Tafuta

Papa Leo XIV kwa Kanisa la Visiwa vya Kanari:Kristo ndiye kitovu cha maisha ya Kikristo

Papa Leo XIV kwa Kanisa la Visiwa vya Kanari atoa wito wa kuendeleza umoja kupitia Msalaba na pamoja na kuimarisha ibada ya kuabudu Ekaristi.Lakini pia kuendelea na kuwahudumia walio katika mazingira magumu kwa mshikamano na matumaini.Ni wakati wa kukutana maaskofu,mapadre,mashemasi,watawa, waseminari na wahudumu wa kichungaji katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Anna huko Las Palmas de Gran Canaria,Juni 11,2026.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu mara baada ya Mkutano katika Kisiwa kikubwa cha Kanari  na wanahusika na wahamiaji, Alhamisi tarehe 11 Juni 2026 alikutana na maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa, waseminari, na wahudumu wa kichungaji katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Anna huko Las Palmas de Gran Canaria. Mkutano huo ni katika hatua yake ya mwisho ya Zara yake ya kitume nchini Hispania. Katika hotuba yake Papa alikazia juu ya uhamiaji, changamoto za kijamii, na jukumu la Kanisa katika kusindikiza jamii zilizo katika mazingira magumu.

Papa katika Kanisa Kuu
Papa katika Kanisa Kuu   (@Vatican Media)

Visiwa vya Kanari vimekuwa moja ya sehemu kuu za kuingia Ulaya kwa wahamiaji wengi sana wanaosafiri kutoka Afrika Magharibi, na jumuiya za Kanisa mahalia zimekuwa na jukumu muhimu katika kutoa msaada wa kibinadamu na kichungaji. Katika hotuba yake  kwa waliokuwa  katika Kanisa kuu, Papa Leo XIV aliwashukuru kwa ushuhuda wao kwa kile alichokielezea kama "Kanisa lililo hai," linaloakisi "furaha na matumaini, huzuni na uchungu wa watu wa wakati wetu, hasa wale ambao ni maskini au wanaoteseka." Papa alisema jinsi alivyofika huko visiwani akiwa kama "kama baba na ndugu katika imani," akikumbuka maneno aliyosema mwanzoni mwa upapa wake: "Mimi ni Mkristo pamoja nanyi, na kwa ajili yenu, mimi ni Askofu."

Shuhuda
Shuhuda   (@Vatican Media)

Akitafakari usomaji wa siku hiyo kutoka Barua kwa Waefeso, Baba Mtakatifu alisisitiza umuhimu wa kutambua karama na huduma tofauti ndani ya Kanisa na kuzitumia kujenga umoja. "Wito wa Bwana unasikika upya mioyoni mwetu leo ​​na unathibitisha wito na utume wetu: kujenga Kanisa pamoja, lililojengwa juu ya Kristo, 'jiwe la pembeni'," alisema. Aliwahimiza waamini wote "kujenga juu ya yaliyo mema, kuoanisha tofauti zetu na kufanya kazi pamoja kwa ajili ya mema ya wote." Papa avile vile alizungumzia mitazamo miwili ambayo alisema ni muhimu kwa Wakristo wanaotafuta kuwa "wasanifu wenye busara" katika kujenga kile alichokiita "ustaarabu wa upendo."

Kusikiliza shuhuda
Kusikiliza shuhuda   (@Vatican Media)

La kwanza lilikuwa ni kukumbatia Msalaba wa Kristo. Akitumia taswira ya bahari inayozunguka Visiwa vya Kanari, alibainisha kuwa ingawa bahari inaakisi nyumbani na kumilikiwa, inaweza pia kuashiria changamoto, umbali, na kutokuwa na uhakika. Akimnukuu Mtakatifu Agostino wakati huo, alikumbuka kwamba wanadamu wanatamani nchi yao ya kweli lakini lazima wavuke "bahari ya ulimwengu huu" ili kuifikia kutuonesha njia, Yule ambaye tulitamani kumwendea alikuja mwenyewe. "Hakuna mtu anayeweza kuvuka bahari ya ulimwengu huu isipokuwa wamebeba msalaba wa Kristo." Papa Leo XIV alisema watakatifu wanatoa mfano wa jinsi ya kukabiliana na magumu ya maisha kwa kumwamini Kristo. "Walipokabiliana na dhoruba za maisha, walijua jinsi ya kumchukua Yesu kwenye mashua zao; walimwamini, wakakumbatia msalaba na hivyo kutuliza mawimbi ya kutokuwa na uhakika na hofu."

Papa aliwahutubia Kanisa la Visiwa vya Kanari
Papa aliwahutubia Kanisa la Visiwa vya Kanari   (@Vatican Media)

Mtazamo wa pili uliokisiwa  na Papa Leo XIV ulikuwa ni hitaji la kukuza hali ya ibada ya  kiroho ya Ekaristi. Baba Mtakatifu airejea utamaduni wa muda mrefu wa kutumia  maua na kutupa mbele ya Sakramenti Takatifu wakati wa sherehe za Kupaa kwa Bwana, akiuelezea kama ukumbusho kwamba Kristo ndiye kitovu cha maisha ya Kikristo. "Katika hija yetu, lengo ni kukutana na Kristo; yeye ndiye kitovu cha maisha ya Kikristo, ambaye tunapiga magoti mbele yake kwa ibada, ambaye tunakusanyika karibu naye ili kuunda mwili mmoja," alisema.

Ndani ya Kanisa Kuu wakimsikiliza Papa Leo XIV
Ndani ya Kanisa Kuu wakimsikiliza Papa Leo XIV   (@Vatican Media)

Kisha akinukuu Lumen Gentium ya Mtaguso wa Pili wa Vatican, Papa alisisitiza kwamba kushiriki katika Ekaristi huimarisha umoja wa Kanisa na kunapaswa kuwaongoza waamini kwenye hisia ya kina ya ushirika. "Kukuza hali ya kiroho ya Ekaristi kunamaanisha kuchunguza zaidi 'hali ya kiroho ya umoja wa kikanisa katika upendo,'" alisema. Kwa kuhitimisha hotuba yake, Papa Leo XIV alibainisha kwamba  Kanisa mahalia lipate  nguvu kutokana na ushuhuda wa wanaume na wanawake wengi watakatifu ambao wameunda historia ya Ukristo katika Visiwa vya Kanari.

Papa alikariibishwa na Askofu wa Jimbo hilo
Papa alikariibishwa na Askofu wa Jimbo hilo   (@Vatican Media)

Aliwahimiza waamini kubaki wameungana katika imani, matumaini, na upendo, akielezea fadhila hizo, kwa maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kama "nyota tatu zinazoinuka angani ya maisha yetu ya kiroho ili kutuongoza kwa Mungu." Akiwakabidhi Kanisa katika Visiwa vya Kanari kwa Bikira Maria chini ya jina "Stella Maris",yaani  Nyota ya Bahari, Papa aliwahimiza Wakatoliki kuendelea na utume wao kwa kujiamini, akimwomba Roho Mtakatifu neema ya kubaki wameungana na waaminifu katikati ya changamoto za wakati huu.

Papa wakati akielekea Kanisa Kuu
Papa wakati akielekea Kanisa Kuu   (@Vatican Media)
PAPA AKUTANA NA KANISA LA KANARI

KANISA LA VISIWA VYA KANARI

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

11 Juni 2026, 17:53