakuwa ni fursa ya kukutana mubashara na watu wa Mungu katika maeneo yao, ili kuhamasisha na kuragibisha mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu; ustawi, maendeleo sanjari na haki msingi za binadamu. Hii pia ni nafsi ya kuangalia changamoto na fursa zinazopatikana katika maeneo husika tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaofumbata maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 22 Agosti 2026 anafanya hija ya kichungaji Jamhuri ya San Marino na kuhudhuria Kongamano la Urafiki kati ya Watu: “Meeting per l'amicizia fra i popoli” na hatimaye, majira ya jioni, anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Bandari ya Rimini. Jamhuri ya San Marino ni nchi iliyoanzishwa na Mtakatifu Marino tarehe 3 Septemba 301 BK. Hii ni nchi ndogo iliyo milimani karibu na Pwani ya Italia. Ni moja ya nchi tajiri kwa kigezo cha pato ghafi la mwaka na ina idadi ndogo ya watu ambao kadiri ya takwimu za Mwaka 2026 wanakadiriwa kufika 34, 300.
Kongamano la Urafiki Kati ya Watu “Meeting per l'amicizia fra i popoli” ni tamasha kubwa la kimataifa la utamaduni, imani, na majadiliano linalofanyika kila mwaka mjini Rimini, nchini Italia, lilianzishwa na Muasisi wa harakati za “Comunione e Liberazione” Don Luigi Giussani aliyezaliwa tarehe 15 Oktoba 1922 huko Desio, Italia na kufariki dunia tarehe 22 Februari 2005 huko Milano, Italia. Mtumishi wa Mungu Padre Luigi Giussani ni kiongozi aliyebahatika kuwa na karama, maono na tafakari ya kina kuhusu Ukristo na mchango wake katika ustawi, mafao na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili. Alikazia kwamba, Ukristo si dini inayojikita tu katika muundo wa mafundisho sadikifu, kanuni maadili na utu wema, bali ni sehemu ya mchakato wa kutaka kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha ya mwanadamu, ili kumtolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama alivyofanya Mtumishi wa Mungu Luigi Giussani.Ukristo unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuwaonjesha ile furaha, upendo, huruma na imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ushuhuda wenye mvuto unashinda yote, kwani hapa mwamini anaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kumwangalia Kristo Yesu Mkombozi wa dunia, ili kuweza kuwashirikisha na kuwamegea wengine ile furaha ya Injili. Ni changamoto inayowasukuma, waamini kutoka katika ubinafsi wao, ili kuwaendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, tayari kuwashirikisha: amana na utajiri ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa. Huruma ya Mungu inapaswa kuwa ni chachu ya mageuzi, toba, wongofu wa ndani na utakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; sanjari na kuenzi uhusiano kati ya watu binafsi na jamii ya watu katika ujumla wake.
Dante Alighieri ni "Baba wa Lugha ya Kiitalia" aliyefanya uamuzi mkali wa kuandika kazi yake ya “Comedy Divine” “La Divina Commedia”, katika lugha ya kienyeji ya Florentine badala ya Kilatini. Alitaka safari yake kupitia Kuzimu, Toharani, na Paradiso ipatikane kwa kila mtu. Umaarufu mkubwa wa kazi hii ulieneza lahaja ya Florentine kote nchini Italia. "Upendo unaolisogeza jua na nyota nyingine" Ni mstari wa mwisho wa kazi ya Dante Alighieri iitwayo “Divine Comedy” ndiyo kauli mbiu inayonogesha Kongamano la 47 la Urafiki kati ya Watu: “Meeting for Friendship Among Peoples,” ambalo limeanza kutimua vumbi huko Rimini kuanzia Ijumaa tarehe 21 na linatarajiwa kuhitimishwa tarehe 26 Agosti 2026. Baba Mtakatifu Leo XIV, anatembelea maonesho, kukutana na kuzungumza na vijana wanaohudhuria Kongamano hili na baadaye atakutana na kuzungumza na washiriki wote wa Kongamano. Akiwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Rimini, atakutana na kusalimiana na wagonjwa, walemavu na maskini wanaohudumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Rimini, Caritas Rimini. Baadaye, Baba Mtakatifu Leo XIV ataelekea Uwanja wa “Porto”, Uwanja wa Bandari ya Rimini ili kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baadaye atarejea mjini Vatican baada ya maadhimisho haya.
Wakati huo huo, Rais Sergio Mattarella wa Italia katika ujumbe aliomtumia Bwana Bernhard Scholz, Rais wa Mfuko wa Urafiki Kati ya Watu “Meeting per l'amicizia fra i popoli” aliyechaguliwa kunako mwaka 2020 na hivyo kuchukua nafasi ya Bwana Emili Guarnieri aliyeongoza Mfuko huu tangu Mwaka 1993 hadi mwaka 2020. Kongamano la 47 la Urafiki kati ya Watu, lina historia ya pekee katika nyakati za mabadiliko makubwa, unalenga kuendelea kuchangia katika kuunda historia kwa kuunganisha kwa uthabiti mkubwa simulizi zake kwa kukazia fadhila ya upendo unaoelezea zaidi si tu hisia zinazotokana na tajiriba na uzoefu wa mtu binafsi. Huu ni upendo unaofungua milango kwa wengine kwa kuvuka mipaka ya nafsi na wakati huu wa sasa. Hii ni nguvu ya ndani inayopata sura ya thamani katika uhusiano na hivyo kuwa na chapa ya mwelekeo wa kijamii, inayowaunganisha watu kwa kutoa mwelekeo kwa safari za maisha ya mwanadamu dhidi ya mtazamo potofu unaosababisha watu kutokuchua hatua, kutokuaminiana; na hali ya kukata tamaa, wakati hatima ya jamii ni kuchukua jukumu la dhati katika kuunda mustakabali wake, kwa kujali dhuluma na mateso ya wengine, tayari kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kama anavyosema Baba Mtakatifu Leo XIV katika Waraka wa “Magnifica humanitas.”
Rais Sergio Mattarella wa Italia anakaza kusema, mshikamano, urafiki wa kijamii, na asili ya upendo wa hiari na bila masharti vinaweza kufungua nyanja mpya kwa siasa, uchumi, na maisha ya kiraia. Binadamu anaishi katika zama zinazokabiliwa na vita vya kikatili na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, huku makundi madogo yenye nguvu kubwa yakijilimbikizia mamlaka inayozidi ile ya Mataifa mengi huru. Ni katika muktadha wa ubinadamu ndipo binadamu anapoweza kupata nguvu ya kukataa kufuata mkumbo, kutochukua hatua, chuki, na uhasama dhidi ya wale walio tofauti au wageni, na badala yake ni kujenga na kukuza utamaduni wa amani. Rais Sergio Mattarella wa Italia amehitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia washiriki wote mafanikio mema na endelevu katika kujenga kwa moyo mkuu nyanya za ubinadamu.
