Ziara ya Kichungaji ya Papa Leo XIV Pavia: Liturujia ya Neno la Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija za Kitume na Kichungaji zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ndani na nje ya Italia zinalenga pamoja na mambo mengine kuwaimarisha waamini katika fadhila ya imani, matumaini, mapendo na mshikamano, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu chimbuko la maisha na uzima wa milele. Kwa Baba Mtakatifu ziara hizi zinakuwa ni fursa ya kukutana mubashara na watu wa Mungu katika maeneo yao, ili kuhamasisha na kuragibisha mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu; ustawi, maendeleo sanjari na haki msingi za binadamu. Hii pia ni nafsi ya kuangalia changamoto na fursa zinazopatikana katika maeneo husika tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji unaofumbata maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 20 Juni 2026 amefanya hija ya kichungaji kwa kutembelea Mkoa wa Lombardia, Kaskazini mwa Italia katika miji miwili ya Pavia na Sant’Angelo Lodigiano; miji ambayo imeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Leo XIV. Mtakatifu Augustino ni Muasisi wa Shirika la Waagostiniani: “The Order of St. Augustine, OSA.” Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Leo XIV alitia nia ya kutembelea maeneo ya maisha na utume wa Mtakatifu Augustino. Mji wa Pavia unahifadhi masalia ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa ambaye katika mafundisho yake aliutazama unyenyekevu kama msingi wa imani ya Kikristo. Kwa tajiriba ya maisha na utume wake, Mtakatifu Augustino hatimaye alitambua kwamba ni mtu tu aliye na unyekekevu ndiye anaweza kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni unyenyekevu wenyewe maana “hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu.” (Flp. 2:6-7).
Mji wa Pili ni Sant’Angelo Lodigiano unaohifadhi moyo wa Mtakatifu Francesca Cabrini, Muasisi wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyezaliwa mjini Lodigiano na kuitupa mkono dunia huko Chicago, nchini Marekani, mahali alipozaliwa Baba Mtakatifu Leo XIV. Akiwa mjini Pavia, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na watoto walioathirika na ugonjwa wa Saratani wanaohudumiwa katika Kituo cha “Centro Nazionale di Androterapia Oncologica,” amekutana na kusalimiana na Jumuiya ya Waagostiani wanaoishi na kufanya utume wao mjini Pavia na hatimaye, akashiriki katika Maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu kwenye Kanisa kuu la “San Pietro in Ciel D’oro. Maaskofu wa Kanisa Katoliki mkoa wa Lombardi, pamoja na watu watakatifu wa Mungu wameshiriki katika Ibada hii ya Liturujia ya Neno la Mungu na hatimaye akapata fursa ya kutoa heshima zake kwenye Masalia ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Baba Mtakatifu amepata pia fursa ya kusali mbele ya Altare ya Mtakatifu Siro, Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Pavia, anayetambulika na kuheshimika kwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu si tu Jimboni Pavia, bali hata: Verona, Brescia, Genova na Asti. Inakadiriwa kwamba alifariki dunia kunako mwaka 380 baada ya kutekeleza utume mzito wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kama sehemu ya Liturujia ya Neno la Mungu, amewataka watu wa Mungu kuwa na moyo wa imani katika shida na changamoto za maisha; wawe na matumaini ya Injili, huku wakiendelea kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu, tayari kutekeleza vyema shughuli za kichungaji na uinjilishaji wa kina.
Kristo Yesu ndiye jiwe la msingi na kiini cha maisha na utume wa Kanisa, mwaliko kwa Makleri kujenga na kudumisha udugu wa Kipadre na kuendelea kushirikiana kwa karibu na waamini walei katika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwani ushuhuda wa imani hai unawafanya kuwa ni mawe hai, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha kwamba, Jumuiya ya Pavia inakita mizizi yake katika Mapokeo ya miaka mingi, inaendelea kusoma alama za nyakati, bila kukata wala kukatishwa tamaa na shida pamoja na changamoto zinazoibuliwa katika ulimwengu mamboleo, kama sehemu ya mchakato wa kurithisha imani. Waamini wawe na moyo wa imani unaorutubisha matumaini, ili hatimaye kukataa usorajua tasa. Pale imani yao inapopata changamoto ipambanue jinsi mvinyo unavyoweza kutokana na maji, na jinsi ambavyo ngano inavyoweza kumea kati ya magugu. Huu ni mwaliko kwa waamini wa Jimbo Katoliki la Pavia kuwa ni mawe hai, huku wakishikamana na kuambatana na Kristo Yesu. “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.” 1Pt 2:4-10. Kristo Yesu ni msingi wa maisha ya kiroho, safari ya kikanisa, mchakato wa utekelezaji wa shughuli za kichungaji sanjari na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Ujenzi wa maisha ya kiroho upate chimbuko na hatima yake katika Kristo Yesu, chemchemi ya mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika Neno la Mungu. Hii ni hija ambayo kwayo Kanisa linatembea bega kwa bega, bila kugawanyika, kwa kutambuana kuwa wote ni ndugu wamoja katika Kristo Yesu, wanaofanya kazi kwa: furaha, umoja na ushirika katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu pamoja na kuendelea kujikita katika mambo msingi, yaani kuishi na Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Huu ni wosia ambao Baba Mtakatifu Leo XIV anautoa kwa Makleri kwani katika maisha na utume wao wanaweza kuteseka na hatimaye kukumbwa na ugonjwa wa sonona na msongo wa mawazo kutokana na kuchoka na kazi nyingi wanazozifanya, lakini daima wakumbuke kurejea kwenye kiini cha maisha na utume wao, yaani kwa Kristo Yesu, jiwe kuu la msingi. Makleri wajenge na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa Kipadre pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi na waamini walei, ili kuweka pamoja karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na ujenzi wa Kanisa la Jimbo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Pavia kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu, ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika kutangaza na kurithisha imani. Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayookoa, inayoibua uzuri wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini na ndani ya jamii. Kiini cha Injili hii ni Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu unaofunua Fumbo la Mungu na kwamba binadamu naye ni sehemu ya Fumbo hili. Hii ni huduma ya kichungaji katika mtindo wa kimisionari unaozingatia mambo msingi, yale yaliyo mazuri na makubwa zaidi, yenye kuvutia na yaliyo muhimu zaidi. Rej. Evangelii gaudium, 35. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, imani na sala katika maisha yao inakuwa ni kikolezo cha chaguzi, matendo na mahusiano katika maisha. Mama Kanisa anaendelea kufanya hija ya maisha na utume wake katika shida na changamoto mbalimbali; katika matumaini ya watu wa Mungu, na kuendelea kutambua kwamba, Kanisa ni mtaalamu wa sanaa ya kusikiliza kwa makini, kuwasindikiza waja wake pamoja na kuganga na kuponya uhusiano wa kifamilia pamoja na wale wote wanaojiandaa kupokea Sakramenti za Kanisa au wale ambao wamelipatia Kanisa kisogo.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Pavia kuhakikisha kwamba, wanawaendea na kuwafikia watu wengi zaidi kwa njia ya furaha ya Injili, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kusoma na kutafakari Neno la Mungu kama wanavyofanya kwenye Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Usikivu makini pamoja na tafakari ya kina ni mambo yanayopyaisha ushuhuda wa maisha ya Kikristo sanjari na ushiriki wa waamini katika mashirika na vyama vya kitume. Hizi ni cheche zinazowasukuma waamini kujenga mtandao wa upendo na mshikamano na maskini. Baba Mtakatifu anaendelea kulihimiza Jimbo Katoliki la Pavia ili kuhakikisha linatoa kipaumbele cha pekee kwa shughuli za kichungaji kwenye Chuo Kikuu na Taasisi za Elimu ya Juu, sanjari na kuendeleza majadiliano na Ulimwengu wa tamaduni. Imani iwasaidie waamini kutafuta na kuambata ukweli, haki na mshikamano wa kuweza kutembea bega kwa bega. Waamini waendelee kujenga Kanisa la kimisionari na la kisinodi katika maisha ya watu wa kawaida, daima kwa kuendelea kusoma alama za nyakati kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji, unaosimikwa katika ushirika, mang’amuzi ya pamoja sanjari na kubainisha miradi ya pamoja, wakijitahidi kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu pamoja na uwajibikaji. Bikira Maria Mama wa Kanisa, awajalie kadiri ya hamu ya nyoyo zao kila wanachotamani kupata, ili kuishi na kutangaza Injili inayofumbatwa katika upendo wa kidugu unaowafanya kuwa ni Taifa la pekee wanapomwendea Mungu.
Kwa upande wake Askofu Corrado Sanguineti wa Jimbo Katoliki Pavia katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV kuongoza Ibada ya Neno la Mungu, amekumbusha kwamba, Kanisa hili lina Mapokeo ya Kale na kwamba, Mwaka 2007 Baba Mtakatifu Benedikto XVI alilitembelea na Mwaka 2024 katika Maadhimisho ya Miaka 1,300 tangu masalia ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa yahamishiwe kutoka Sardegna hadi Jimboni Pavia, alishiriki tukio hili la kihistoria kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri. Kanisa la Jimbo la Pavia linaendelea kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ya Kimisionari; kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, kung’amua na kutekeleza kwa pamoja vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa, huku waamini walei wakiwajibika vyema. Kanisa katika shughuli zake za kichungaji linaendelea kutangaza na kushuhudia Injili katika medani mbalimbali za maisha ya kijamii, maeneo ya kazi; katika huduma ya elimu na afya; kwa familia na vijana wa kizazi kipya; kwenye Jumuiya za wakimbizi na wahamiaji pamoja na kuendelea kusimama kidete kupambana na umaskini unaopelekea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, ili kutangaza na kushuhudia furaha na uzuri wa Injili.
Naye Mheshimiwa Sana Padre Joseph Lawrence Farrell, OSA, Mkuu wa Shirika la Waagustiani Ulimwenguni katika hotuba yake amesema kwamba, Mwaka 2027, wanaadhimisha kumbukizi ya Miaka 700 tangu Shirika lao, lilipopewa dhamana ya kuhifadhi Masalia ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Mwaka 2030, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 1600 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Augustino mwaka 430. Miali ya moto inaashiria hamu kubwa inayohuisha nyoyo za Watoto wa Mtakatifu Augustino; wanawakilisha wale wanaojitolea kuishi katika maisha ya kijumuiya na imani inayosimikwa katika upendo wa Kikristo. Miale hiyo mingi pia inawakilisha moyo mmoja unaounganisha wanadamu wote katika hija yao kwa Mwenyezi Mungu. Imani ya Mtakatifu Augustine kwa Kristo Yesu, pamoja na mafundisho na hekima aliyoliachia Kanisa na ulimwengu, vinaendelea kuwatia moyo watu wa kila zama. Mwishoni wanamwombea kwa Daktari wa Neema ili aendelee kumtia moyo na kumwongoza katika huduma yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
