Tafuta

Tarehe 12 Desemba 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV atakutana na kuzungumza na Mapadre wote wa Italia. Tarehe 12 Desemba 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV atakutana na kuzungumza na Mapadre wote wa Italia.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Tarehe 12 Desemba 2026 Anakutana na Mapadre wa Italia

Tarehe 12 Desemba 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV atakutana na kuzungumza na Mapadre wote wa Italia, tukio ambalo litatanguliwa na Mkesha wa Sala, Tafakari, na Ujenzi wa udugu wa Kikleri Ijumaa tarehe 11 Desemba 2026, tayari kupyaisha dhamana na utume wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ujenzi wa umoja na ushirika na Askofu mahalia na katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Kumbukumbu Endelevu!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.

Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!

Ijumaa tarehe 11 Desemba 2026 Mkesha wa Sala, Tafakari na Udugu
Ijumaa tarehe 11 Desemba 2026 Mkesha wa Sala, Tafakari na Udugu   (@Vatican Media)

Mapadre ni viongozi walioteuliwa miongoni mwa waamini kwa ajili ya waamini kwa mambo yanayomhusu Mungu. Wanayo dhamana ya kutoa sadaka na kuwaondolea watu dhambi zao na kwamba, wanaishi kati ya watu kwa ajili ya watu. Mapadre ni watu wanaozaliwa katika mazingira ya kibinadamu, kumbe wanapaswa kufumbatwa na tasaufi ya watu ili kukuza na kudumisha mahusiano mema. Mapadre ni watu wenye historia wanayopaswa kuikuza na kuidumisha katika mchakato mzima wa malezi na majiundo yao. Historia hii imwilishwe katika wito wa kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu katika huduma ya Kipadre inayopaswa kushuhudiwa katika maisha kwa kutambua kwamba, familia ni kiini cha wito na maisha ya kipadre. Wahamasishaji wa shughuli za miito ndani ya Kanisa wanapaswa kukumbuka umuhimu wa familia kwani hapa wanakutana na Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa majindo makini ya kiutu na chachu ya kiu ya wito na maisha ya Kipadre, tayari kuanza kujisadaka na kuonesha moyo wa ukarimu. Familia inaweza kupata mwelekeo mpana zaidi kwa kujumuisha: Shule, Parokia, Vyama vya kitume na makundi ya marafiki. Hapa ni mahali ambapo Wakleri wanajifunza kuishi kwa pamoja ili kukuza maahusiano ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko anasema Padre mwema kwanza kabisa ni mtu mwema pia anayeifahamu historia ya maisha yake; anatambua: amana, utajiri na mapungufu yake ya kibinadamu, tayari kujirekebisha ili kuwa na maisha bora zaidi, kwa kujikita katika utulivu wa ndani kielelezo makini cha mfuasi wa Kristo. Majiundo makini ni muhimu sana kwa Wakleri ili kujifunza kutumia vyema karama na mapaji yao badala ya kuelemewa na mapungufu yao ya kibinadamu. Padre ni mtu wa amani anayepaswa kusambaza amani hata wakati wa shida na magumu, ili kuwashirikisha wengine mahusiano mema na Mwenyezi Mungu. Haipendezi kumwona Padre anayesikitika, mwenye moyo mgumu na aliyechanganyikiwa kwani hii ni hatari kwa Padre mwenyewe na kwa wale wote wanaomzunguka!

12 Desemba 2026 ni Siku ya Kumbukizi ya Nyaraka: Waseminari na Mapadre
12 Desemba 2026 ni Siku ya Kumbukizi ya Nyaraka: Waseminari na Mapadre   (Vatican Media)

