Tafuta

Papa Leo XIV, Jumatano jioni tarehe 29 Julai 2026 ameshiriki katika mkutano wa sala na udugu wa kibinadamu kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipofariki dunia. Papa Leo XIV, Jumatano jioni tarehe 29 Julai 2026 ameshiriki katika mkutano wa sala na udugu wa kibinadamu kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipofariki dunia.  (ANSA)

Papa Leo XIV Ashiriki Mkutano wa Sala Na Udugu! Miaka 800 Tangu Afariki dunia Mt. Francisko

Papa Leo XIV kwa namna ya pekee ameushukuru Mfuko wa Andrea Bocelli kwa kazi kubwa unaoifanya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wanaokabiliana na changamoto za kielimu na kijamii. Kupitia nguvu ya muziki, wanachangia katika utume wa Mama Kanisa wa kukuza maendeleo kamili ya kila mwanadamu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu. Mwenyezi Mungu apende kubariki jitihada hizi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Borgo Laudato si' kilichoanzishwa huko Castel Gandolfo, Italia, kwa matakwa ya Papa Francisko, kinalenga kukuza na kudumisha: elimu ya ikolojia fungamani ya binadamu, utunzaji bora wa kazi ya uumbaji, na kuoanisha maendeleo, uchumi, na heshima kwa utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu mintarafu kanuni za Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano jioni tarehe 29 Julai 2026 ameshiriki katika mkutano wa sala na udugu wa kibinadamu kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipofariki dunia.

Kwaya ya Vijana wa Mfuko wa Bocell
Kwaya ya Vijana wa Mfuko wa Bocell

Tukio hili la pekee liliandaliwa na Kituo cha Mafunzo ya Juu cha Borgo Laudato si' huko Castel Gandolfo kwa ushirikiano na Mfuko wa Andrea Bocelli, “Andrea Bocelli Foundation.” Amesikiliza wimbo wa amani “Cantico della pace” ulioimbwa na watoto kutoka: Uganda, Nchi Takatifu na Italia sanjari na sauti ya “Maestro” Andrea Bocelli na sauti za ABF. Hawa ni watoto kutoka Uganda, Nchi Takatifu na Italia, walioguswa, wakatikiswa na hatimaye, wakapekenywa na vita, umaskini, mateso na mahangaiko mbalimbali ambao kwa sasa kwa njia ya sanaa ya muziki wanaonesha jinsi sanaa hii inavyoweza kuwa ni lugha ya Kimataifa katika kukuza na kudumisha majadiliano, matumaini na upatanisho. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi na wanakwaya wote kwa kuungana na watu wa Mungu Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo kushiriki katika sala na maonesho haya ya muziki. Muziki una uwezo wa ajabu wa kuleta sauti mbalimbali pamoja kwa umoja, ambapo kila moja inachangia kitu cha kipekee katika ujumla wake. Kwa maana hiyo, kwaya inakuwa ni kielelezo bora cha maelewano na ushirikiano.

Papa Leo XIV akitoa neno la shukrani kwa wote waliochangia kufanikisha tukio hili
Papa Leo XIV akitoa neno la shukrani kwa wote waliochangia kufanikisha tukio hili   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ni jambo la maana kwamba Maandiko Matakatifu na Liturujia ya Kanisa huzungumzia "Makundi ya Malaika na Watakatifu" wakati wa kuelezea furaha ya mbinguni; si kwa sababu wanaimba kihalisi wakati wote, bali kwa sababu wakiwa wameunganishwa katika upendo, wanamtazama Mwenyezi Mungu pamoja na kupata utimilifu wa furaha ndani yake. Vijana hawa walipokuwa wanatumbuiza, muziki ulivuta kitu kikubwa kwa sababu ya umoja, kuliko kama muziki huu ungeporomoshwa na mtu mmoja na kwamba, hii ni tajiriba njema, inayofungua upeo na kuamsha ndani mwao shauku ya kwenda kuukabili upeo huo, ambao kimsingi ni Mungu Muumbaji mwenyewe. Kama vile watu wanavyoweza kufuata mkondo wa maji hadi kwenye chanzo chake, uzuri wa muziki unawaalika watu wa Mungu kukutana na Mungu ambaye ni Uzuri wenyewe.

Papaq Leo XIV akifuatilia muziki
Papaq Leo XIV akifuatilia muziki   (ANSA)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawahimiza vijana hawa kuendelea kukuza na kudumisha karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha yao na hivyo kuzipatia mwanya ili ziwaongoze kumwelekea Mwenyezi Mungu, hatima ya maisha ya binadamu na kwamba, wameumbwa kwa ajili ya mambo makuu na kwamba, Ulimwengu huu hautoshi kukidhi kiu yao ya ndani ya kutafuta maana na furaha ya maisha. Baba Mtakatifu anawapenda na kuwaombea wao, familia pamoja na nchi zao za asili. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Leo XIV ameomba amani iweze kutawala katika nyumba zao pamoja na nchi zao za asili. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee ameushukuru Mfuko wa Andrea Bocelli kwa kazi kubwa unaoifanya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wanaokabiliana na changamoto za kielimu na kijamii. Kupitia nguvu ya muziki, wanachangia katika utume wa Mama Kanisa wa kukuza maendeleo kamili ya kila mwanadamu , kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu. Mwenyezi Mungu apende kubariki jitihada hizi. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru watu wote waliohudhuria tukio hili na muziki na hatimaye, akawakabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Matia, mwishoni akawapatia baraka zake za kitume.

Mfuko wa Andrea Bocelli ni mfano mzuri wa kuigwa
Mfuko wa Andrea Bocelli ni mfano mzuri wa kuigwa   (ANSA)

Baba Mtakatifu  Leo XIV katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni NBC kutoka Marekani mara baada ya tukio la sala na nyimbo kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo amesema, anaipenda nchi ya Marekani kwa sababu ya msingi wa uhuru wake na kwamba, kwaya ya watoto hawa kutoka sehemu mbalimbali za dunia ni kielelezo cha kutia moyo. Anatambua kwamba, amezaliwa nchini Marekani, lakini kwa sasa amechaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro, akiwa na sauti ni fursa ya kuzungumza na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kuchaguliwa kwake kama Khalifa wa Matakatifu Petro kutoka nchini Marekani kwa wakati huu ni tukio la pekee sana, kama Mmarekani wa kwanza kuchaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, upendo wake kwa Marekani unakita mizizi yake zaidi katika uhuru, fursa na mwaliko kwa Marekani kuwa ni mahali ambapo watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanapata hifadhi na makazi yao. Anasema, familia yake ni sehemu ya wahamiaji, walikuwa ni watumwa na baadaye wakamiliki watumwa na kwamba, katika maisha na utume wake anaendelea kujitambua kwamba, amekuwa ni mtu wa pekee katika maisha na historia ya Marekani kwa sasa na kwa nyakati zijazo. Katika mipango ya safari zake za kitume nje ya Italia, Baba Mtakatifu anasema, hata nchi ya Marekani imo, ingawa mipango bado inaendelea kuboreshwa na hatimaye, kutangazwa rasmi.

Papa leo XIV Muziki
30 Julai 2026, 15:01