Hija ya Kichungaji ya Papa Leo XIV Kisiwani Lampedusa: Utu, Heshima na Haki Msingi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni fursa, changamoto kubwa na janga la Kimataifa linalopaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwa kulinda kwanza kabisa: Utu, heshima na maisha ya watu; amani na usalama; ulinzi na huduma makini. Kanisa linashiriki kikamilifu katika mchakato wa huduma na haki za wakimbizi na wahamiaji kwa kutambua kwamba hii ni sehemu ya maisha na utume wake ulimwenguni. Hii ni changamoto iliyovaliwa njuga na Papa Pio XII kuanzia mwaka 1944 na kunako mwaka 1952 akachapisha Waraka wa Kitume unaojulikana kama “Exsul familia” yaani “Familia ya Wahamiaji”; Waraka ambao kwa miaka yote hii umekuwa ni dira na mwongozo kwa ajili ya huduma ya kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Mtakatifu Paulo VI alilihamasisha Kanisa kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya Kitaifa na Kimataifa mintarafu: Utu, heshima na haki msingi za wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakasimama kidete kukuza na kudumisha mchakato wa huduma ya mshikamano na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji, bila kuangalia tofauti zao ya kitaifa, kidini, kiimani, kisiasa, kiuchumi na kijiografia! Jambo la msingi ni kuzingatia: haki, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko tangu alipoingia madarakani kunako mwaka 2013 akatoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi na wahamiaji; wahanga wa biashara haramu ya binadamu pamoja mifumo yote ya utumwa mamboleo mambo yanayoendelea kusigina na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji imekuwa ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwani kwa wakati huu kuna mambo mengi yanayochangia wimbi hili. Vita, kinzani, migogoro; athari za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha: ukame, mafuriko pamoja na majanga asilia ni kati ya mambo yanayopelekea wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Mama Kanisa anawahimiza Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kujenga Uekumene wa huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na maskini. Kwa Jumuiya ya Kimataifa anaitaka kuwa na sera ya wakimbizi na wahamiaji kimataifa inayojikita katika huduma na hifadhi; kwa kuwa na jicho la pekee: kwa makundi ya watoto, wanawake na wazeee ambayo yanalazimika kukimbia au kuhama nchi zao kutokana na sababu mbalimbali. Kunako mwaka 1985, Mtakatifu Yohane Paulo II akawa ni kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Ni matumaini ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Siku ya wakimbizi na wahamiaji inaadhimishwa tarehe 27 Septemba 2026 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Hata mmoja tu wa watoto hawa” kwa kufanya rejea kwenye Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo: “Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi.” Mt 18:5. Kwa uchaguzi wa kauli mbiu hii, Baba Mtakatifu Leo XIV kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 112 ya wakimbizi na wahamiaji duniani, anakusudia kuelezea wasiwasi wa Kanisa kwa watoto wadogo wanaohusika moja kwa moja na uhamiaji, akikumbuka wajibu wa kumkaribisha kila mmoja wao kama Injili inavyofundisha. Hii si mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kuzungumza kwa mamlaka juu ya suala hili, lakini hali ya sasa ya ukimbizi na uhamiaji inatoa changamoto mpya ambazo zinatishia kwa kiasi kikubwa: Utu, heshima haki msingi za watoto wadogo zenye kuhitaji majibu ya haraka yenye tija na ufanisi. Kwa hivyo, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hili sio suala la kujadili namba au asilimia, kwa sababu “hata mmoja tu” anathamani kubwa zaidi mbele ya Mungu na Jamii. Ilikuwa ni tarehe 8 Julai 2013 kwa mara ya kwanza kabisa, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alipofanya ziara yake ya kwanza kutoka mjini Vatican ili kwenda kwenye Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa Kisiwani hapo. Lakini pia, Baba Mtakatifu alipenda kusali na kuwaombea wale wote waliofariki dunia na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania na makaburi