Ziara ya Kitume ya Papa Leo XIV,Barcelona:Katika giza tusiache kumtafuta Mungu
Na Angella Rwezaula–Vatican.
Katika mkesha wa maombi na vijana katika Uwanja wa Olimpiki wa Lluís Companys jijini Barcelona, Jumanne usiku, tarehe 9 Juni 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV alijibu shuhuda tatu zilizohusu uongofu, afya ya akili, mateso, vurugu na msamaha na mwisho tafakari yake zaidi. Mkesha huo ulifunguliwa na tamasha la kiutamaduni la mnara wa kibinadamu, ulioinuka haraka kutoka ardhini, hadi juu, mikono ikiwa imeshikamana kwa nguvu, watu wakipanda vizuri juu ya kila mmoja, kana kwamba wanataka kugusa anga, wakiwa imara, katika usawa kamili, wakiwa, wameungana, na kisha, kwa ghafla, wote wamerudi ardhini, kila mmoja akienda zake.
Mfano huo ulikuwa ni "urithi usioonekana wa ubinadamu," ambao, kama mfano uliashiria mada kuu ya maneno ya Papa. Akijibu maswali kutoka kwa vijana na kumalizia na mahubiri yake, alizungumzia mbio isiyozuiliwa ya mafanikio, tija, na ibada ya sanamu ambayo jamii inatuongoza, na wakati huo huo, anguko letu, nafasi hiyo tupu, uchovu wa roho, na hitaji la kupata kutotulia kwa afya jambo ambalo linatualika kwenda ndani zaidi ya ujuujuu ili kutafuta nuru ya kuangazia njia na shauku yetu ya ukweli na furaha."
Akizungumza na kijana aliyebatizwa hivi karibuni, Ferran, ambaye alizungumzia utupu alioupata licha ya kutafuta mafanikio na kutambuliwa, Papa Leo XIV alisema kwamba kutotulia huko si jambo la kuogopwa bali la kukumbatiwa. "Tumeumbwa kwa ajili ya usio na mwisho", alisema Papa. "Ndiyo maana kila upeo wa mwisho, kila hatua, kila mafanikio, huku yakituridhisha pia hutusukuma mbele na kutualika kuendelea kutafuta".
Papa Leo XIV alionya dhidi ya kile alichokielezea kama "ibada ya sanamu ya faida na utendaji na ibada ya kujiona kama mtu binafsi, akiviita kama dawa za ganzi zilizoundwa kupooza dhamiri yetu na kuiunda kwa maono fulani ya jamii. Badala yake, Papa aliwahimiza vijana kukuza ukimya na kuondoa ubinafsi katikati ya utamaduni wa kuvuruga kila mara." Aliwahimiza kutazama ndani ya mioyo yao: "Jaribu kutozidiwa na kasi ya maisha na vishawishi vya nje. Kuza muda wa ukimya, labda ukisimama kwa dakika chache kila siku kusoma Injili na kuzungumza na Mungu," alitoa ushauri
Ushuhuda wa pili ulitoka kwa Carmina, mwanamke kijana ambaye alizungumza waziwazi kuhusu mapambano yake ya kushuka moyo na jaribio la zamani la kujiua. Akiuliza ni wapi Mungu anaweza kupatikana wakati giza linaonekana kuwa tupu, alielezea kupokea kile alichokiita "nafasi ya pili" maishani. Akimshukuru kwa ujasiri wake, ambapo Papa Leo XIV alisema afya ya akili inazidi kutishiwa katika jamii zinazojiona kuwa zimeendelea. "Hii ni ishara kwamba kuna jambo lisilo sahihi katika dhana fulani ya maendeleo ambayo inawaweka watu kwenye shinikizo, matarajio na mivutano ambayo inaathiri usawa wa afya. Akitafakari Mateso ya Kristo, Papa Leo XIV alionesha uzoefu wa Yesu mwenyewe wa uchungu, kuachwa na mateso. "Mwana wa Mungu alichukua uchungu wote, upweke na mateso ya wanadamu juu yake mwenyewe, katika mwili wake mwenyewe. Katika saa hizo za giza, alipokuwa akifa msalabani, Yesu alishiriki maumivu yetu na kutufunulia uso wa Mungu mwenye huruma," Papa alibainisha.
Baba Mtakatifu hata hivyo alikiri kwamba mateso yanaweza kufanya ionekane kana kwamba Mungu hayupo, lakini alisisitiza kwamba Msalaba unaelezea historia tofauti. "Msalaba wa Yesu unatuambia kwamba Mungu hatuachi, kwamba yuko kando yetu, amesulubiwa pamoja nasi wakati wa maumivu na upweke mkubwa". Wakati huo huo, aliwaonya Wakristo dhidi ya kutoa maelezo rahisi kuhusu mateso. "Hatupaswi kuyafanya maumivu kuwa ya kiroho, tukiyahusisha na 'mapenzi ya Mungu' au mpango wake wa ajabu. Mungu hataki mateso. Anayabeba nasi," alifafanua Papa.
