Papa Leo XIV: Wosia Kwa Vijana: Amani na Furaha ya Kweli! Upendo kwa Mungu na Jirani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kama sehemu ya juhudi za uhamasishaji za Chuo Kikuu cha Wafranciskani cha Steubenville, Ohio, nchini Marekani; "Steubenville Summer Youth Conferences" Makongamano ya Vijana ya Majira ya joto ya Steubenville hutoa fursa ya pekee kwa vijana wa Jumuiya za Kikatoliki kutoka sehemu mbalimbali za Marekani kukusanyika kwa ajili ya: kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kuabudu na Kumtukuza Mwenyezi Mungu chanzo na kilele cha wema na utakatifu wa maisha. Hiki ni kipindi cha sala, ujenzi wa umoja na udugu wa kibinadamu sanjari na kutoa burudani ya muziki safi unaogusa na kutikisa sakafu ya maisha ya vijana wa kizazi kipya. Kongamano hili linawashirikisha vijana zaidi ya 50,000 wa Kikatoliki kutoka sehemu mbalimbali za Marekani na lilianzishwa kunako mwaka 1976 na kwa Mwaka 2026 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake sanjari na Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, mtu wa amani na majadiliano, aliyejitahidi kuishi ukweli katika hali ya unyenyekevu. Kwa hakika maisha yake yanang'aa kwa mwanga angavu, kwa kuwa yalitiwa msukumo na ujasiri wa kuishi katika ukweli, na ufahamu kwamba ulimwengu wa amani unajengwa kuanzia na mioyo ya unyenyekevu iliyoelekezwa kuelekea mji wa mbinguni. Moyo mnyenyekevu na wa kupenda amani ndio ambao Baba Mtakatifu Leo XIV anatamani kuuona kwa kila mmoja wao na kwa watu wote wa Mungu. Anasema, wakati huu wa kufanya kumbukizi ya ujumbe wake wa amani na Mwenyezi Mungu, majirani pamoja na kazi yote ya uumbaji.
Maadhimisho haya yanaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 9 Julai hadi tarehe 12 Julai 2026. Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya maadhimisho haya anasema, amani ya kudumu na furaha ya kweli inapata chimbuko lake kwa kukutana na Mwenyezi Mungu, kwa kujiaminisha katika uweza na nguvu yake ya kuweza kumletea mwanadamu mabadiliko ya kweli katika maisha!Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya wanaposhiriki Kongamano hili, iwe ni fursa ya kutafakari pia umuhimu wa kutafuta na kuambata amani ya kudumu na furaha ya kweli mambo msingi katika hija ya maisha ya binadamu. Kama wangekuwepo wakati wa maisha na utume wa Mtakatifu Francisko, bila shaka kama angekutana nao, angewaangalia na hatimaye, kuwaonjesha furaha ya kukata na shoka na bila shaka angesema: “Amani na salama.” Katika sala ya Mtakatifu Francisko, inamwonesha kuwa ni mtu aliyeshikamana na upendo wa Kristo Yesu katika mwili na roho yake; Madonda Matakatifu yawasaidie watu kujifunza kumpenda Kristo Yesu, pamoja na jirani zao. Wajifunze kumtafakari na kumfuasa Kristo Yesu maskini na Mteswa. Imani, matumaini na mapendo ya Mtakatifu Francisko, yawasaidie kubeba mizigo ya maisha, ili hatimaye, waonje huruma ya Baba na faraja ya Roho Mtakatifu.
Madonda ya watu wa Mungu yagangwe na kuponywa na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili hatimaye, waweze kama Mtakatifu Francisko wa Assisi mashuhuda wa huruma ya Mungu, huku wakiendelea kuganga, kuponya na kupyaisha maisha, kwa wale wote wanaomtafuta Kristo Yesu katika ukweli. Madonda Matakatifu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi yawe ni mng’ao wa maisha na ufufuko yanayoelekeza njia mpya za haki, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana kutia nia ya kutafuta, kuambata na kusambaza amani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko aliyesambaza amani kwa sababu ndani mwake, ilikuwemo chemchemi ya amani ya kweli, ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na amani kwa kuanzia katika familia, jumuiya, nchini mwao na hatimaye, Ulimwengu mzima. Wajifunze kutunza ukimya ndani mwao, ili kuonja amani ya ndani ambayo Kristo Yesu aliwahidia wafuasi wake akisema: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu wala msiwe na woga.” Yn 14:27.
Mtakatifu Francisko wa Assisi anatambulikana kuwa kwa asili yake alikuwa ni mtu wa furaha, aliyependa na kuwathamini maskini sanjari na mazingira nyumba ya wote; alikuwa ni mtu mwema aliyetamani kuwaona watu wakitubu na kumwongokea Mungu, ili waonje huruma na upendo wake wa daima, na hatimaye, kuonja furaha ya Mungu, kwa kuvumilia shida na changamoto za maisha kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Jambo hili linawezekana hata kwa vijana wa kizazi kipya, ikiwa kama maisha yao yatasimikwa katika uhusiano wa dhati na Mwenyezi Mungu. Kamwe anasema Baba Mtakatifu Leo XIV furaha ya kweli haipatikani kwenye mitandao ya kijamii na badala yake, vijana wa kizazi kipya watumie muda wao mwingi katika: Sala na tafakari ya Neno la Mungu, katika maisha ya Kisakramenti na matendo ya huruma; watumie muda wao katika masomo na michezo. Matumizi haramu ya dawa za kulevya, unywaji na ulevi wa kupindukia, vitendo vya ngono, uhusiano wa juu juu, uchoyo na ubinafsi pamoja na mambo ambayo ni hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kwa hakika si vyanzo vya furaha ya kweli kama ilivyo pia kwa uzuri wa sura, umaarufu au afya njema, kwani yote haya ni mambo ya mpito! Upendo kwa Mungu na jirani ni chemchemi ya furaha ya kweli na kamwe hawataweza kughafilika kwani wao wanapendwa na kwamba ni watoto wateule wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa vijana kujenga na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa mambo ambayo yatawawezesha kudhibiti maisha yao, mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kugundua siri hii katika maisha yao.
Kimsingi ujumbe wa Mtakatifu Francisko wa Assisi ni kwamba, amani ya kudumu na furaha ya kweli ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Leo hii, Mwenyezi Mungu ana haja ya wamisionari; watu wema na watakatifu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili; Mapadre ambao ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa; Watawa ambao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Ikiwa kama vijana wanahisi ndani mwao wito wa kipadre na kitawa, kamwe wasisite kuitikia wito huu kwa woga na wasi wasi, bali wapige moyo konde na kuitikia wito huu kwa kusema, “Kisha nikamsikia Mwenyezi Mungu akisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekuwa mjumbe wetu?” Nami nikajibu, “Niko hapa! Nitume mimi.” Isa 6:8. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya kujenga uhusiano mwema na mapadre, watawa na marafiki wema, wanaoweza kuwashirikisha siri za maisha yao. Kongamano hili liwe ni fursa muhimu ya kusali, ili kuonja upendo na huruma ya Kristo Yesu katika maisha yao; ni nafasi ya kukutana na kufahamiana na vijana wengine kutoka sehemu mbalimbali za Marekani, ili kwa pamoja waweze kushirikishana ile furaha ya kweli! Baba Mtakatifu Leo XIV anawaweka vijana wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria sababu ya furaha ya waamini: “Causa Nostrae Laetitia” na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume zinazosheheni amani na nguvu.
