Papa Leo XIV:Askofu awe Baba kwa Padre na Padre amwone mwenzake kama ndugu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tumeitwa kujenga uhalisia mpya kupitia mazungumzo ya heshima na matumizi ya lugha mpya. Ni kwa kushiriki mambo yote mema katika urithi wetu, kila mmoja akichangia mchango wake mwenyewe, ndipo tunaweza kujenga uhalisia mpya ambapo imani inaweza kuota mizizi mirefu. Ili kufanya hivyo, kimantiki, ni lazima tuanze kwa kujifunza lugha ya kila mmoja wetu, kuanzisha michakato na kujenga vifungo ambapo mbegu za Ufalme zinaweza kupandwa. Haya na mengine yamo katika hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV, katika siku ya Tatu ya ziara ya Kitume ya nchini Hispania, Jumatatu tarehe 8 Juni 2026 alipokutana na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Hispania(CEE) huko Madrid, muda mfupi baada ya Mkutano na Bunge nchini humo. Kwa hiyo alikaribishwa na Askofu Mkuu Luis Javier Argüello García wa Valladolid, Rais wa Baraza la Maaskofu nchini humo ambaye kabla ya Hotuba yake alitoa utangulizi.
Tumeitwa na Bwana kulinda umoja na kuhamasisha mazungumzo na kuponya
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake aliwaeleza kuwa nguvu ya Kanisa haitokani na ukuu wa rasilimali zake, bali kutokana na utakatifu wa watoto wake, kutokana na ushirika wa wachungaji wake, na kutokana na uaminifu mnyenyekevu na wa kudumu wa wale wanaojiruhusu kuongozwa na Roho. Papa aliewatia moyo katika imani na kujitolea kwao licha ya changamoto nyingi, akikisitza kuwa “tumeitwa kulinda umoja, kuhamasisha mazungumzo, kuponya migawanyiko na kusindikiza katika safari ya watu waliokabidhiwa uangalizi wenu." Katika maelezo yake, Papa aliwakumbusha kwamba kwamba: “ni Bwana anayetuongoza na ambaye ni Mwalimu wa historia na wa kila moja ya historia zetu. Ni yeye anayeamua mdundo. Tunatembea nyuma Yake; kiu, tunatembea Naye kama viungo vya mwili mmoja."
Katika wakati wenye mipasuko,Kanisa litoe ushuhuda
Baba Mtakatifu alisisitiza kwamba “Uhusiano huu unadai kwamba Kanisa, katika wakati huu wa kuongezeka kwa mgawanyiko litoe ushuhuda wa umoja katika utofauti. Kwa njia hiyo alitoa mwito wa Kanisa nchini Hispania kuhamasisha ushirika wenye uwezo wa kukumbatia utajiri wa karama, na hisia, na akasisitiza kwamba katika kazi hii, huduma ya Askofu inachukua umuhimu maalum. "Tumeitwa kuwa ishara inayoonekana ya ushirika: kwanza kabisa, ushirika na Kristo, tukilinda kwa upendo imani tuliyopokea, kwa unyenyekevu kwa Neno la Mungu na kwa Mapokeo hai ya Kanisa. Hili linahitaji kuishi kwa uwazi katika ushirika na Mrithi wa Petro na Kanisa la ulimwengu wote, pamoja na wazee wa Kanisa na jumuiya ya Jimbo yenyewe, pamoja na maisha yaliyowekwa wakfu, pamoja na harakati, pamoja na vyama, na kila karama halisi ambayo Roho hutoa kwa ajili ya manufaa ya wote."