yao hayana alama wala kumbukumbu tena! Hili ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kiasi hata cha kuanzisha Idara ya Wakimbizi na wahamiaji kwenye Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, inayowajibika moja kwa moja kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Wale watu wanaopambana na mawimbi mazito ya Bahari ya Mediterrania; ni watu wanaoteseka kwenye vizuizi vya wakimbizi na wahamiaji kwa muda mrefu. Hii ni mifano ya watu ambao Yesu anawataka wafuasi wake kuwaonesha upendo na kuwainua tena katika utu, heshima na haki zao msingi. Inasikitisha kuona kwamba, pembezoni mwa miji mbalimbali duniani kumesheheni watu waliotelekezwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni watu wanaotengwa na kubaguliwa; wanaonyanyaswa na kudhulumiwa; maskini, wagonjwa na wale wanaoteseka. Kristo Yesu, kwa njia ya Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho yake makuu, anawataka wafuasi wake kuwafariji na kuwahurumia wale wanaoteseka; kuwalisha na kuwanywesha wenye njaa na kiu ya haki; ili wasikie kutoka katika undani wa maisha yao kwamba wanapendwa na Mungu na hatimaye, kuwaonesha njia inayowapeleka mbinguni kwa Bab. Ni katika muktadha wautekelezaji wa sera na mikakati ya Mama Kanisa kwa wakimbizi na wahamiaji, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 4 Julai 2026 anafanya hija ya kichungaji Kisiwani Lampedusa kwa kutembelea Makaburi na kutoa heshima kwa Marehemu waliolazwa mahali hapa! UNHCR inasema tangu mwaka 2014 wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 32, 700 wamefariki dunia wakijaribu kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Kunako mwezi Oktoba 2013 watu zaidi ya 368 walifariki dunia kwenye Kisiwa cha Lampedusa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji, baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa heshima yake kwa Sanamu ya Bikira Maria Bandari Salama “Portosalvo.” Anakutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, watoto wagonjwa pamoja na watu wa kujitolea.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Barham Ahmed Salih, hivi karibuni ametoa pongezi kwa ujasiri na azma ya wakimbizi duniani kote, akisisitiza kwamba, ingawa mtu anaweza kuwa mkimbizi kwa kipindi fulani, hali hiyo haipaswi kufafanua maisha yake yote. Amebainisha kwamba wakimbizi na wahamiaji huchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawijamii zinazowapokea, wakifanya kazi kama wafanyakazi, wanafunzi, wafanyabiashara, wasanii na viongozi. UNHCR inasema tangu mwaka 2014 wakimbizi na wahamiaji zaidi ya 32, 700 wamefariki dunia wakijaribu kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV Kisiwani Lampedusa ni kutaka kuikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji duniani inapaswa kushughulikiwa katika msingi wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Kisiwa cha Lampedusa ni mahali pa huzuni na masikitiko makubwa, lakini pia ni mahali bandari ya matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa hija yake kitume huko kwenye Visiwa vya “Grand Canaria na Tenerife alizungumzia tema hii ya wakimbizi na wahamiaji kwa kina na mapana mintarafu Mkataba wa Wahamiaji na Wakimbizi “The EU Pact on Migration and Asylum” ambao kimsingi ni vifungu vya sheria zinazosimamia uhamiaji na kuanzisha mfumo wa pamoja wa hifadhi katika ngazi ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, ambao unatoa matokeo kwa kuzingatia kanuni maadili ya Ulaya. Hizi ni Sheria ambazo zimepyaishwa na kuimarishwa kwa kuzingatia sera muhimu za Umoja wa Ulaya, EU kuhusu: Uhamiaji, hifadhi, ulinzi na usimamizi wa mipaka na ushirikiano. Haki ya wakimbizi na wahamiaji, unyambulifu wa kushughulikia changamoto hususan zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji pamoja na ulinzi wao. Mkataba huu mpya umeanza kutumika tarehe 12 Juni 2026 na kwamba, Mkataba ulipitishwa kunako mwaka 2024 na hivyo kurekebisha pamoja na kupyaisha jinsi ya Umoja wa Ulaya unavyopaswa kusimamia mipaka yake, kushughulikia maombi ya hifadhi; ugawanaji na uwajibikaji wa nchi wanachama katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.
