Tafuta

Papa Leo XIV amekutana na kuzungumza na Wajumbe wa "Centro de Investigacion y Formacion de Proteccion al Menor Latinoamerica": Umuhimu wa ulinzi, usalama na makuzi ya watoto Papa Leo XIV amekutana na kuzungumza na Wajumbe wa "Centro de Investigacion y Formacion de Proteccion al Menor Latinoamerica": Umuhimu wa ulinzi, usalama na makuzi ya watoto  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Umuhimu wa Ulinzi, Usalama na Malezi Kwa Mtoto

Wawakilishi wa Kituo cha Utafiti na Mafunzo Kuhusu Ulinzi wa Mtoto kutoka katika nchi mbalimbali za Amerika ya kusini Jumanne tarehe 11 Juni 2026 wamekutana na kuzungumza na Papa Leo XIV mjini Vatican. Kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni muhimu kukazia: Ukweli na uwazi; toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ili kuunda mazingira salama ya malezi na makuzi ya watoto

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wawakilishi wa Kituo cha Utafiti na Mafunzo Kuhusu Ulinzi wa Mtoto kutoka katika nchi mbalimbali za Amerika ya kusini “Centro de investigación y formación de Protecctión al Menor, CEPROME”, Jumatano tarehe 17 Juni 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican. Kanisa linapaswa kuonesha ujasiri kwa kusimama kidete kulinda na kutetea maisha na utume wake. Liwe tayari kuanzisha mfumo utakaolisaidia kurekebisha kasoro na mapungufu ya kibinadamu yaliyojitokeza kiasi cha kusababisha kashfa kama ilivyo wakati huu, kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Ukweli na uwazi; toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Papa Leo XIV akutana na wajumbe wa CEPROME, mjini Roma
Papa Leo XIV akutana na wajumbe wa CEPROME, mjini Roma   (ANSA)

Mama Kanisa kwa kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwalinda watoto wadogo, kumelifedhehesha sana mbele ya walimwengu, sasa ni wakati wa kujikita katika utume wake na kutenda haki sanjari na kuhakikisha kwamba, Jumuiya za Kikanisa zinakuwa ni mahali salama pa malezi na makuzi ya watoto wadogo na vijana na kwamba, hii ni dhamana na wajibu nyeti sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tajiriba ya kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao, tayari kuanza safari ya toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Papa Leo XIV akiingia Ukumbini kuzungumza na wajumbe wa CEPROME
Papa Leo XIV akiingia Ukumbini kuzungumza na wajumbe wa CEPROME   (ANSA)

Hii ni changamoto inayotekelezwa kwa sasa kwa njia ya uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kuonja na kuguswa na upendo wa Kristo Yesu usiokuwa na kikomo, kwanza kabisa kwa waamini kutoa nafasi kwa Kristo Yesu katika maisha yao. Mkutano huu, unawawezesha waamini kuwa na mtazamo mpana zaidi unaosimikwa katika upendo na uhuru kamili na kinyume chake ni kwa waamini kutumbukia katika kashfa na hivyo kuibua madonda makubwa katika maisha ya watu; mambo yanayokwamisha ukuaji wa mtu kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaonya wawakilishi wa Kituo cha Utafiti na Mafunzo Kuhusu Ulinzi wa Mtoto kuhakikisha kwamba, wao wenyewe hawageuki na kuwa ni sehemu ya kashfa hii mbaya katika maisha na utume wa Kanisa akifanya rejea kutoka kwa Kristo Yesu aliyewaonya wafuasi wake juu ya kuwakosesha wengine. “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.” Mt 18:6.

Ulinzi na usalama wa watoto na dhaifu ni muhimu sana
Ulinzi na usalama wa watoto na dhaifu ni muhimu sana

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema wakati wa hija yake ya Kitume nchini Hispania alipata nafasi ya kukutana na kusikiliza shuhuda juu ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizofanywa na wale waliopewa dhamana ya ulinzi, malezi na makuzi yao na kwamba, Kanisa kwanza kabisa linapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Kusikiliza, kwa kutafuta ukweli; kwa kutenda haki sanjari na kulipa fidia pamoja na Kanisa kuendelea kujikita katika mchakato wa ulinzi na utunzaji dhamana na jukumu la viongozi wa Kanisa wakiwa katika mstari wa mbele, lakini hii ni dhamana ya Kanisa zima na kwamba kama wawakilishi hawa wamejitwika dhamana na wajibu wa kuwa ni wataalamu waliotalaumiwa katika tafiti na ulinzi wa Mtoto. Baba Mtakatifu Leo XIV anawatia shime kusonga mbele katika utume huu, kwa kuendelea kujenga na kuimarisha mitandao ya ushirikiano kati ya Makanisa mahalia, pamoja na Taasisi za kiraia, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa kuzuia na kuwahudumia watoto wadogo na watu dhaifu katika jamii. Ni matumaini halali ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, kila eneo ndani ya Kanisa, liwe ni katika maumbile halisi au katika mfumo wa kidigitali, liwe kweli ni mahali pa watu kukutana na Kristo Yesu, anayewakomboa kutoka katika hofu na wasi wasi; hali ya kudhaniana vibaya na kutojali. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatakia heri na baraka katika maisha na utume wao pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kushirikisha Kanisa zima katika mchakato wa ulinzi wa Mtoto.

Ulinzi wa Mtoto

 

17 Juni 2026, 14:57