Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea Toba, Wongofu na Utakatifu wa Mapadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 amefanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inueni macho yenu.” Yn 4:35. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa “Las Palmas de Grand Canaria” Ijumaa tarehe 12 Juni 2026 amekutana na kuzungumza na wakimbizi na wahamiaji na baadaye akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Bandari ya “Santa Cruz de Tenerife.” Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Huu ni mwaliko kwa Mapadre kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho na kiutu unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu.” Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu, uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta maisha na uzima wa milele!
Kristo Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Margherita Maria Alacoque huko Paray-le-Monial, alimwomba, watu wafanye toba na malipizi kwa maondoleo ya dhambi zinazoendelea kuutesa Moyo wake Mtakatifu. Hii ndiyo dhamana na wajibu wa Mapadre kuhakikisha kwamba, waamini wanaendeleza ibada ya toba na maondoleo ya dhambi, kama sehemu ya hija ya toba na wongofu wa ndani inayotekelezwa na kila Mbatizwa ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 aliitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Mapadre wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu. Kwa kupakwa mafuta, Mapadre wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kanisa na watu wake, kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu. Mapadre watoe kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Mapadre wasikubali kumezwa na malimwengu, bali: utii, useja na ufukara, viwe ni dira na mwongozo katika maisha na utume wao. Utakatifu wa Mapadre ni hitaji muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Ukweli huu wa imani katika maisha na utume wa Mama Kanisa, unagusa hata maisha ya waamini walei ambao usiku na mchana wanatafuta utakatifu wao, kwa kutambua au kwa kutokujua kutoka kwa mtu wa Mungu. Waamini wanamwona Padre kuwa ni mshauri wa maisha ya kiroho, mpatanishi wa amani; mtu mwenye hekima na busara. Ni kiongozi salama ambaye watu wa Mungu wanaweza kujiaminisha kwake nyakati ngumu na wakati wa majaribu ya maisha, ili kuonja na hatimaye, kupata faraja na usalama wao.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa Mapadre wanapoadhimisha Ijumaa tarehe 12 Juni 2026 Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre anasema, utakatifu ni kushiriki katika Fumbo la Kristo Yesu, ni safari ya umoja na kwamba, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni moyo wa Watakatifu, mahali ambapo utakatifu wa Mapadre unafunuliwa katika unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wote; kwa kuwa na huruma pamoja na kujenga utamaduni wa kusikiliza. Mwaliko wa utakatifu na ukamilifu wa maisha ni changamoto endelevu, lakini kwa namna ya pekee kwa Mapadre, kwani huu ni utambulisho kwa wale wote wanaotaka kushiriki katika maisha ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko wa kujiachilia, kujisadaka na hatimaye kujiaminisha mbele ya Mungu, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaletea mabadiliko ya maisha, kwa kutambua kwamba, wito huu wa kushiriki katika utakatifu wa Mungu unahifadhiwa katika vyombo vya udongo. Rej 2 Kor 4:7.
Hii ni kutokana na mapungufu, udhaifu, uchovu na madonda wanayobeba ndani mwao Mapadre, lakini Mapadre wanapata faraja ya kweli kutoka katika Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu; katika Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hii ni safari ya umoja inayopata chimbuko lake katika maisha ya Kisakramenti na hususan Ekaristi Takatifu inayoadhimishwa kila siku. Mapadre watambue kwamba, wanaitwa ili kuwa “Alter Christus yaani: “Kristo mwingine”, hadhi inayowataka Mapadre kuwa ni wanyenyekevu, kutambua udhaifu wao wa kibinadamu na hivyo kukimbilia huruma ya Mungu mara kwa mara kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Ni mwaliko wa kujikita katika maisha ya sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu; huduma kwa watu wa Mungu inayosimikwa katika unyenyekevu; kwa maneno mafupi huu ni mwaliko wa kuungana na Kristo Yesu kila siku ya maisha, kwa kuishi vyema neema na baraka zake katika sala, utumishi, uhusiano, uchovu, mapungufu na hata pale upendo unapotumiwa vibaya, yote haya ni maeneo ambayo Mwenyezi Mungu anaweza kuyatumia kufunua upendo wake usiokuwa na mipaka. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni moyo wa Watakatifu, mahali ambapo utakatifu wa Mapadre unafunuliwa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema Padre mwenye moyo kamili na sahihi anafanya tafakari ya kina kati kati ya matendo yake, ni mtu mwenye huruma, mwaminifu katika majaribu; mwenye furaha ya kweli katika kujisadaka bila ya kujibakiza. Ulimwengu unahitaji sana wachungaji wanaotangaza na kushuhudia moyo uliopatanishwa, moyo unaoeneza harufu nzuri ya utakatifu wa Kristo Yesu. Maisha ya Mapadre thabiti yaliyowekwa katika Moyo Mtakatifu wa Yesu ni ishara ya kuaminika; kielelezo cha umoja, amani na huruma. Katika Ulimwengu mamboleo uliogawanyika na kusambaratika kwa hofu, Mapadre wanaweza kuwa ni wajenzi wa: haki na amani; Mashuhuda wa huruma ya Kristo Mchungaji mwema anayetambua jinsi ya kuwakusanya wanaondoo waliotawanyika na kuwaponya waliojeruhiwa, ili kuwa tayari kuonjesha upendo unaofurika hadi kutoka nje; upendo unaogeuka kuwa sadaka na fursa ya watu kukutana. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni mahali ambapo utakatifu unajidhihirisha kama ukaribu na huruma; unyenyekevu na ujasiri; kwa kujisadaka kwa ajili ya wote, moyo ambao uko wazi tayari kwa wale walioko tayari kuingia ili kupata malisho na raha. Rej. Yn 10:9.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema hii ni changamoto kwa Mapadre kujenga uhusiano na Mungu pamoja na watu wengine na hivyo kuwafanya kuwa ni majirani wema na hatimaye kujenga mtandao wa ukaribu, huruma na kusikiliza na kwa njia hii, safari ya utakatifu wa maisha inatimizwa ndani mwao na hivyo kuishi si kwa ajili ya yao, bali ushuhuda wa Kristo Yesu anayeishi ndani mwao. Rej. Gal 2:20. Hii ni changamoto kwa Mapadre kuishi katika umoja na udugu wa Kikuhani; kwa kusikilizana na kusaidiana, kwani Padre anayejitenga, polepole atajikuta ametumbukia kwenye upweke hasi, lakini Padre anayeishi na kushikamana na Mapadre wengine atakuwa na kusitawi; mwaliko wa kujenga na kudumisha upendo na umoja. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika Mapadre kupyaisha kila siku wito wao mbele ya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu kwa sababu Upadre ni upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu. Upendo huu ni dhamana na amana kwamba hakuna chochote kati yao kinachoweza kupotea, ikiwa wote watajitoa na kujisadaka. Baba Mtakatifu amewakabidhi Mapadre wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mapadre wote, ili Yeye ambaye alilihifadhi Fumbo la Mwanaye mpendwa Moyoni mwake, awafundishe kuulinda na kuufanya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu udunde ndani ya mioyo yao pia.