Maaskofu waendeleze umoja
Baba Mtakatifu Leo XIV alisisitiza kuwa Maaskofu hao waendeleze umoja na kuwasindikiza watu wao, ili kuchangia nguvu ya umisionari. Kanisa ambalo lina amani ya ndani linaweza kuzungumza kwa uhuru zaidi na kaka na dada wa madhehebu mengine ya Kikristo na dini zingine, kwa wale wasioamini, kwa mamlaka ya kiraia, na kwa watu wote wenye mapenzi mema wanaofanya kazi kwa manufaa ya wote Baba Mtakatifu pia aliwasihi kukaa karibu na vijana, waseminari na walio katika mazingira magumu. Hapo awali, Papa alisema “tulitaja mizigo mizito. Mahujaji katika safari ya ya Santiago wanajua vyema kwamba vitu muhimu tu vinavyopaswa kubebwa kwenye mkoba. Kama Papa Francisko alivyosema mara nyingi, katika muktadha wa sasa wa kitaaluma, uhifadhi wa miundo hauwezi kupewa kipaumbele kuliko mema ya wito wenyewe. Waseminari wana haki ya malezi bora iwezekanavyo, na Kanisa, kwa upande wake, lina haki ya mapadre waliohitimu vizuri. Kigezo cha seminari kuwa nyumba halisi za malezi ni kwamba zinahakikisha uzoefu wa kutosha wa maisha ya jamii; kwamba zina walimu waliojitolea kikamilifu kusoma na kufundisha, wenye uzoefu katika kusindikiza kiroho; na kwamba wana vituo vya elimu ya juu ya taalimungu, vilivyo na vifaa muhimu vya kutimiza utume wao. Kwa lengo hilo, ni muhimu sio tu kuunganisha nguvu bali pia kujifunza kufanya kazi pamoja katika kudhibiti changamoto hizi.”
Magumu yanaweza kuonekana fursa
Katika nyanja hiyo, Baba Mtakatifu Leo XIV alisema magumu yanaweza kuonekana kama fursa. Wakati mwingine, tunaona ni vigumu kuelezea wito wa walei na ujumuishaji wao katika safari hii ya maisha ambayo sisi kama Kanisa tunaifanya. Kwa upande mwingine, tunaona jinsi katika huduma nyingi, ambazo kwa kawaida husimamiwa na watawa, washirika wa kawaida wanavyoitwa kuendelea na kazi. Ni ugumu ambao tunaweza kuubadilisha kuwa fursa ya kukutana, mazungumzo na mawasiliano. Ni juu yetu kuhakikisha kwamba watu hawa wa kawaida wanaelewa ushiriki wao katika huduma hii ya kikanisa kama wito kutoka kwa Mungu wa kuchukua jukumu lao kama Wakristo, wakiingiza roho ndani na kuhisi sehemu ya utume ambao Bwana aliwakabidhi watawa waliouanzisha.”
Hispania ni nchi ya Maria
Papa aliendelea kukumbusha kuwa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliita Hispania "Nchi ya Maria." Akimtaja Bikira Maria kama mama wa ushirika na matumaini, na hivyo Maaskofu wana Mwenza wao wa kwanza katika safari na hazina yao kubwa zaidi. Maria, anawaonesha wamini jinsi ya kukaribisha Neno na kuliweka mioyoni mwao, kuongozana na wanafunzi katika njia yao, na kubaki kuwepo katika safari yote ya Kanisa. Na kwake Papa Leo XIV alisema "Ninamkabidhi huduma yenu ili aweze kuwasaidia katikati ya watu waliokabidhiwa uangalizi wenu.”
Mfano wa Mtakatifu Yohane wa Avila kwa Mapadre
Papa pia alikumbuka kwamba mwaka huu 2026 unaadhimisha miaka mia tano ya kuwekwa wakfu kwa Mtakatifu Yohane wa Avila, Msimamizi wa Hispania. Alikumbusha kwamba Mtakatifu Paulo VI alimtaja kama "mwalimu mkarimu na mwenye busara wa maisha ya kiroho, mrekebishaji wa mfano wa maisha ya kikanisa na tamaduni za Kikristo na, wakati huo huo, Padre rahisi." Kama mwalimu huyu mtakatifu wa Kanisa, Papa Leo alisema, Kanisa “linatambua maisha ya kikuhani ambayo kila Askofu ameitwa kuyalinda na kuyakuza ndani ya wazee wake.” Katika muktadha huo, Papa Leo XIV alisema kwamba marafiki wa karibu wa Maaskofu katika safari hii ni 'mapadre rahisi,' kwa maana ya juu na inayohitaji sana ya neno hilo, ambao"wanampenda Kristo, wamejikita katika sala, waaminifu kwa Kanisa, wako karibu na watu, na wenye uwezo wa kuunganisha mafundisho sahihi, bidii ya kitume na upendo wa kichungaji."
