Tafuta

Papa Leo XIV:Tusali kwa ajili ya kaka na dada zetu waliopoteza maisha yao baharini

Papa Leo XIV katika mahubiri yake alitafakari kuhusu upendo,mateso na unyenyekevu Alhamisi jioni,Juni 11,katika Ibada ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Gran Canaria,kisiwa kikubwa cha Hispania kilicho karibu na pwani ya Magharibi ya Afrika,ambapo ni mahali pa kuwasili kwa wahamiaji wanaotafuta maisha mapya barani Ulaya.“Tukiwa tumechochewa na upendo wa Moyo wa Yesu,tuwe wabebaji wa huruma yake na amani yake,ili vita vikome duniani."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika Ziara yake ya Kitume na kituo chake cha Mwisho huko Visiwa vya Kanari aliongoza Ibada ya Misa Takatifu, Alhamisi jioni, tarehe 11 Juni 2026 ikiwa ni tayari kwenye Mkesha wa Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Misa ilifanyika katika Uwanja wa michezo huko Las Palmas ambapo waamini 50,000 waliudhuria tukio hili muhimu. Na ndiyo ilikuwa hitimisho la siku yake ya kwanza katika uwanja wa mji huu. 

Misa ya Papa Leo XIV katika Visiwa vya Kanari
Misa ya Papa Leo XIV katika Visiwa vya Kanari   (@Vatican Media)

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu

Baba Mtakatifu akianza mahubiri alisema: “Wapendwa kaka na dada, baada ya siku yenye wingi wa kukutana na kushiriki, sasa, nikisherehekea Ekaristi hii pamoja nanyi, kwanza kabisa nataka kumshukuru Bwana kwa mema mengi yanayofanyika hapa kila siku, nikimkabidhi Yeye kujitolea kwa wote na wakati huo huo mateso ambayo nchi hii inashuhudia. Pia ninawaalika kusali pamoja, katika Misa hii Takatifu, kwa ajili ya kaka na dada waliopoteza maisha yao baharini. Tunaleta kila kitu madhabahuni, pamoja na mkate na divai, tunapoingia, pamoja na sherehe ya jioni ya Mkesha, katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambayo nchini Hispania yote imewekwa wakfu kwake. Tumwombe Bwana kwamba kwa wakati huu hisia zile zile za ubinadamu, upole na huruma za Moyo Mwokozi ziweze kuwa hai ndani yetu.”

Misa katika Kisiwa cha Kanari
Misa katika Kisiwa cha Kanari   (@Vatican Media)

Mungu anawakumbusha Waisraeli kuhusu upendo

Baba Mtakatifu aliendelea kusema, “Tujiruhusu kuongozwa katika kutafakari kwetu kwa masomo tuliyosikia. Kwanza kabisa, Mungu anawakumbusha Waisraeli kuhusu upendo usio na masharti ambao aliwapenda nao. Hakuwachagua kwa sababu walikuwa na mapendeleo, zawadi, au sifa zozote maalum, bali kwa upendo safi (taz. Kum 7:7-9), na ataendelea kuwapenda siku zote, hata wakati, kwa sababu ya mioyo yao migumu, hawarudishi hisia zake. Huu ni upendo wa Mungu, ambapo wito wetu wa kupenda umejikita. Hautegemei hesabu, wala hisia tu, wala hauwezi kupunguzwa kuwa upendo rahisi, bali unaenea katika nafsi yetu yote. 

Papa akitoa mahubiri
Papa akitoa mahubiri   (@Vatican Media)

Moto kwa ajili ya roho, mwanga kwa ajili ya akili, msukumo usiozuilika wa uhuru, amani na wakati huo huo mateso kwa ajili ya moyo, ambao hudunda kwa upatanisho na mioyo mingine, ikimhusisha mtu mzima. Kwa sababu upendo ni wa asili kwa wanadamu; kiukweli, ni sharti la ukamilifu wa kuwepo. Hivi ndivyo upendo unavyooneshwa kwetu katika ubinadamu wa Mwokozi na katika harakati za Moyo wake Mtakatifu Zaidi: usiobadilika na mwaminifu hata katika hali ya kutoelewana na kukataliwa, hofu, huzuni na upinzani wa kibinadamu(Lk 22,39-46).