Ushuhuda wa tatu na wa mwisho ulitoka kwa mwanamke kijana anayeitwa Cecilia ambaye alisimulia utoto wake uliojaa vurugu za nyumbani, uraibu, na kutengana na familia yake. Baada ya kugundua imani kupitia usaidizi aliopokea katika kituo cha utunzaji cha Wakatoliki, aliuliza jinsi angeweza kumsamehe baba yake kwa kujaribu kumuua mama yake na jinsi angeweza kupatanishwa na Mungu. Akigeukia msamaha, Papa Leo XIV hakuuelezea kama kitendo kimoja bali kama mchakato wa taratibu. "Lazima tujifunze kuuona msamaha, tiba yenye nguvu ya uovu inayoponya majeraha yetu ya ndani kama sehemu ya mchakato na safari," alisema.
Akitambua jinsi msamaha unavyoweza kuwa mgumu kwa wale ambao wameteseka sana, Baba Mtakatifu Leo XIV alisisitiza kwamba mara nyingi ni kuanza na kumwomba Mungu aponye sehemu zilizojeruhiwa ndani ya moyo wa mwanadamu. "Tunasonga mbele kwa hatua ndogo kuelekea msamaha. Upatanisho na yaliyopita ni taratibu." Papa pia alifafanua kwamba msamaha haimaanishi lazima urejeshe uhusiano wa awali, hasa pale ambapo vurugu zimetokea.
"Tunaweza kudumisha mtazamo mzuri wa moyo kwa mtu huyo, kukataa aina zote za chuki au kisasi, kujitahidi kurekebisha uhusiano huo iwezekanavyo na labda kumwombea," alitoa ushauri. Akihitimisha kufafanua majibu yake, Papa Leo XIV aliwahimiza wale walio na kumbukumbu zenye uchungu "wasipoteze tumaini, wakiamini kwamba Mungu anaweza kubadilisha chuki polepole kuwa huruma na upole."
Giza hadi nuru
Kufuatia mazungumzo na vijana hao, Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa tafakari iliyolenga sura ya Nikodemu, akielezea kila mtu kama msafiri usiku, akitafuta maana, ukweli na upendo katikati ya kutokuwa na uhakika wa maisha. "Sisi ni waombaji wa upendo; tuna njaa na kiu kweli. Tunatafuta maana ya kina zaidi itakayotutegemeza, kututia moyo, na kutusaidia kuelewa fumbo la maisha yetu,"alisema.
Kisha Papa Leo XIV alitafakari ukweli kwamba kila mwanadamu hupata nyakati za giza, kuchanganyikiwa na shaka, maishani na katika imani. Lakini badala ya kuona nyakati hizi kama ishara za kushindwa, aliwaalika wote kuziona kama fursa za upyaisho. Papa alisema "Nikodemo anatufundisha kwamba usiku huu unaoambatana na maisha yetu, safari yetu ya imani, na historia tunayoishi, ni wakati wa baraka, mahali pa kuzaliwa upya, tumbo la uzazi ambalo huzaa maisha mapya kila wakati", alisema.
Kisha aliendelea kusema kwamba, giza linaweza kuondoa barakoa ambazo watu huvaa na kufichua kile ambacho ni muhimu, na kuunda kile alichokiita "nafasi tupu" ambapo Mungu anaweza kuleta mabadiliko. "Nafasi tupu' usiku huo huunda, hata wakati inachukua umbo la mateso au kutoridhika, la kukata tamaa au kutoamini, inaweza kuwa fursa ya kupokea maisha mapya, kubadilika na kufanywa upya." Kwa kutazama simulizi ya Injili ya kukutana kwa Yesu na Nikodemu, Papa Leo XIV alisisitiza kwamba Mungu hawakaribii wanadamu kwa hukumu, bali kwa hamu ya kuokoa na kurejesha. "Kwa sababu hiyo, sisi pia tumeitwa kutohukumu giza, wala usiku wa maisha yetu wenyewe, ule wa Kanisa, wala ule wa jamii inayotuzunguka,"alisema.
Baba Mtakatifu akigeuza mtazamo kuelekea Hispania ya leo hii aliwaalika waamini kutafakari kwa uaminifu changamoto zinazokabili jamii, ikiwa ni pamoja na umaskini, mgawanyiko wa kijamii na mabadiliko ya kiutamaduni, akiuliza ni aina gani ya mustakabali wanaotaka kujenga pamoja. "Nchi hii inaweza kuwa nafasi ya kukaribisha kwa wote, ambapo heshima ya kila mtu inaheshimiwa na kila mtu anapendwa kwa jinsi alivyo", alibainisha. Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kuhitimisha tafakari yake aliwatia moyo waamini wote waliokuwepo na wanaofuatilia kutoka mbali kuendelea kumtafuta Mungu kwa uwazi na uaminifu, wakiwa na uhakika kwamba nuru ya Injili inaweza kuwaongoza kutoka usiku hadi nuru. Mungu hataki chochote kipotee. Hata sasa anatamani kutupatia uzima wa milele na kutuongoza kwenye furaha isiyo na mwisho".
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here