"Askofu awe Baba kwa Padre na Mapadre waonane kama ndugu wa kushirikishana magumu"
Baba Mtakatifu Leo XIV alisisitiza kwamba mpadre wanapaswa kupata kutoka kwa Askofu wao sio tu mamlaka inayotambulika, bali baba anayesindikizana nao, na kwa mapadre wenzao wawaone kama ndugu ambao wanaweza kushirikishana magumu na furaha ya hija hii iliyojaa mikutano, na ambayo sisi sote tunamtafuta Kristo.” Kwa kuhitimisha Papa aliomba amalizi na sala kutoka kwa Mtakatifu ambaye aliwakumbusha waamini kwamba kila ufufuko wa Kanisa huzaliwa na moyo unaofanana na Kristo, aliposema, "Ukiniamuru, Bwana, kufanya ulichofanya, nipe moyo wako (Mahubiri 57:20)”. Kwa hivyo Papa alisema “Hili pia liwe ombi letu: Bwana, tupe moyo wako, moyo unaoweza kuinua macho yako kwako, wa kuanza safari, wa kusikiliza, wa kutambua, wa kutumikia, wa kurekebisha kwa upendo, wa kuhudhuria kwa uvumilivu na wa kutangaza kwa furaha. Kwa maana Kanisa linalopokea moyo wa Kristo hubeba nguzo ya moto inayoliongoza, inayolitegemeza, inayolitetea na kulifariji, vitu muhimu vya kukabiliana na changamoto yoyote.”
Muhimili wa Baraza la Maaskofu Hispania
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Hispania katika salamu zake alieleza juu ya kiungo cha Baraza la Maaskofu kwamba kinahesabu Majimbo 69, yanayounganisha Kanda 14 za Kikanisa, Uaskofu Mkuu wa Kijeshi na katika Uaskofu wa Wakatoliki wa Mashariki. Kisha Rais wa maaskofu alikumbusha Ziara ya kwanza ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Hispania mnamo 1982, mwaka ambao uliashiria mwanzo wa maendeleo ya Baraqz ala maaskofu hao (EEC) ya mwelekeo wa pamoja na miongozo ya kichungaji. Tangu wakati huo, hati kumi na mbili zimefuata, ikiwa ni pamoja na ya hivi karibuni kwa miaka ya 2026-2030, yenye kichwa "Poneos en camino!" “Enendeni” (Luka 10:3). Leo hii "wasiwasi wa uinjilishaji unaendelea, kwa umakini mkubwa kwa tangazo la kwanza na kuanzishwa ukristo, sherehe za kila dominika, na uwepo wa umma."
Msisitizo mkubwa" umewekwa "katika kuhamasisha maisha kama wito na juu ya utekelezaji wa ushirika wa kimisionari katika uwajibikaji tofauti na watu wote wa Mungu, kama ilivyoombwa na Sinodi kuhusu Sinodi," ambayo hati yake ya mwisho Kanisa la Hispania linatekeleza. Hatimaye, akitaja kauli mbiu ya Ziara ya kitume ya Papa Leo XIV nchini Hispania, Alzad la mirada, yaani kuinua Macho ambapo Askofu Mkuu huyo alisema alikuwa na uhakika kwamba uwepo wa Papa utasaidia Kanisa "kuinua macho yake kwa Yesu Kristo na kufanya upya furaha ya kuwa wanafunzi wapendwa na wamisionari wenye bidii wa huruma ya Mungu."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.