Maaskofu katika misa
Maaskofu katika misa   (@Vatican Media)

Mwitikio bora wa upendo kwa moyo wa Yesu ni kwa kaka na dada

Na ni katika uso huu wa Mungu, daima "katika upendo," ambaye anatamani sana mema yetu na furaha yetu kamili, Papa alieleza " ndipo tunapotambua njia ya maisha, kujifunza njia mpya ya kuishi na kuhusianisha, kigezo tofauti cha kutathmini maamuzi, mtindo mpya na wa kuchochea wa kujenga ushirika. Katika suala hili, Papa Francisko, akizungumzia upendo wa Kristo, alisema kwamba: "mwitikio bora kwa upendo wa Moyo wake ni upendo kwa kaka na dada zetu" (Dilexit nos, 167) na akaongeza: "hakuna ishara kubwa zaidi tunayoweza kumpa ili kurudisha upendo kwa upendo.

Misa katika kisiwa kikubwa cha Kanari
Misa katika kisiwa kikubwa cha Kanari   (@Vatican Media)

"Kurudisha upendo kwa upendo": Huu ni ubadilishanaji wa ajabu, "biashara ya kupendeza"  ambayo Injili inatualika tuvutwe, ikitafsiri kipimo kisicho na kikomo cha upendo wa Mungu kuwa ukarimu ambao tunamtumikia, kila siku, katika kaka na dada katika Yeye mwenyewe anayemweka njiani mwetu. Hasa kwa wale walio na uhitaji mkubwa, wasio na ulinzi, wasioweza kutoa chochote (taz. Lk 6:32-36).

Umati wa waamini katika Misa kwenye Kisiwa cha Kanari
Umati wa waamini katika Misa kwenye Kisiwa cha Kanari   (@Vatican Media)

Papa aliwapongeza kwa ukarimu kwamba "Kama inavyotokea kisiwani hapa, katika kukaribisha, kushiriki, katika kutoa bila ubinafsi.” Hata hivyo, kujitolea kwa Moyo wa Kristo hakuishii hapo. Kunaendelea zaidi, kujitoa kumsaidia kila mtu si tu kuishi, bali pia kupata tena kujiamini na kuanza safari yake, kukua na kustawi kikamilifu katika upekee wake, kwa manufaa ya wote. Katika suala hili, Papa Benedikto XVI aliandika kwamba upendo "ambao Yesu Kristo alishuhudia kwa maisha yake ya kidunia [...] ndiyo nguvu kuu ya kuendesha maendeleo halisi ya kila mtu na ya wanadamu wote." (Caritas in veritate, 1).

Mama Maria utuombee
Mama Maria utuombee   (@Vatican Media)

Mungu alituma mwanae wa pekee

Baba Mtakatifu Leo alijikita kutazama katika somo la pili, kwamba "Mtakatifu Yohane alitukumbusha kwamba “Mungu alimtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa njia yake” (1 Yoh 4:9). Maneno yake yanarudia yale ya Yesu, ambaye alisema kwamba alikuja ili tupate uzima, na kuupata tele (taz. Yh 10:10), na ambaye alimwagiza yule aliyepooza na kuponywa kuwa: “Inuka, beba kitanda chako, utembee” (Mk 2:9). Katika misemo hii, tunatambua mwaliko wa kukumbatia mateso kwa upendo wa kimama, lakini wakati huo huo kuwaandaa na kuwatia moyo waliojeruhiwa ili waweze kuinuka na kusonga mbele tena, kuelekea maisha huru na yenye heshima.

Wakubwa kwa wadogo wakishiriki misa Takatifu
Wakubwa kwa wadogo wakishiriki misa Takatifu   (@Vatican Media)

Tumaini katika safari

Hakika, Papa Leo alionya kuwa "upendo wetu haupaswi kuwa msaada tu, bali ujumuishaji wa watu kwa ajili ya utambuzi wao kamili, kiroho, kiakili, na kimwili na ujumuishi wao wenye hadhi na kujenga katika jamii (taz. Fratelli tutti, 129). Ni kwa njia hiyo  tu, ndipo kukutana kwetu, hata katika kukabiliana na matukio magumu na yenye uchungu, kutakuwa fursa za kupanda mbegu za matumaini katika safari ya wanadamu kuelekea mustakabali bora.