Mapadre wanapaswa kuwa ni mitume wa furaha na watangazaji mahiri wa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, zawadi ya maisha na wito wa Kipadre inahifadhiwa katika chombo cha udongo, kinachopaswa kutunzwa kwa uangalifu mkubwa, ili kuwashirikisha wengine uzuri wa zawadi ya Upadre. Padre ana mizizi na utamaduni wake na ameitwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya watu kwa mambo matakatifu na kwa ajili ya huduma kwa ndugu zake katika Kristo Yesu. Padre ni kielelezo cha Kuhani mkuu, Mhudumu na Mchungaji mwema anayepaswa kuwachunga watu wake kwa moyo mkuu! Mapadre wanatumwa kuwahudumia watu ili waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao kwa njia ya Neno, lakini zaidi kwa ushuhuda wa maisha. Mapadre wamepakwa mafuta kwa ajili ya huduma na wala si kwa ajili ya kujitafuta wao wenyewe! Ni wahudumu wa Familia ya Mungu na Jamii katika ujumla wake na ndiyo maana, wanapaswa kufundwa barabara ili waweze kutekeleza dhamana hii kwa moyo mkuu. Mapadre wafundwe katika maisha ya kiroho, kiutu na kiakili ili kuwajengea ari na moyo wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi tayari kutekeleza dhamana waliyokabidhiwa na Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa. Mapadre wakumbuke kwamba, daima wako kati ya watu kwa ajili ya watu, daima wakijitahidi kuwahudumia kwa moyo wa unyenyekevu, ili kuwaonjesha uzuri unaofumbatwa katika Injili na upendo wa Mungu unaoshuhudiwa kwa njia ya wito na maisha ya Kipadre. Mama Kanisa anatamani sana kuwa na Mapadre wema, watakatifu na wachapa kazi kadiri ya matakwa ya Kristo Yesu mwenyewe!

Tarehe 12 Desemba 2026 ni Siku ya furaha na upyaisho wa utume wa Kikuhani
Tarehe 12 Desemba 2026 ni Siku ya furaha na upyaisho wa utume wa Kikuhani   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha huu: “A fidelity that generates the future of the Holy Father Leo XIV on the sixtieth anniversary of the conciliar Decrees Optatam Totius and Presbyterorum Ordinis.” Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV Kuhusu “Uaminifu Unaoandaa Mustakabali wa Baadaye” kama kumbukumbu ya Mwaka mmoja, tangu Baba Mtakatifu Leo XIV achapishe Waraka wake huo wa Kitume Sanjari na Maadhimisho ya miaka sitini ya Tamko la Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Optatam Totius” Kuhusu Malezi ya Waseminari na “Presbyterorum Ordinis” Tamko Kuhusu Huduma na Maisha ya Kipadre, tarehe 12 Desemba 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV atakutana na kuzungumza na Mapadre wote wa Italia, tukio ambalo litatanguliwa na Mkesha wa Sala, Tafakari, na Ujenzi wa udugu wa Kikleri Ijumaa tarehe 11 Desemba 2026, tayari kupyaisha dhamana na utume wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ujenzi wa umoja na ushirika  na Askofu mahalia na katika huduma makini kwa watu wa Mungu.

Watu wa Mungu wanashukuru kwa huduma na faraja kutoka kwa Mapadre
Watu wa Mungu wanashukuru kwa huduma na faraja kutoka kwa Mapadre   (@Vatican Media)

Hayo yamo kwenye barua iliyoandikwa na Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kwenda kwa Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki nchini Italia. Katika barua hii, Kardinali Zuppi anaukumbuka wema na ukarimu wa Mapadre kwa watu wa Mungu nchini Italia, katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi; katika mchakato wa kuwasindikiza na kuwafariji waamini, lakini hata katika shida na changamoto za maisha yao, mambo ambayo kamwe hayawezi kuwa na neon la mwisho katika maisha na utume wa Mapadre, ndiyo maana kuna haja ya kusali kwa pamoja, kutegemezana, ili hatimaye kupata tena ile furaha ya kuitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kama Mapadre. Mkutano huu na Baba Mtakatifu Leo XIV itakuwa ni fursa ya kuwaimarisha Mapadre katika imani, matumaini na mapendo; kwa kuwatia moyo kusonga mbele katika maisha na utume wao, kwa kuendelea kushikamana katika ushirika, ndiyo maana Mapadre wanapaswa kukita maisha yao katika sala, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza na udugu wa kibinadamu, ili kuenzi mustakabali wa maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni.

Papa na Mapadre wa Italia
31 Julai 2026, 15:46