Wakati wa kutoa sadaka
Wakati wa kutoa sadaka   (@Vatican Media)

Moyo wa Kristo:utajiri unatupofusha

Papa alikazia kusema alivyopenda kuzingatia "Neno la Mungu tulilosikia, kuhusu sifa moja ya mwisho ya Moyo wa Kristo: unyenyekevu (taz. Mt. 11:29). Moyo wa Yesu ni mnyenyekevu, na ndiyo maana mapigo yake hayasikiwi na "wasomi," "wenye hekima," yaani, wale wanaojiona kuwa wanajitosheleza, kujua kila kitu, kutohitaji Mungu wala wengine. Kiukweli, watu hawa, wamezidiwa na kelele za "umimi" wenye majivuno, waliopo kila mahali, na wenye kufadhaika, hawana ukimya unaohitajika kusikia ndani yao wenyewe na ndani ya kaka na dada zao mapigo ya upendo yaliyofichwa.

"Mara nyingi, utajiri hutupofusha, hadi kufikia hatua ya kufikiria kwamba furaha yetu inaweza kupatikana tu ikiwa tutaweza kuishi bila wengine"(Dilexi te, 108). Yesu, kwa upande mwingine, anatufundisha kinyume chake: ili kupata furaha ya kweli ya maisha, ambayo inakaa katika upendo, ni muhimu kujiondoa kutoka kwenye misingi ya kiburi inayogawanya, na kujikuta katika unyenyekevu unaotuunganisha kama kaka na dada.

Sanamu ya Bikira Maria na Mtoto
Sanamu ya Bikira Maria na Mtoto   (@Vatican Media)

Mtakatifu Agostino:palipo na upendo kuna amani

Mtakatifu Agostino alisema: “Pale palipo na upendo, kuna amani, na palipo na unyenyekevu, kuna upendo”(Katika Barua ya Kwanza ya Mtakatifu Yohane kwa Waparthi, Dibaji). Ndivyo ilivyo. Pale palipo na unyenyekevu wa kweli, kuna upendo, na palipo na upendo, kuna amani, Papa alikazia tena, kwa sababu aliongeza " ni katika unyenyekevu pekee ndipo tunapojua kweli sisi ni akina nani na, kwa hivyo, tunaweza kupendana, kukutana, kujitolea kwa kila mmoja, na kusameheana kiukweli.

Neno la Mungu lituongoze
Neno la Mungu lituongoze   (@Vatican Media)
Maua yalipopambwa kwa ajili ya Misa
Maua yalipopambwa kwa ajili ya Misa   (@Vatican Media)

Tunaabudu Moyo Mtakatifu wa Yesu

"Kaka na dada wapendwa, Papa Leo XIV aliongeza:"leo tunaabudu Moyo Mtakatifu wa Yesu, moyo ambao mara nyingi tunauonesha ukivikwa taji la miiba na kuwaka kwa moto, kulingana na maono ya Mtakatifu Margaret Mary Alacoque. Tukumbuke kwamba sisi ni uwepo hai wa Bwana duniani (Lumen Gentium,8). Kwa hivyo, “tutazame kila mmoja wetu, si leo tu, bali kila wakati, kwa heshima na uaminifu, na tupyaishe, katika ufahamu huu, kujitolea kwetu kutimiza ndani yetu, kupitia upendo, kile kilichopungua katika mateso ya Kristo, kwa ajili ya mema ya Kanisa (taz. Kol 1:24).” Kwa kuhitimisha Papa Leo alisema kwamba “Tukiwa tumechochewa na upendo wa Moyo wake, tuwe wabebaji wa huruma yake na amani yake, ili vita vikome duniani na ubinadamu mpya, uliopatanishwa katika upendo, uweze kukua karibu nasi.”

Wakati wa misa: waamini vijana
Wakati wa misa: waamini vijana   (@Vatican Media)
Waamini wa kila kabila na rangi wameshiriki misa
Waamini wa kila kabila na rangi wameshiriki misa   (@Vatican Media)
Misa ya Papa Leo XIV katika Kisiwa Kikubwa cha Kanari Juni 11,2026
Kabla ya Misa Papa alizungukia uwanja
Kabla ya Misa Papa alizungukia uwanja   (@Vatican Media)
KANISA LAVISIWAVYA KANARI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

11 Juni 2026, 21:30